2016-05-05 10:45:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Duniani


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kutafakari kuhusu mawasiliano na huruma. Kimsingi, Kanisa likiwa limeungana na Kristo Yesu, umwilisho wa huruma ya Mungu linaalikwa kwa namna ya pekee kumwilisha huruma kwa uwepo na matendo. Kanisa liwe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu inayojionesha kwa namna ya pekee katika upendo, wema na huruma ya Mungu kwa wote. Upendo kwa asili ni mawasiliano yanayojielekeza katika kuwashirikisha wengine na wala si kujifungia katika ubinafsi. Ikiwa kweli waamini watakuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, mawasiliano yao yatakuwa ni chombo kinachobeba nguvu ya Mungu.

Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, ambayo kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 8 Mei 2016, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto ya kujenga na kudumisha mawasiliano na wote pasi na ubaguzi. Maadhimisho haya yanayoongozwa na kauli mbiu “Mawasiliano na huruma ni makutano yenye uhai”.

Ni wajibu wa Mama Kanisa kutangaza huruma ya Mungu, ili kugusa nyoyo za watu na kuwaenzi katika hija yao kuelekea kwenye utimilifu wa maisha, ambayo Yesu Kristo aliyetumwa na Baba anataka kuwakirimia watu wote. Huu ni mwaliko wa kuupokea ujumbe na kuonja vuguvugo la Mama Kanisa, ili Yesu aweze kufahamika na kupendwa! Hili ni joto linalobubujika imani inayofumbatwa katika mahubiri na shuhuda zinazolifanya Neno hili kuwa hai!

Baba Mtakatifu anasema, mawasiliano yana nguvu ya kujenga madaraja na kusaidia watu kukutana na kushirikiana, kiasi hata cha kuitajirisha jamii. Inafurahisha kuona watu wakichagua kwa umakini mkubwa maneno na vitendo ambavyo vitasaidia kuvuka mipaka ya watu kutoelewana; ili kuponya kumbu kumbu zenye machungu katika maisha, ili hatimaye, kujenga amani na utulivu. Maneno yanaweza kujenga daraja kati ya mtu na mtu; familia na jamii katika ujumla wake. Mchakato huu unaweza kutendeka katika ulimwengu wa mawasiliano ya digitali na analogia.

Maneno na matendo yawasaidie watu kutoka katika mzunguko wa laana na kulipizana kisasi, hali inayoendelea kuwatendea watu binafsi na mataifa, wanaotupiana maneno ya chuki. Neno la Mkristo lisaidie mchakato wa ujenzi wa umoja hata pale anapolaani ubaya, daima akijitahidi kutovunja mahusiano na mawasiliano. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kugundua nguvu ya huruma tayari kuganga na kuponya mahusiano yenye makovu; kurejesha tena amani na utulivu kwenye familia na jamii katika ujumla wake. Machungu na madonda ya zamani yanaweza kuwa ni kikwazo kikubwa katika mchakato wa mawasiliano, upatanisho na mahusiano kati ya watu. Katika maeneo yote haya huruma ina nguvu ya kuamsha tena namna mpya ya kuzungumza na kujadiliana, kwani huruma ni baraka yenye makali kuwili: kwa mtu anayepokea na yule anayetoa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, lugha ya wanasiasa na wanadiplomasia itaweza kujikita katika huruma; tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuunda maoni jamii, daima wakijitahidi kuwa makini, ili kutojenga mazingira ya kutoaminiana, woga na chuki. Watu waoneshe ujasiri katika kukuza na kudumisha mchakato wa upatanisho, ili kujenga amani ya kudumu! Heri wenye rehema maana hao watapata rehema na heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Kanisa kujenga mawasiliano na huduma katika hali ya unyenyekevu na kamwe wasiwe na “majigambo” na kiburi cha ushindi dhidi ya adui zao au kuwadharau wale ambao wamemezwa na malimwengu, bali huruma isaidie kuwasha moto wa maisha mapya na joto kwa wale ambao katika maisha yao wameonja ukasisi na hukumu; hali ya kuwatenga wadhambi na wenye haki, bali wawe na ujasiri wa kutoa hukumu katika masuala ya dhambi, uhalifu, rushwa, ufisadi, unyonyaji bila kuwahukumu watu, kwani Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Hakimu mwenye haki anayemsoma mtu kutoka katika undani wa moyo wake.

Viongozi watambue kwamba, wanayo dhamana ya kuwaonya wakosefu, kupambana na maovu na ukosefu wa haki, ili hatimaye, kuwakomboa wahanga na kuwanyanyua wale walioanguka. Huu ndio ukweli unaobubujika kutoka kwa Kristo mwingi wa huruma na mapendo; kipimo cha kutangaza ukweli na kulaani ukosefu wa haki. Ni wajibu wa viongozi kukazia ukweli kwa njia ya upendo. Maneno yanayosemwa kwa upendo, huruma na unyenyekevu yanagusa undani wa mioyo ya wadhambi. Maneno makali yanahatari ya kuharibu mchakato wa toba na uhuru, kiasi cha kuwafanya wawe sugu na hatimaye kuwa wakanimungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka huu anakaza kusema, mwelekeo wa Jamii inayosimikwa katika huruma ni jambo la kawaida kama inavyojionesha ndani ya familia. Wazazi walionesha upendo na huruma kwa watoto wao; wakasaidia mchakato wa mafanikio na hatimaye, kuwaunda jinsi walivyo kwa sasa. Wazazi wanataka ustawi na maendeleo ya watoto wao na kwamba, familia ni mahali pa kuonja wema na ukarimu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusikiliza kwa makini, tayari kuanzisha mchakato wa kushirikishana na kuonjeshana ukarimu kwa kuwasiliana, ili kujenga mahusiano ya karibu zaidi. Utamaduni wa kusikiliza unajikita katika uwezo wa kushirikishana na wengine maswali na wasi wasi ya maisha, ili kuweza kutembea na wengine bega kwa bega, kwa kujenga unyenyekevu, tayari kushirikisha nguvu, karama na mapaji yako kwa ajili ya huduma na mafao ya wengi. Kusikiliza si rahisi, yataka moyo! Ni hali ya kuwa makini kwa kuonesha hamu ya kufahamu, kuthamini, kuheshimu na kutunza neno linalotoka kwa mwingine. Kusikiliza ni sanaa inayojikita kwenye ushuhuda na sadaka, kwa kuthamini utu na utakatifu wa jirani yako. Kufahamu kusikiliza ni neema kubwa na zawadi ambao waamini wanapaswa kuiomba, ili hatimaye waweze kuimwilisha katika uhalisia wa maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumizi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuwa ni njia sahihi ya mawasiliano ya kibinadamu, ikiwa kama mwanadamu atakuwa na uwezo wa kutumia vyema mitandao hii ya kijamii, kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema ya kijamii; kwa kutafuta na kuendeleza mafao ya wengi. Mitando ya kijamii isipotumiwa vyema inaweza kuwa ni sababu ya mipasuko na kinzani za kijamii. Mazingira ya digitali ni jukwaa na mahali ambapo watu wanaweza kuonjeshana upendo, kuganga na kuponya madonda; mahali pa majadiliano yenye tija na mashiko au jukwaa la “wachovu” wa maadili na utovu wa nidhamu.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wakimwilisha huruma katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu itakuwa ni fursa ya kujenga majadiliano, ili kufahamiana vyema zaidi, tayari kufuta kila aina ya ubinafsi, nyanyaso, uhalifu na ubaguzi. Mitandao ya kijamii iwe ni jukwaa la ujenzi wa raia wema na kwamba, watu watumie mitandao hii kwa kuwajibika, kwa kulinda na kuheshimu utu wa wengine. Mitandao ya kijamii inaweza kutumiwa vyema katika kukuza jamii iliyoko wazi na yenye kushirikishana.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa kukumbusha kwamba, mawasiliano: maeneo na vyombo vyake ni mwendelezo wa upeo mpana wa watu, zawadi kutoka kwa Mungu inayowawajibisha kwa kujenga ukaribu. Makutano kati ya mawasiliano na huruma ni uhai unaosaidia kudumisha ujirani mwema, huduma, faraja, uponyaji, usindikizaji na hufanya siku kuu. Katika ulimwengu uliogawanyika, kumeguka na kuvutana; mawasiliano yanayojikita katika huruma yana maanisha kuchangia mchakato wa ujenzi wa wema, uhuru na mshikamano kati ya watoto wa Mungu na ndugu katika ubinadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.