2016-05-03 07:13:00

Wafungwa kuweni na ujasiri wa kuandika upya kurasa za maisha yenu!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, Jumapili, Mei Mosi, 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa kwa wafungwa wanaotumikia adhabu zao kwenye Gereza kuu la Regina Coeli lililoko mjini Roma. Anasema, utu na heshima ya binadamu vinapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utu wa mwanadamu haupimwi kutokana na matendo yake mema au mabaya, kumbe hata wafungwa magerezani wanapaswa kuheshimiwa utu wao, kwani wameumbwa na kukombolewa kwa njia ya Fumbo la Msalaba! Yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!

Yesu alidhalilishwa, akapigwa mijeledi, akavikwa taji la miiba kichwani, akatundikwa na hatimaye kufa Msalabani, damu yake azizi ikawa ni chemchemi ya ukombozi kwa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu Kristo, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo kikuu cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Kardinali Baldisseri anakasa kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake!

Katika mahubiri yake, Kardinali Baldisseri amefafanua kwamba, Yesu ambaye hakuwa na dhambi hata kidogo, alijinyenyekesha na hatimaye kushikamana na wadhambi, ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wa Baba wa milele. Katika maisha yake, alionja adha ya kutuhumiwa, kuhojiwa, kuhukumiwa na hatimaye kutekeleza adhabu ya kifo Msalabani, hata kama hakutenda kosa lolote! Huu ni ushuhuda wa maisha ya Yesu unaojikita katika uhalisia na wala si jambo la kusimulia kutoka vitabuni au kwa kuangalia kwenye Luninga.

Wafungwa magerezani katika maisha wanakumbana hata wakati mwingine na upweke hasi, kiasi hata cha kuwakatisha tamaa, lakini wanapaswa kukumbuka kwamba, hata Yesu mwenyewe katika maisha yake alikumbana na kipindi cha giza na mahangaiko makubwa, lakini akashinda yote kwa kujiaminisha mbele ya Baba yake wa mbinguni. Hata wafungwa katika shida na mahangaiko yao, wawe na ujasiri wa kumkimbilia na kumwonesha Yesu upendo wao wa dhati, kwani wana thamani kubwa machoni pa Mungu. Yesu ni chemchemi ya amani,utulivu na faraja.

Yesu anawakirimia waja wake amani ya kweli inayojikita katika: ukweli, uhuru, haki na upendo. Amani ya Kristo ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na ubaya, chachu ya kuambata toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kweli kwa ajili ya maondoleo ya dhambi. Waamini watambue kwamba, adui wa mtu ni mtu mwenyewe na kamwe wasitafute mchawi nje ya maisha yao ya kila siku! Hii ni changamoto ya kushinda kiburi na maisha ya giza yanayomwandama mwanadamu katika safari yake hapa duniani.

Waamini wawe na ujasiri wa kuandika kurasa mpya za imani, matumaini na mapendo kwa kuuvua utu wao wa kale uliochakaa kutokana na ubaya pamoja na dhambi. Wajitahidi kuwa kama mshumaa unaowaka ili kufukuza giza la dhambi na ubaya kwa kutenda mema kwa kutambua kwamba, ndani mwao kuna karama na vipaji ambayo wamekirimiwa na Mungu na kwamba, wanapaswa kuvifanyia kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ibada hii ya Misa Takatifu kwenye Gereza kuu la Regina, Coeli imehudhuriwa pia na Askofu Giafranco Girotti pamoja na viongozi wakuu wa gereza hili. Baada ya Misa, wafungwa walitumbuiza kwa nyimbo, ikikumbukwa kwamba, hii pia ilikuwa ni Siku kuu ya wafanyakazi duniani kwa mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.