2016-05-23 09:34:00

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ufunuo wa huruma ya Mungu!


Leo Kanisa zima liaadhimisha ukuu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Maneno ya antifona ya mwaliko katika adhimisho hili yanatuambia kwamba: “Asifiwe Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu kwa sababu ametufanyizia huruma yake”. Tunafunuliwa sifa hii ya Mungu anayejitambulisha katika Utatu yaani Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Hivi ndivyo tunafundishwa na kufunuliwa juu ya Mungu wetu na hii ndiyo imani yetu, imani tunaona fahari kuikiri kila mara.

Fumbo hili la Utatu Mtakatifu ni fumbo ambalo linamstaajabisha na hata kumweka mwanadamu na kwa ndani zaidi linatuweka sisi wakristo daima katika maswali. Pengine tunakumbana na changamoto nyingi za kushuhudia juu ya hiki tunachoamini ila maneno yetu yanaonekana kutokidhi haja za wao watuulizao. Ningependa leo hii kutoa tafakari fupi kama msaada kwetu na kutufanya tusiyumbe katika imani yetu. Jambo la kwanza ni kujaribu kuzama na kujiuliza Mungu ni nani kwetu, ukubwa wake upo namna gani na ni jinsi gani akili yetu ya kibinadamu inaweza kuzama na kumuelewa Mungu sawasawa. Kwa hakika Mungu ni mkuu mno kupita uwezo wetu na hekima yake kwetu hatuwezi kuielewa katika ukamilifu wote. Mtunga Zaburi anatuambia kuijua hekima yake tunapaswa kuwa sawa naye.

Barua kwa Waebrania inatuambia kwamba “Mungu ambaye alisema zamani na Baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema nasi katika Mwana, aliyemweka kuwa mirthi wa yote, tena kwa Yeye aliufanya ulimwengu” (Ebr 1:1 – 2). Ufunuo tunaopewa kupitia Neno lake na zaidi katika ukamilifu wake kupitia nafsi ya pili ya Mungu, Yesu Kristo Bwana wetu unatupatia elimu inayotosha kulielewa fumbo hilo. Tunapata uhakika wa Ufunuo huo kwa kuwa Yeye anayetufunulia katika hali ya juu kabisa ni mmoja kati ya nafsi za Fumbo hilo. Sala ya Utangulizi ya Ekaristi, katika Sherehe hii ianelezea Ufunuo huo kwa kifupi kabisa ikisema: “Wewe pamoja na Mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa nafsi, ila katika Utatu wa umungu mmoja. Mambo tunayo yasadiki juu ya utukufu wako, kwa sababu ya ufunuo wako, twayasadiki pia juu ya Mwanao na juu ya Roho Mtakatifu pasipo tofauti ya kutengana”.

Hii ndiyo elimu tunayofunuliwa na Mungu juu ya haiba yake. Sisi wanadamu tunaalikwa kuipokea elimu hii kama ukweli unaofunuliwa kwetu na mwisho uimarishe imani yetu juu ya umoja huu katika Utatu Mtakatifu. Somo la Injili katika adhimisho la leo, Kristo anatufunulia juu ya umoja huo. Roho Mtakatifu anafafanuliwa kwetu kama mwalimu wetu na mwanga wetu wa yale ambayo yamo ndani ya fumbo hilo la Utatu Mtakatifu. “Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari”.

Mwana wa Mungu ni Neno la Mungu na Roho Mtakatifu ni tunda la Upendo uliopo kati ya Baba na Mwana. Tofauti yao katika nafsi inaweza tu kuelezeka katika tofauti ya utendaji wao, Baba anayejidhihirisha katika uumbaji, Mwana katika ukombozi na Roho Mtakatifu katika kulitakatifuza Kanisa. Utendaji wao wote huo unajifungamanisha na Ufunuo wa huruma ya Mungu ambayo ni uthibitisho wa Upendo wake kwa viumbe wake. Ukweli huu unafunuliwa na maandiko matakatifu na kwa hakika ni hapa tunapopata msingi wa kujenga imani yetu katika Utatu Mtakatifu.

Yapo maeneno mengi katika maandiko matakatifu yanayothibitisha umoja huu lakini inatosha tu kuangalia katika nyaraka za mtume Paulo ambapo daima salamu yake na hata namna yake ya kuaga ililitambulisha fumbo hili: “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote” (2Kor 13:14). Hii inatudokezea uwepo wa imani hii tangu mwanzo mwa Kanisa imani ambayo Kristo aliwapatia wafuasi wake kabla ya kupaa kwake kama kitambulisho na tiketi ya kuingia katika imani ya kikristo akiwaagiza akisema “Basi, enendeni,  mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na Roho Mtakatifu”. Ndiyo maana kila mwaka Mama Kanisa anatualika wakati wa mkesha wa Pasaka kukiri upya imani hii na huitimisha kwa kusema kwamba hiyo ndiyo imani yetu tunayoona fahari kuiungama.

Mtume Paulo anatuambia katika somo la pili kwamba “tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa Yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu”. Hilo ndilo jukumu tunalopokea kama wana Kanisa na hasa tunapokuwa tayari kuruhusu kuongozwa na Roho Mtakatifu anayeelezewa na Kristo katika somo la Injili kama kiongozi na mwenye kutukumbusha yale aliyoyafanya Kristo. Ikiwa Kristo ndiye anayetufunulia utendaji wa Fumbo hili la Utatu Mtakatifu basi sisi tulio wafuasi wake tunaalikwa katika utendaji wetu wa kila siku kumkaribisha Roho Mtakatifu kusudi kwa uongozi wake maisha yetu yaufunue Upendo wa Mungu unaomiminwa na Roho huyu tunayepewa.

Hapa kwa namna ya pekee na tunapoadhimisha sherehe hii katika mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu napenda kuyakariri maneno ya Baba Mtakatifu Fransisko anapotuambia katika Bula lake Misericordie Vultus akisema: “Macho yetu yakiwa yamemkazia Yesu anayetutazama kwa huruma, tunaonja upendo wa Utatu Mtakatifu. Utume ambao Yesu ameupokea kwa Baba ni ule wa kudhihirisha fumbo la pendo tukufu katika utimilifu wake. ‘Mungu ni Upendo’ (1Yoh 4:8,16) ... Upendo huu umewekwa wazi na wa kushikika katika maisha yote ya Yesu. Ubinadamu wake si kitu kingine ila upendo, upendo uliotolewa huria. Mahusiano anayoyajenga kati yake na wale watu wanaomwendea yanaonyesha jambo la kipekee na lisiloweza kujirudia. Ishara anazozifanya hasa kwa wenye dhambi, maskini, wale walioko pembezoni, wagonjwa na wanaoteseka, yote ni kwa ajili ya kufundisha huruma. Kila kitu ndani yake kinaongelea huruma. Hakuna chochote kwake kinachopungukiwa na huruma”. (MV, 8) .

Kristo anakuwa kweli kwetu ufununuo wa fumbo hili la Utatu Mtakatifu. Somo la kwanza katika sherehe hii ya leo linamwelezea Yeye kama hekima iliyokuwapo kwa Baba kabla hata ya uumbaji na hekima yenye kujua yote yaliyo mapenzi ya Mungu. “Bwana alikuwa pamoja nami katika njia yake ... nalitukuka tokea milele, tangu awali kabla haijawako dunia”.  Hekima anaendelea kujitambulisha uwepo wake wakati wa uumbaji akisema “ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi”. Utambulisho huu wa hekima unarandana kabisa na utambulisho unaotolewa na Mwinjili Yohane anapomwelezea Kristo akisema: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu ... vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika ... Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana wa pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli” (Yoh 1: 1, 3, 14).

Roho Mtakatifu anayetajwa katika somo la Injili kama Roho wa kweli na atakayetuongoza katika kweli yote anatambulishwa na Yesu kwamba anatoka kwa Baba: “Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea toka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia” (Yoh 15:26). Ni takribani juma moja sasa limepita tangu tulipoadhimisha tukio hilo la Kanisa kushukiwa na Roho Mtakatifu katika Sherehe ya Pentekoste. Roho Mtakatifu alitajwa kwa nafasi mbalimbali ikiwamo ya kuangaza na kutenda ndani ya Kanisa.

Leo hii tunafunuliwa juu ya nafasi nyeti ya nafsi hii ya Utatu Mtakatifu yaani kutufunulia ukweli wa kimungu, kuyajua mawazo ya Mungu na hivyo ni pale tu Kanisa na wanakanisa wanapokuwa wanatenda na Roho Mtakatifu watajaliwa kuzijua siri za ufalme wa Mungu tulizofunuliwa na Kristo katika fumbo la Pasaka. Pengine hata imani yetu katika fumbo la Utatu Mtakatifu itaimarika zaidi pale tu tutakapompatia Roho Mtakatifu nafasi inayostahili ndani ya maisha yetu.

Hakika Fumbo hili la Utatu Mtakatifu linatumbulia huruma ya Mungu. Leo hii tunapolitafakari fumbo hili tunaalikwa kuiona huruma yake hiyo inayojikita katika matendo yake makuu na upendo wake kwetu sisi wanadamu, iwe ni katika tendo la Baba la uumbaji, iwe ni katika tendo la Mwana katika ukombozi na zaidi iwe ni katika safari yetu hapa duniani kuelekea utakatifu huku tukiangaziwa na Roho wa Mungu na hivyo kutoa shukrani na sifa anazostahili Mungu mkuu. Tuimbe sote kwa pamoja tukisema Wastahili enzi, utajiri na heshima na twakushangilia Wewe Mungu mwenye enzi milele.

Na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.