2016-05-23 08:18:00

Fumbo la Utatu Mtakatifu


Mungu ameongea nasi katika historia. Hivyo hata hii sherehe ya leo ni matokeo ya uwepo huo wa Mungu katika matukio ya maisha yetu. Mungu amejionesha katika matuko ya maisha ya mwanadamu. Katika somo la I – halizungumzii Fumbo la Utatu Mtakatifu ila zipo dalili za ukweli huo. Iko wazi habari ya Mungu mmoja wa Israel Mungu ni mmoja. Na huyu Mungu anaonekana kwao katika matukio mbalimbali ya maisha yao ambayo kabla yake hayakuwa hivyo.

Katika somo la II Mt. Paulo twaona utatu ukiwa kazini hatuna maelezo ya utatu mtakatifu yanayotolewa bali ni nini Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanafanya katika maisha yetu. Aongea juu ya ua na n.k ila hilo linawezekana kwa sababu ya ufunuo wa mwana na kwa njia yake sisi tunakuwa wana. Je Mtume Paulo alifahamuje ukweli huu? Ni katika maisha ya wafuasi na katika maisha yake mwenyewe. Wote walimwita Mungu Baba kama alivyofanya Yesu. Ni nguvu gani inamsukuma Paulo?

Ni Roho wa Mungu katika barua nyingine za mtume Paulo aongea kumtambua roho katika nafasi mbalimbali kama kufundisha kuponya n.k katika somo la Injili – habari juu la fumbo la utatu mtakatifu iko wazi. Mitume na wafuasi wanatumwa kubatiza na katika ubatizo Fumbo la Utatu Mtakatifu huanza kuwepo katika maisha yetu. Ungamo la imani yetu huthibitisha rasmi tamko letu la upendo kwa fumbo hilo. Gal 5: 22 Matokeo ya Roho, Upendo, Furaha, Amani, Uvumilivu, Hisani, Ukarimu, Uaminifu na upole kiasi.

Mt. Agostino wa Hippo akitaka kueleza utatu mtakatifu kadiri ya akili ya mwandamu siku moja akitafakari jambo hili maeneo ya ufukweni ghafla akamwona mtoto mdogo peke yake ufukweni. Huyo mtoto alikuwa ametengeneza kishimo na alikuwa akichota maji baharini na kuyamwaga katika kale kashimo. Mt. Agostino akamwuliza unafanya nini? Mtoto akamjibu nataka kuweka bahari hii katika kashimo haka. Mt. Agostino akamwambia itawezekanaje? Kujaza kashimo haka kwa maji ya bahari yaliyo mengi kiasi hiki? Naye yule mtoto akamwambia nawe je wadhani kuwa kichwa chako kidogo na moyo wako mdogo utaweza kuelewa kw akina na kupenda kikamilifu fumbo la utatu mtakatifu? Mara mtoto yule akatoweka.

Rum 5.1-5 huunganisha utatu mtakatifu na maisha ya kila siku ya mkristo mt Paulo anaunganisha mtandao mzima wa haki na wokovu kama kuwa na amani na Mungu. Kuwa na uhusiano na Mungu ni wajibu wetu mkuu na ni njia ya kristo 5:1-2 basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani na tuwe na amani kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake katika tumaini la utukufu wa Mungu. Lengo letu ni kuwa pamoja na Baba. Hii inawezekana kwa njia ya kristo. Matumaini yetu ni kushiriki utukufu wa Mungu. Hii huwezekana kwa njia ya imani inayotupa matumaini. Mungu ametupa matumaini hayo 5:5 na tumaini halihatarishi kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumininwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.

Huu upendo wa Mungu umemwagwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Msingi wa maisha ya Kristo hujengwa katika utatu mtakatifu hii ndiyo tofauti moja kubwa kati ya dini ya kikristo na dini nyingine. Dini nyingine hutazama mhusika (mwamini) na Mungu wake tu. Ukristo pia una mtazamo huo, ila huongeza uwepo wa Yesu kristo anayetuunganisha na baba na roho mtakatifu anayetutakatifuza. Wajibu wetu wa kikristo hauanzii na kuishia tu katika imani kwa kristo na kupewa haki na Mungu. Huo tu ni mwanzo toka hapa huanza kazi ya kusaka wokovu, kuwa watakatifu kama baba alivyo mtakatifu. Sherehe ya roho mtakatifu tuliyosherekea jumapili iliyopita inashika kasi hapa. Kwa njia ya roho upendo wa Mungu humwaga mioyo mwetu na kwa njia yake tunajifunza kumpenda Mungu na jiranikama alivyotufundisha bwana.

Swali muhimu hili Fumbo linatuambia nini juu ya Mungu tumwaminiye na ni aina gani ya watu tunapaswa kuwa? Mambo mawili.

Katika Mt. 5:48 tunasoma hivi basi ninyi mtakuwa wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu Mungu ni wa ushirika tasaufi ya kikristo inatuwajibisha ulimwenguni. Pendo la kweli lahitaji watu watatu cfr. Msemo wa zamani wawili ni ushirika, watatu ni umati, cfr. Baba/mama/mtoto hutengeneza upendo huyu Mungu tumwaminiye sisi hufahamika kwetu katika utatu. Kidunia tunahusiana kati yetu kimbingu tunahusishwa na Mungu. Mimi ni mkristo kweli nikiishi katika ushirika wa upendo na Mungu na watu wake.

Fumbo la Utatu mtakatifu haliwezi kueleweka wazi. Ukuu wake hubaki kuwa fumbo. Na leo hatutegemei kupata jibu kwa fumbo hilo. Wakristu wa kwanza kwa akili yao walielewa ufunuo wa Baba kwa njia ya mwanae. Yesu ameongea nasi habari ya Baba aliyemtuma na juu ya Roho mtakatifu atakayempeleka hii iko wazi kwenye maandiko matakatifu. Yesu hutuambia wazi kuwa Mungu amemkabidhi yote naye amemkabidhi yote Roho mtakatifu. Hapa twaona muungano wa UTATU.

Katika historia ya wokovu. Mungu baba ni mwumbaji Mungu mwana ni mkombozi na Mungu roho ni mtakatifu. Hutakatifuza. Ingawa ni nafsi tofauti umungu ni mmoja kama ilivyokuwa kwa Mt. Agostino hatutaelewa ni kwa namna gani ila ni kwanini Mungu amejifunua kwetu. Ukuu wa Fumbo hili ni huu: sisi tumeumbwa kwa mfano na sura yake Mungu. Kwa kadiri tunavyomuelewa Mungu ni jinsi hiyo hiyo tunavyojielewa zaidi. Wataalamu wa mambo ya dini wanatuambia kuwa waabuduo hujitahidi kufanana na kila wanachokiabudu. Wanaoabudu Mungu wa vita huwa watu wa vita wanaoabudu Mungu wa upendo huwa watu wa mapendo n.k kama alivyo Mungu anayeabudiwa ndivyo walivyo wale wanaomwabudu.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.