2016-04-29 08:02:00

Amani ya Kristo humfunulia mwanadamu huruma ya Mungu!


Kanisa linaadhimisha Dominika ya sita ya Pasaka ya Mwaka C. Neno kubwa linaloongoza tafakari yetu leo hii ni amani ya Kristo ambayo anatuachia kwa ajili ya kutufunulia huruma ya Mungu mioyoni mwetu. Siku ya sherehe ya Pasaka Kristo aliwatokea wanafunzi wake na kuwapatia amani kama zawadi ya kwanza, amani kama tunda linalotokana na ufufuko wake, amani ambayo inapatika pekee ndani ya Kristo mfufuka anayesema: “waambieni walio na moyo wa hofu, ‘jipeni moyo, msiogope!” (Is 35:4). Pengine ni ujumbe mzuri tunaopewa na Mama Kanisa na hasa tunapoelekea kuhitimisha kipindi hiki cha Pasaka ili tukiongozwa na Roho Mtakatifu tuendelee kuidhihirisha amani hiyo kwa watu wote katika maisha yetu ya kila siku.

“Amani yangu nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo”. Ujumbe huu wa Kristo unatualika kuzama ndani kabisa na kujiuliza nini maana ya hiyo amani ya Kristo na ni nini tofauti yake na amani tuipatayo ulimwenguni. Neno amani linaashiria utulivu. Tunamwona mwanadamu leo hii katika hali ya mahangaiko mengi na daima anatafuta utulivu. Sote tunashuhudia vita kati ya jamii na jamii, mivutano katika njanja mbalimbali ziwe ni za kisiasa au za kiuchumi na mambo mengine mengi. Hali hii inamfanya mwanadamu kuhangaika katika kutafuta suluhu ili atulie.

Kila mmoja anatafuta mbinu zake iwe ni za kiuchumi au ni za kiushawishi kutafuta utulivu ndani yake, katika familia yake na kadhalika. Lakini utulivu au amani hii mara nyingi huwa ni kwa muda tu sababu hujengwa nje ya Mungu. Hapa ninakumbuka wimbo mmoja unaosema: “uzio wa umeme, mlinzi wa kimasai, mbwa mkali, tunguli na silaha za kisasa, havifai kitu”. Mwanadamu anaweza kujizingira kwa namna nyingi sana na kujihakikishia usalama na amani lakini kama chanzo cha amani hiyo kisipokuwa katika Kristo amani au utulivu huo huwa ni wa muda tu.

Amani ya kweli ya Kristo inapatikana pale tunapokuwa na Kristo ndani mwetu. Katika Injili ya leo anatupatia mbinu ya kuuhisha huo uwepo wake: “Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake”. Amani yetu ya kweli inapatikana au inajengwa katika hofu ya Mungu ndani mwetu. Hapa ndipo tunaoona umuhimu wa paji la imani katika kujenga amani ya kweli. Paji la imani hutupeleka katika kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza na kutimiza mapenzi yake. Jumuiya ya kikristo ambayo inaelezewa katika somo la kwanza iliingia katika vurugu baina yao kwa sababu tu utashi wa kibinadamu ulitaka kutawala kati yao. Barua ya mitume kwa Jumuiya hii inalithibitisha hili: “kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza”. Umoja na mshikamano ndani ya Kanisa ambalo linaongozwa na Roho Mtakatifu unaiepusha Jumuiya hii kutoka katika changamoto hiyo na kuwa katika hali ya amani.

Katika mantiki ya kawaida sauti nyingi ndani ya kichwa cha mtu mmoja kamwe haziwezi kumweka mtu huyo salama. Jumuiya ya mwanadamu inahitaji kuwa na mwongozo mmoja madhubuti ambao ndiyo utamfikisha katika utulivu wa kudumu. Tangu kuumbwa kwa mwanadamu tumeshuhudia kupitia maandiko matakatifu jinsi ambavyo anaangaika sana kwa sababu ametoka katika kumsikiliza Mwenyezi Mungu na kuendelea kujisikilizia sauti zake mwenyewe. Huu ndiyo ulimwengu unaoelezewa leo hii na huria katika maadili, yaani kila mmoja kutenda kadiri anavyoona inampendeza yeye. Tusitegemee kuvuna zabibu katika mchongoma. Hali kama hii lazima itatuingiza katika kusikia sauti nyingi sana ambazo daima hutudanganya kuwa ndipo tutapata utulivu wa kweli.

Leo hii utaambiwa kwamba tukitumia mbinu hii ama ile tunatulia na kuwa na amani lakini baada ya muda tunaona hali inakuwa kinyume kabisa. Kila mmoja anaweza kukumbuka kukiri kwa Rais wa Marekani hivi karibuni kwamba harakati zao za kumng’oa Rais wa Libya Gadaffi lilikuwa ni kosa kubwa sana kwa sababu nchi hiyo imeingia katika machafuko ambayo kutulizwa kwake bado ni kitendawili. Yapo matukio mengi tu na yote husababishwa na kiburi cha binadamu kuona kuwa akili, ujanja na uwezo wako ni utimilifu wa yote bila kumweka Mwenyezi Mungu mbele.

Imani ya kikristo inajengwa juu ya msingi wa mitume. Msingi huu ndilo Kanisa ambalo kwalo ndipo tunapata kuingia ndani na kuuona mji mpya wa Mungu, Yerusalemu mpya ambayo inafafanuliwa katika somo la pili. Mji huo ambao huangazwa na Mungu mwenyewe “na taa yake ni Mwana-Kondoo” ni ishara ya upya wa maisha uletwao na Kristo Mfufuka. Tukiingia ndani zaidi tunaona kwamba Kanisa hili ambalo linafunuliwa na jumuiya ya waamini inayoonekana linachipuka ndani kabisa katika nafsi ya kila mmoja wetu. Hii inamaanisha kwamba kila mmoja anapolijenga Kanisa ndani ya nafsi yake atalazimika kumjenga Kristo ndani mwake Yeye ambaye atamwelekeza yaliyo mapenzi ya Mungu ambayo yatampatia amani ya kweli. Uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya kila mbatizwa ni uthibitisho wa kuipatia msingi imara sura hiyo ya Kanisa ndani yao na hapo ndipo atafundishwa na kuongozwa kadiri ya mapenzi ya Mungu.

“Huburini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake, aleluya!” Ni mwaliko tunaopewa kutoka antifona ya mwanzo ya Dominika hii. Sisi Wakristo tunaalikwa kuionesha amani ya kweli ipatikanayo katika Kristo, amani ambayo inajengeka katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Tuueleze ulimwengu kuwa “Bwana amelikomboa Taifa lake!” Ni kweli Yeye aliye mkanilifu na anayejua yote atatuelekeza katika kweli ambayo itatupatia amani ya kweli. Tunaalikwa kutafuta usuluhisho na kufanya mapatano iwe katika familia zetu, katika jumuiya zetu na hata katika jamii ya taifa letu au jamii ya kimataifa kwa kuisikiliza sauti ya Mungu. Kwa maneno mengine tunaalikwa kumtanguliza Mungu kwa njia ya sala na tafakari ya Neno lake na zaidi kujiimarisha kiroho kwa njia ya masakramenti ili kupata ujasiri wa kusonga mbele na kutafuta iliyo kweli inayojengeka katika Kristo na si katika matakwa ya kibinadamu.

Amani ya Kristo inatufunulia huruma ya Mungu! Mwanadamu aliyejeruhiwa na dhambi anatulia moyoni mwake kwa njia ya Fumbo la Pasaka ambalo ni utimilifu wa huruma ya Mungu na linafunua ukuu wa Upendo wa Mungu kwa wanadamu. Tunapokuwa katika adhimisho la Jubilei ya Huruma ya Mungu tunaalikwa kuionja amani hiyo na kuieneza kwa wengine. Tukumbuke kwamba amani hiyo inapatika katika kulishika neno la Kristo. Tukae ndani yake, tumkaribishe ndani yetu. Yeye mwenyewe anatuambia kwamba: “Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake”.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.