Tarehe 8 Mei, ilikuwa ni Siku ya Mawasiliano Duniani , mwaka huu ikiwa ni adhimisho la 50 tangu kuanzishwa kwake. Kwa ajili hii, Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia zaidi mawasiliano kama fursa ya kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu, kupitia njia ya majadiliano na mazungumzo ya amani kati ya watu. Na kwamba huruma ina uwezo wa kuponya uhusiano uliojeruhiwa , kurejesha matumaini na maelewamo kati ya wanafamilia na katika jamii. Ujumbe huu wa Papa, uliwasilishwa siku za nyuma 24 Januari, ili kutoa muda wa kutosha kusomwa, kabla ya adhimisho lenyewe. Papa aliandika ujumbe wake chini ya jina: “Mawasiliano na Huruma: matunda ya kukutana ” .
Papa ametoa ujumbe wake katika mtazamo wa maadhimisho ya Mwaka wa Huruma sanjari na maadhimisho ya kupita miaka 50 tangu adhimisho la Siku ya Dunia ya Mawasiliano lilipoanzishwa, akisema, mwaka Mtakatifu, unatoa mwaliko kwetu sote, kutafakari uhusiano uliopo kati ya mawasiliano na huruma . Kanisa katika muungano wake na Kristo , mwili hai wa Baba wa Huruma , linaitwa kuiishi huruma kama tabia yake yenye kuonyesha kwamba, ni Yeye Baba mwenye huruma anayetenda. Papa amewahimiza wakristo wote kuwa na lugha nzuri inayotoa mwangi wa wema na huruma akisama ni lazima kujali tunasema nini na jinsi tunavyosema ,na kila neno na tendo , ni lazima litoe picha ya huruma ya Mungu, upendo na msamaha wake kwa wote.Aliongeza, “Upendo, kwa asili yake, ni mawasiliano yanayoongoza kwa uwazi na ushirikiano. Kama mioyo yetu na matendo vinaongozwa na upendo wa Mungu, basi mawasiliano yetu yatapata nguvu yake kutoka kwa Mungu mwenyewe”.
Hivyo Papa amesisitiza katika ujumbe huo kwamba, wote kama wana wa Mungu, wake kwa waume , tumeitwa kuwasiliana na kila mtu, bila ubaguzi. Na kwa namna ya Kipekee, Kanisa kwa maneno na matendo yake yote, yanatakiwa kutoa maana ya huruma na kuifikisha huruma hiyo kwa watu, ikigusa mioyo ya watu na kuwadumisha katika safari yao ya maisha hadi katika ukamilifu wake ambaye ni Yesu Kristo aliyetumwa na Baba, kuwapeleka wote kwake Mungu. Hii ina maana kwamba sisi wenyewe lazima kuwa tayari kukubali upendo huu wa Mama Kanisa na kuushiriki ili na wengine pia wapate kujua kwamba, wanapendwa na Yesu. Ni upendo huo wenye kutoa maana ya Neno la Imani , kwa mahubiri na shuhuda , hutoa "cheche" za maisha.
Ujumbe wa Papa unaendelea kufafanua kwamba, mawasiliano yana uwezo wa kujenga madaraja, yenye kuwawezesha kukutana na kushirikiana , na hivyo kuwa na jamii iliyoimarika katika umoja na mshikamano. Papa ameeleza na wakati huohuo akaonya kwamba , wakati wa kuwasiliana, inafaa kuchagua maneno na matendo , na kufanya kila jitihada za kuepuka kutokuelewana, na kuponya kumbukumbu za waliojeruhiwa na kujenga amani na utulivu. Papa anasisitiza maneno na matendo yetu lazima iwe ni nyenzo ya kutusaidia sote kuepuka mzunguko wa matatizo na kuhukumu na kulipiza kisasi , ambavyo kwa mara zote huleta utengano kwa watu, kibinafsi na hata kimataifa. Ni lazima kuepuka maneno yanayojenga chuki. Kwa Wakristo lugha yao daima iwe ni kuleta faraja na mshikamano , hata katika matukio yenye kuchukiza, wao ni lazima wawe imara kulaani uovu uliofanyika , lakini kamwe si kuvunja mahusiano na mawasiliano.
Papa amewaomba wale wenye majukumu hasa ya uongozi kitaasisi na kisiasa, na watoa maoni kwa umma,ni lazima wawe makini na maneno yao, hasa wanapokosoa wengine wanaodhani wamefanya makosa, kwa kuwa katika hali hiyo ya kukosoana ni rahisi kuingia katika mtego wa kushutumiana na hivyo kuwasha moto wa kutoaminiana, hofu na chuki. Papa ameomba ujasiri katika kuongoza watu, ili zaidi iwe ni kuelekea mchakato wa maridhiano ma siyo utengano. Ni muhimu daima kuwa na mtazamo chanya na ujasiri bunifu katika kutoa ufumbuzi wa kweli hata katika migogoro ya kale na nafasi ya kujenga amani ya kudumu. Papa alikamilisha na aya " Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu" (Mt 5: 7-9)
All the contents on this site are copyrighted ©. |