2016-04-29 14:34:00

Magonjwa adimu: Utu, tafiti za kisayansi na tiba ni mambo muhimu!


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 29 Aprili 2016 amekutana na kuzungumza na wajumbe waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la utamaduni kwa kushirikiana na Mfuko wa “Stem for Life”. Ni mkutano ambao umechambua jinsi ambavyo imani, sayansi, teknolojia, habari na mawasiliano yanavyoweza kusaidia kuboresha tiba ya binadamu mintarafu magonjwa ambayo yanapatikana kwa nadra sana katika jamii.

Wajumbe wa mkutano huu wamefanya tafakari ya kina jinsi ya kumwilisha weledi, ujuzi na uzoefu wao katika tafiti na tiba bila kupuuuzia masuala mtambuka katika elimu ya binadamu, jamii na tamaduni pamoja na suala changamani la huduma na tiba kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa adimu, watu ambao mara nyingi hawapewi kipaumbele cha pekee kwani ni watu ambao hawasaidii kusongesha mbele mchakato wa uwekezaji.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika maisha na utume wake anakutana na watu wenye magonjwa adimu yanayoendelea kuwaandama mamillioni ya watu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kusababisha mateso na wasi wasi hata kwa watu wenye wajibu wa kuwahudumia kuanzia ndani ya familia! Mkutano huu unapata uzito wa pekee kabisa wakati Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; huruma ambayo ni sheria msingi inayojikita katika sakafu ya moyo wa mwanadamu anayemwangalia kwa unyofu wa macho jirani anayemkuta akiogelea katika shida ya maisha.

Mkutano huu anasema Baba Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini inayowashirikisha watu, taasisi, tamaduni na dini mbali mbali, wote kwa pamoja wakipania kutoa huduma makini kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu, anawataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuendeleza mchakato wa uragibishaji, ili jamii iweze kuguswa na kuonesha huruma na upendo kwa wanaosumbuliwa na magonjwa adimu. Uragibishaji uguse utu na heshima ya binadamu nje kabisa na imani, jamii na mazingira ya mtu kitamaduni.

Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya peke kuhusu tafiti inayojikita katika elimu na tafiti za kisayansi ili kukuza na kuimarisha: akili, ujuzi na maarifa ya wanafunzi kitaaluma. Wanafunzi wafundwe vyema katika utu na maadili; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Tafiti zijikite katika tunu msingi za maisha ya binadamu yaani: mshikamano, ukarimu, sadaka na majitoleo, ushirikishanaji wa maarifa; heshima kwa maisha ya binadamu pamoja na upendo wa kidugu usiotafuta faida binafsi.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, watu wengi wanapata fursa ya kutibiwa kwani kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sayansi na teknolojia mintarafu masuala ya tiba ya binadamu, elimu na mawasiliano, lakini haya ni mambo yanayohitaji kusimikwa katika uchumi unaojali na kudumisha usawa, badala ya kutafuta faida kubwa inayohatarisha maisha ya watu sanjari na kuondokana na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya watu. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kuwekeza katika tafiti, ili kupata takwimu sahihi huku binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupata suluhu ya kudumu kwa wagonjwa wanaoteseka na kuwawezesha kupata tiba muafaka.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, anawataka wajumbe kupyaisha tunu hizi msingi ambazo wamekuwa wakizifanyia kazi katika maisha yao, kwa kuwahusisha watu wengi zaidi, ili katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Baba wa mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.