2016-05-02 07:22:00

Askofu mkuu Francis Assisi Chullikatt , Balozi mpya huko Kazakhstan!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Francis Assisi Chullikatt kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Kazakhstan na Tadjikistan. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Chullikatt alikuwa ni mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Francis Assisi Chullikatt alizaliwa kunako tarehe 20 Machi 1953 huko Bolghatty, India. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja takatifu la Upadre hapo tarehe 3 Juni 1978, Jimboni Verapoly, India. Tarehe 15 Julai 1988 akaanza utume wake katika tasnia ya diplomasia mjini Vatican na kubahatika kutekeleza utume huo huko: Honduras, Afrika, Ufilippini na Umoja wa Mataifa.

Tarehe 29 Aprili 2006 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akamteua kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Yordani na Iraq. Tarehe 25 Juni 2006 akawekwa wakfu kuwa Askofu. Tarehe 17 Julai 2010 akateuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuwa mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Tarehe 1 Julai 2014 akahitimisha utume wake na Askofu mkuu Bernardito Cleopas Auza akachukua nafasi yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.