2016-05-02 06:31:00

Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA-CERAO, hivi karibuni, baada ya maadhimisho ya Mkutano wake wa pili tangu kuanzishwa kwake, limekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika. Mwaka huu ulitangazwa na kuzinduliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika!

Hapa mkazo unaendelea kutolewa kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inayoendelea kushika kasi hususani wakati huu wa kipindi cha Kwaresima. Kanisa ni chambo na shuhuda wa upatanisho, dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu!

Kanisa linawaalika na kuwahimiza waamini kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao pamoja na kujipatanisha na mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika ni kipindi kilichokubaliwa cha kufanya toba na wongofu wa ndani; tayari kuambata huruma, msamaha na upendo wa Mungu! Maaskofu kutoka Afrika Magharibi, wanapoangalia kwa umakini mkubwa hali ilivyo katika eneo hili, wanasema, kwa hakika kuna haja ya kutubu, kuongoka na kujipatanisha na Mungu.

Waamini wawe ni vyombo, mashuhuda na mabalozi wa upatanisho ndani ya jamii zao. Hii ni dhamana waliyojitwalia walipopokea Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha kwa namna ya pekee: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anawaalika Wakristo wote kuwa kweli ni Wamissionari, mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kw akujikita katika misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi katika ujumbe wake kwa Familia ya Mungu huko Afrika Magharibi linakaza kusema, linapenda kuivalia njuga changamoto ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kukuza na  kudumisha majadiliano ya kidini na kiekuemene; kwa kuonesha umoja na mshikamano na Wakristo wanaoendelea kuteswa na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Maaskofu wanakaza kusema, wanawaombea na kuwatakia nguvu na ujasiri kutoka juu, ili viweze kuwasaidia kukabiliana na changamoto hizi. Maaskofu pia wanawataka viongozi wa kimataifa kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu na haki msingi za binadamu zinakuzwa na kudumishwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Itakumbukwa kwamba, mkutano huu uligusia pia umuhimu wa Familia ya Mungu Barani Afrika kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia; kukuza na kudumisha misingi ya demokrasia ya kweli; kusimama kidete kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; Pamoja na hayo Maaskofu wamewataka vijana kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na upatanisho, kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa ucharwa kuvuruga amani na utulivu na kwamba, Wakristo wote wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.