2016-05-24 09:13:00

Kuna watu wanateseka na kunyanyasika sana duniani!


Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ambalo halijawahi kutokea tangu baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Jumuiya ya Kimataifa inawajibu wa kuhakikisha kwamba, inapunguza hadi kufikia nusu ya idadi ya wakimbizi, ifikapo mwaka 2030. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya watu millioni 60 ambao wamelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali.

Kati yao kuna watu wasiokuwa na makazi maalum ndani ya nchi zao wapatano millioni 40 na wengine millioni 20 ni wakimbizi. Umoja wa Mataifa unakiri kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 130 wanaohitaji msaada wa dharura kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuendelea kuishi! Wakimbizi na wahamiaji wanategemea kwa kiasi kikubwa msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Haya yamesemwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon wakati akifungua mkutano wa kwanza wa msaada wa kiutu kimataifa unaoendelea huko Istanbul, nchini Uturuki, Jumatatu, tarehe 23 Mei 2015.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anazitaka nchi ambazo kwa sasa ziko katika migogoro na kinzani za kivita kuheshimu sheria za kimataifa. Kwa mfano nchini Syria, hata hospitali zinaendelea kulipuliwa kwa mabomu. Mkutano huu unahudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali 65 na Vatican inawakilishwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Jumla kuna wawakilishi 600 kutoka katika nchi na mashirika ya misaada kimataifa. Huu ni mkutano wa siku mbili unaopembua kwa kina na mapana chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii inayojitokeza kutokana na vita au athari za mabadiliko ya tabianchi.

Lengo kuu kwa sasa ni Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, waathirika wa majanga haya wanapata mahitaji yao msingi; umuhimu wa kujikita katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu na elimu kwa mamillioni ya watoto ambao wanapaswa kuwa darasani lakini kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii wanajikuta wanashindwa kwenda shuleni. Mkutano huu umeandaliwa na Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka mitatu.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inawajibika na kutekeleza dhamana yake kikamilifu, kwani kwa sasa kuna nchi ambazo zinaelemewa na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Kwa upande wake Angela Merkel amekiri kwamba, mtandao wa msaada kimataifa kwa sasa hivi haufanyi kazi, kumbe, kuna haja ya kuibua mbinu mkakati mpya ili kuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali katika maisha yao. Jambo la pili anasema, Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikipitisha ajenda za misaada pasi na kutoa fedha inayohitajika katika kufanikisha malengo yaliyokubaliwa na Jumuiya ya Kimataifa. Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba,  Jumuiya ya Kimataifa inakidhi mahitaji ya mtu mzima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.