2016-05-02 15:33:00

Roho Mtakatifu huitia nguvu ya kumshuhudia Kristo hata wakati wa mateso


Roho Mtakatifu huwatia nguvu ya kuendelea  kumshuhudia Yesu Kristo,  hata  wakati wa mateso na dhulumna katika nyakati za hatari zinazodai kuyatoa maisha kama sadaka, licha ya mateso yanayotokana na mambo mengine  mengine madogomadogo, yatokanayo na  masengenyo, uzushi  na ukosoaji.  Ni maelezo ya Baba Mtakatifu Francisko, mapema Jumatatu hii wakati  akiongoza Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta ,ndani ya  Vatican.

Papa alisema pia  kwa kadiri tunavyoelekea katika adhimisho la Siku Kuu ya kushuka kwa Roho Mtakatifu, ndivyo masomo katika  liturujia ya Neno yanavyotuelekeza katika tukio hili la “Pentecoste”. Na katika somo la leo kutoka Matendo ya Mitume , linalenga kutuonyesha sisi kwamba , Bwana aliufungua moyo wa  Lidia,Mfanyabiashara wa nguo za zambarau kutoka mji wa Thyatria , ambako watu walifika kumsikiliza Mtakakafu Paul.

Papa alieleza hisia za mwanamke huyo , aliyesikia kuguswa na kitu ndani mwake na kumfanya asema ukweli wake kwamba,  'hii ni kweli! Mimi nakubaliana na kile mtu huyu anachosema, mtu huyu anayemshuhudia  Yesu Kristo”.

Papa alihoji, ni nani hasa aliyegusa moyo wa mwanamke huyo? Na nani alimwambia kusikiliza kwa makini aliyokuwa akihubiri Mtakatifu Paulo?  Papa alitoa jibu kuwa ni Roho Mtakatifu aliyemfanya mwanamke huyu amwone Yesu kuwa ni Bwana wa wokovu kupitia ushuhuda wa  maneno ya Paul.  Alikuwa ni Roho Mtakatifu ndani mwake  aliyemshuhudia  Yesu. Na  ndivyo ilivyo kila  siku katika maisha yetu , tunasikia kitu moyoni chenye kutuleta karibu na Yesu , ni Roho Mtakatifu anayetugusa ndani mwetu na kupata ujadiri huu wa kumshuhudia Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana wa uzima wa milele. 

 Papa ilirejea katika somo la Injili ambamo Yesu anawatahadharissha wafuasi kwake kwamba, kumshuhudia pia huandamana na mateso akitoa ufafanuzi kwamba, mateso hayo pia yanaweza kuanza tangu  adha ndogo ndogo za maudhi,  uzushi , uongo,  masengenyo na  ukosoaji hadi katika mateso makubwa  yenye kumtaka hata mtu ayatoe maisha yake kama sadaka , kama inavyoonekana katika historia ya Kanisa, yanaendelea kuwepo hata leo hii, wengi wakifungwa hata gerezani  au kuuawa kwa sababu za kumshuhudia Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana na  Mkombozi wa dunia.  

Hii ndiyo maana Yesu alionya,  kumshuhudia yeye inaweza kuwa  gharama kubwa kama ilivyoandikwa katika Injili , ”watawafukuzeni katika masinagogi, na wakati unakuja , ambapo kila mtu atakayewaua atafikiri anatoa sadaka kwa Mungu”.

Papa aliendelea kufundisha na kuwataka Wakristo kutokata tamaa  maana uimara wa Mkristo katika kumshuhudia Kristo,  nguvu yake hutoka kwa  Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtaktifu anayewatia nguvu ya  kumshuhudia  Bwana aliye hai,  Bwana Mfufuka, ambaye yupo  katikati ya waamini wake , ambao huadhimisha kifo na ufufuko wa Kristo, kila siku madhabahuni. Wakristo hutoa ushuhuda huu kwa msaada wa Roho Mtaktifu katika njia ya Maisha yao ya kila siku kwa maneno na matendo, licha ya maudhi, mashambulio na mateso. 

Hivyo Papa amesema , ni jambo jema  kumwomba Roho Mtakatifu  aje kukaa moyoni mwetu, ili tuweze kumshuhudia Kristo bila woga.  Kumwomba Roho Mtakatifu  asituache peke yetu lakini alitunfudishe maneno ya Yesu na kuyaishi kama Yesu alivyofanya hapa duniani.  Tumwite Roho Mtakatifu , ili atufundishe kutofautisha  mema yatokayo  kwa Yesu dhidi ya maovu yanayotoka  kwa baba wa uogo, mkuu wa ulimwengu huu na  mkuu wa dhambi  anayetaka kutuweka mbali na Kristo, mwovu mwenye kutoa kitisho dhidi ya kumshuhudia Kristo katika maisha yetu ya kila siku.  








All the contents on this site are copyrighted ©.