2016-05-24 11:39:00

Elimu ni ufunguo wa mafanikio katika majadiliano ya kidini!


Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kwa namna ya pekee na waamini wa dini ya Kiislam ambao wanamwabudu Mungu mmoja, mwenye uhai na mwenye kuwepo, Rahim na Mwenyezi; Muumba wa mbingu na dunia, aliyenena na wanadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha upatanisho, haki na amani; changamoto inayohitaji ushirikiano na mshikamano wa dhati na waamini wa dini mbali mbali duniani. Hii ni changamoto pia ya kuondokana na ubaguzi, hali ya kutovumiliana pamoja na misimamo mikali ya kiimani, ambayo imekuwa mara nyingi ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao.

Katika mchakato huu, waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushikamana ili kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidhamiri mambo msingi katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano katika jamii. Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, tukio la Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Sheikh Ahmad Muhammad Al Tayyib, Imam mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, Cairo, Misri, Jumatatu, tarehe 23 Mei 2016 ni tukio la kihistoria linalopania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Kanisa Katoliki na waamini wa dini ya Kiislam.

Viongozi na waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kujikita katika mchakato wa kutafuta, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho; kwa kukataa vita na matumizi ya nguvu; kwa kupinga kwa nguvu zote vitendo vya kigaidi pamoja na kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinaheshimiwa. Mambo yote haya yanapaswa kuvaliwa njuga kwa njia ya elimu makini, ili kusaidia kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali anasema, Kardinali Jean Lous Tuaran.

Mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Sheikh Al Tayyib umekuwa ni ujumbe wa matumaini kwa Familia ya Mungu huko Mashariki ya kati, kwamba, waamini wa dini mbali mbali wanaweza kuishi kwa amani, upendo na mshikamano wa dhati. Hapa kuna haja ya kuunganisha utashi na mapenzi mema ya waamini ili waweze kutambua kwamba, umoja, upendo na mshikamano ni chachu ya ustawi na maendeleo ya wengi!

Waamini wote wanahitajiana ili kukamilishana katika mchakato wa maisha. Waamini wa dini mbali mbali wajitaabishe kufahamiana, ili kuondokana na mawazo mgando, ambayo kimsingi ni chanzo cha machafuko mengi ya kidini sehemu mbali mbali za dunia. Vitendo vya kigaidi katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, vimechafua sana kurasa za majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam. Hapa dini zinapaswa kuwekeza zaidi katika masuala ya elimu na utamaduni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi kwa sasa na kwa siku za usoni! Kuna matumaini ya kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Chuo kikuu cha Azhari, Cairo, Misri, ili kufufua Tume ya pamoja iliyoundwa kunako mwaka 1998.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.