2016-05-24 10:35:00

Askofu Ndorobo ashuhudia "Live" Padre wake akipambana kijasiri Roma!


Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Muasisi wa taifa la Tanzania ni zawadi, hazina na utajiri mkubwa kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania na Afrika katika ujumla wake kutokana na mchango wake mkubwa uliosaidia kuunda umoja wa kitaifa unaojikita katika udugu, mshikamano na upendo kwa kutambua na kuthamini tunu msingi za maisha ya kiafrika. Kutokana na mchango wake, Kanisa nchini Tanzania linachangamotishwa kuhakikisha kwamba, linawajengea uwezo wa waamini walei ili kuweza kushiriki kikamilifu katika Unabii wa Kristo kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha!

Kanisa linahitaji waamini walei ambao ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Hapa waamini walei wanapaswa kutambua na kuthamini utambulisho wao, nafasi na utume wao katika maisha ya Kanisa. Hapa waamini wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kadiri ya nafasi, karama na vipaji vyao mintarafu sheria, kanuni, taratibu na maisha ya Kanisa mahalia. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kuwa na majiundo awali na endelevu katika: Biblia; Katekisimu na Mafundisho Jamii ya Kanisa, mambo msingi yanayoweza kutumiwa na waamini walei katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu!

Kwa ufupi haya ndiyo yaliyojiri katika utetezi wa kazi ya Padre Onesmo Jeremiah Mnyang’ali kutoka Jimbo Katoliki la Mahenge, Tanzania kama sehemu ya mchakato wa kuhitimisha masomo ya Shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma, Jumatatu, tarehe 23 Mei 2016. Padre Onesmo alionesha umahiri kwa kutetea kikamilifu kazi yake, tukio ambalo limeshuhudiwa “LIVE” na Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge, Tanzania.

Katika mahojiano mafupi na Radio Vatican, Askofu Ndorobo alifurahishwa na kuguswa kwa namna ya pekee kuona jinsi ambavyo Padre Onesmo alivyojiandaa vyema kwa kushirikiana kikamilifu na Majaalimu wake: Prof. Saldhana Peter Paul, Prof. Egbulefu John Okoro pamoja na Prof. Tata Gaston Gabriel, kiasi cha kukubali, kupitisha na hatimaye kutetea kazi yake kwa ujasiri, ari na moyo mkuu.

Askofu Ndorobo anawataka wanajimbo na watanzania wengine wote waliotumwa na Maaskofu pamoja na viongozi wao mahalia kuhakikisha kwamba wanasoma kwa bidii na juhudi ili kujipatia ujuzi na maarifa tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Familia ya Mungu nchini Tanzania. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni masomo. Hata katika changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha yao, wawe na ari, moyo mkuu na matumaini kwa Mungu anayewawezesha katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.