2016-05-04 08:26:00

Uhuru wa vyombo vya habari!


Haki msingi za binadamu, mchakato wa demokrasia katika jamii na mikakati ya maendeleo endelevu kwa kiasi kikubwa inategemea uhuru wa habari na haki ya kupata habari inayojikita katika uhuru wa vyombo vya habari. Hivi ndivyo anavyosema Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya uhuru wa vyombo vya habari kimataifa, ambayo inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Mei!

Maadhimisho haya kwa namna ya pekee yanalenga kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari; kuwaenzi wadau katika tasnia ya habari ambao wakati mwingine wanahatarisha maisha yao wanapotekeleza dhamana na wajibu wao katika tasnia ya habari! Maadhimisho ya mwaka huu, anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa yanapambwa kwa namna ya pekee na matukio makuu matatu: Kumbu kumbu ya miaka 250 tangu kuchapishwa sheria ya kwanza kabisa kuhusu uhuru wa habari duniani na kuenea nchini Uswiss na Finland kwenye ramani ya sasa.

Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Itifaki ya Windhoek ilipopitishwa kuhusu msingi ya uhuru wa vyombo vya habari. Mwaka 2016 ni mwanzo wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Uhuru wa vyombo vya habari na upatikanaji wa habari ni mambo msingi sana katika kuwahabarisha wananchi minatarafu Malengo ya Maendeleoendelevu pamoja na kuangalia utekelezaji wake unaofanywa na viongozi wa nchi husika.

Vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii ni macho na masikio ya watu na kwamba, wengi wanafaidika na habari zinazotolewa na vyombo hivi! Mazingira huru na salama ni muhimu sana kwa waandishi wa habari kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, lakini kwa bahati mbaya, mara nyingi ni watu wanaokabiliwa na vitisho, mashambulizi na hata wakati mwingine kuuwawa wakati wakitekeleza dhamana na wajibu wao.

Baadhi yao wameishia kutupwa magerezani na wengine wanaishi katika mazingira hatarishi kutokana tu na “kuwatumbua” wanasiasa uchwara, mafisadi pamoja na matatizo ya kijamii. Katibu mkuu anaendelea kusema kwamba, watu wengi wanaendelea kuonesha wasi wasi kutokana na vizuizi vya uhuru wa habari, hali ambayo inakwamisha maendeleo ya uhuru wa habari. Siku ya vyombo vya habari iwe ni fursa kwa wadau mbali mbali kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari, vinginevyo uhuru wa wanahabari utadhibitiwa sana na hivyo kudhoofisha nguvu yake. Kwa kushirikiana na vyombo vya mawasiliano ya jamii inakuwa ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa pamoja kuhakikisha kwamba, utu wa wengi unalindwa na kudumishwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.