2016-04-30 09:16:00

Jubilei ya miaka 25 ya Waraka wa "Centessimus Annus"


Ilikuwa ni Mei, Mosi 1991, miaka 100 baada ya Papa Leo wa XIII kuchapisha Waraka wa Kichungaji “Mambo Mapya” “Rerum Novarum”, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kitume “Centesimus Annus” yaani “Miaka Mia moja” tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wa kitume, msingi thabiti wa Mafundisho Jamii ya Kanisa uliojikita katika: haki, utu na heshima ya binadamu, kwa kujibu kwa nguvu na sauti ya kinabii changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa wafanyakazi. Ikumbukwe kwamba utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi.

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa Kitume “Centessimus Annus”, mwendelezo wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayojikita kwa namna ya pekee kabisa katika: utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi; mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanabainisha tunu msingi za kijamii zinazosaidia mchakato wa utekelezaji kanuni msingi nazo ni: ukweli, uhuru, haki na upendo.

Kunako tarehe 5 Juni 1993 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II akaanzisha Mfuko wa “Centessimus Annus” unaosimamiwa na kuratibiwa na waamini walei, wanaotumia taaluma, karama na mapaji yao kwa ajili ya kusaidia mchakato wa kusambaza na kueneza Mafundisho Jamii ya Kanisa. Bwana Domingo Sugranyes Bickel, Rais wa Mfuko wa “Centessimus Annus”  katika maadhimisho haya anasema kwamba, waraka huu wa kichungaji ni dira na mwongozo mpya wa Kanisa Katoliki mintarafu masuala ya uchumi, soko, huduma na maendeleo endelevu ya binadamu.

Ni Waraka ambao umesoma historia ya binadamu na kuangalia yale yajayo, kwani Mafundisho Jamii ya Kanisa ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hii ni changamoto kwa waamini walei kuhakikisha kwamba, kwa njia ya maisha na utume wao wanakuwa kweli ni chachu, mwanga na chumvi ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji!

Mfuko wa “Centessimus Annus” ni kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo, dhamana na utume unaotekelezwa na waamini walei ambao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo! Kwa njia ya utume huu, waamini walei wanaendeleza mchakato wa majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi katika sekta ya uchumi, sayansi jamii na maendeleo endelevu anasema Bwana Bickel.

Ili kufikia lengo hili Mfuko huu umekuwa ukiendesha semina, warsha na makongamano katika ngazi mbali mbali, sanjari na kuendeleza majadiliano na mabingwa waliobobea katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kuhamasishwa na maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, Mfuko wa “Centessimus Annus” tarehe 12- 14 Mei 2016 utaendesha mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Wafanyabiashara katika mapambano dhidi ya umaskini: wimbi la wakimbizi, changamoto yetu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.