2016-04-29 07:28:00

AIF: Ukweli, uwazi na ushirikiano katika masuala ya fedha kimataifa!


Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, (Aif) Alhamisi tarehe 28 Aprili 2016 imewasilisha taarifa ya shughuli zake kwa mwaka 2015 kwa kuonesha habari za kifedha, udhibiti wa fedha: ili kuweza kutenda kwa busara na kudhibiti uwezekano wa utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ufadhili wa vitendo vya kigaidi. Taarifa ya mamlaka hii imetolewa kwa waandishi wa habari na  Dr. Renè Brulhart, Rais wa Mamlaka pamoja na Dr. Tommaso Di Ruzza, Mkurugenzi mkuu wa mamlaka.

Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican kwa mwaka 2015 imejikita zaidi katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ukweli na uwazi katika masuala ya fedha pamoja na kuendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kupambana na vitendo vya kutakatisha fedha sanjari na ugharamiaji wa vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kutishia maisha na usalama wa watu wengi duniani.

Katika kipindi cha mwaka 2015, kumekuwepo utiaji sahihi wa itifaki za maelewano na mamlaka mbali mbali za kisheria katika masuala haya, ili kuweza kubadilishana taarifa; jambo ambalo limeonesha mafanikio makubwa katika upatikanaji wa taarifa muhimu. Mfumo wa kudhibiti dalili za fedha haramu umeimarishwa zaidi na katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na matukio 893 ya usafirishaji wa fedha yaliyotiliwa mashaka. Taarifa zinaonesha kwamba, kwa mwaka 2015 kumekuwepo na matukio 544.

Haya ni matokeo ya kufungwa kwa akaunti ambazo hazikukidhi kanuni, sera, vigezo na sheria za Vatican kuhusiana na masuala ya fedha. Mamlaka ya kodi na mapato kutoka sehemu mbali mbali za dunia zimeendelea kushirikiana na Vatican, hali ambayo inaimarisha mfumo wa udhibiti wa dalili za fedha haramu anasema Dr. Di Ruzza.

Katika kipindi cha mwaka 2015 taarifa 17 zimewasilishwa kwa Ofisi ya Msimamizi mkuu wa haki mjini Vatican kwa ajili ya uchunguzi zaidi unaofanywa na mamlaka ya sheria. Kumekuwepo na ushirikiano mzuri na vyombo vya fedha kimataifa na kwamba, uchukuaji wa fedha taslim zaidi ya Euro 10, 000 ambazo zinakubaliwa kisheria umepungua sana. Hali hii inajionesha pia kwa fedha taslim inayoingizwa.

Haya ni matokeo ya usimamizi na udhibiti bora zaidi wa masuala ya fedha unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha  mjini Vatican, iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 na kufanyiwa marekebisho na Papa Francisko kunako mwaka 2013. Mamlaka hii imetia sahihi itifaki ya ushirikiano na vikosi vya inteligensia ya kifedha na nchi kadhaa duniani, kati yake ni Afrika ya Kusini. AIF kunako mwaka 2013 imekuwa ni mwanachama wa Kundi la Egmont.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.