2016-05-23 11:52:00

Kukua na kupanuka kwa tasnia ya mawasiliano Tanzania na changamoto zake!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake katika maadhimisho ya Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa hapo tarehe 8 Mei 2016 anasema, matumizi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuwa ni njia sahihi ya mawasiliano ya kibinadamu, ikiwa kama mwanadamu atakuwa na uwezo wa kutumia vyema mitandao hii ya kijamii, kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema ya kijamii; kwa kutafuta na kuendeleza mafao ya wengi. Mitando ya kijamii isipotumiwa vyema inaweza kuwa ni sababu ya mipasuko na kinzani za kijamii. Mazingira ya digitali ni jukwaa na mahali ambapo watu wanaweza kuonjeshana upendo, kuganga na kuponya madonda; mahali pa majadiliano yenye tija na mashiko au jukwaa la “wachovu” wa maadili na utovu wa nidhamu.

Hivi karibuni, Waziri mkuu wa Tanzania Kassim M. Majaliwa alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali ya Tanzania kwa mwaka 2015/2016 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017, alikiri kwamba, Serikali ya Tanzania inatambua kwamba, sekta ya habari ni nguzo muhimu katika kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha umma. Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Tanzania imeendelea kusimamia sekta ya habari kikamilifu na kuhakikisha vyombo vya habari vinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia: Sheria, Kanuni, Maadili na Weledi.

Alisema, uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania ni mkubwa na wigo wa ushiriki wa sekta binafsi umeongezeka sana. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016 Serikali ya Tanzania ilikuwa imesajili vituo vya Televisheni 26, Vituo vya Radio 126 na Magazeti 833. Waziri mkuu Kassim M. Majaliwa alikaza kusema, jambo la muhimu hapa ni matumizi mazuri ya kalamu na kuweka uzalendo wa nchi mbele!

Serikali ya Tanzania katika kipindi cha mwaka 2016/2017 itawasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari. Aidha itaboresha Idara ya habari - maelezo ili itimize jukumu lake kama Msemaji mkuu na Mratibu wa mawasiliano Serikalini. Vile vile itaendelea kufuatilia kwa karibu maudhui ya vituo vyote vya utangazaji kupitia mtambo maalum wa ufuatiliaji wa maudhui na kuhakikisha vituo vya utangazaji vinakuwa na wakalimani wa lugha ya alama. Alivitaka vyombo vya habari nchini Tanzania kufanya kazi zake kwa weledi, kwa mujibu wa sheria, maadili na taratibu za nchi; mambo msingi katika tasnia ya habari.

Hii ndiyo changamoto kubwa iliyoko kwenye tasnia ya habari, kama ambavyo imefafanuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2016! Vyombo vya mawasiliano ya jamii viwe ni madaraja ya kuwakutanisha watu ili kuitajirisha jamii husika; watu wawe makini kwa maudhui yanayotolewa kwenye vyombo vya habari ili yasaidie kuganga na kuponya makovu ya utengano, kinzani na mipasuko ya kijamii na kidini, ili kujenga msingi wa haki, amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Wakati huo huo, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Robert Makaramba amemwakilisha Jaji Mkuu katika kongamano la siku ya Uhuru wa Habari Duniani katika ukumbi wa Malaika Beach Resort Jijini Mwanza, Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 3 Mei 2016 imeadhimisha Siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Akisoma hotuba, kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman alisema kuwa, ni nia ya Mahakama kuona kuwa Uhuru wa kupata habari na vyombo vya habari unapewa kipaumbele kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo. Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa vyombo vya Habari ni nguzo muhimu sana katika kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu. “Katika jamii yoyote ya kidemokrasia,vyombo huru vya habari ni silaha muhimu sana katika kurahasisha utawala bora na maendeleo” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa, kwa kutambua changamoto za upatikanaji na utoaji wa taarifa,kote kwa watumishi wa Mahakama na waandishi wa habari, Mahakama imechukuwa hatua kadha kuleta mahusiano mema na vyombo vya habari. Mahakama kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) yalianzishwa mafunzo maalum kwa waandishi habari wanaondikia Mahakama yakilenga namna bora ya kuripoti habari za Mahakama na matunda yake tumeanza kuyaona kwa kufuatilia habari mbalimbali katika vyombo vya Habari. Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Vyombo vya Habari kusini mwa Afrika (MISA) imeanzisha mafunzo maalum yahusuyo upatikaji na utoaji wa taarifa na huduma kwa wateja kwa watumishi wa kada mbalimbali za Mahakama. “Mtaona kuwa kwa uhakika juhudi hizo kwa kiasi kikubwa zinaendana na dhima ya siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari nchini  Tanzania‘’ alisisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu alitoa changamoto zilijitokeza wakati wa kuripoti uchaguzi mkuu kwa mwaka 2015 kwa baadhi ya vyombo vya Habari kuegemea na kuonesha mapenzi binafsi na vyama au wagombea Fulani. “Ni tabia ya baadhi ya vyombo vya habari kutumia matusi, kashfa na maneno ya kejeli ni ya kawaida kwenye jamii, ambayo viwango vya weledi vinazingatia ukweli, usawa na kuwajibika havijahafikiwa”  alifafanua Jaji Mkuu. Mhe. Jaji Mkuu alimalizia kwa kusema kuwa Mahakama inaamini haki za msingi za kujieleza,kujihusisha na uhuru wa vyombo vya habari, na haki ya kupata taarifa kama katiba invyosema.Mahakama inaamini kuwa uwepo wa sheria nzuri za vyombo vya habari na upatikaji wa taarifa ni chachu kubwa ya maendeleo katika nchi.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.