2016-04-28 07:37:00

Unganisheni maisha yenu na Kristo!


Mara nyingi inaposomwa tanzia hutajwa wasifu wa marehemu na kusisitiza kuenzi na kuendeleza kazi zake. Leo tunaalikwa siyo kuenzi na kuendeleza kazi za Yesu, bali kuunganisha maisha yetu na yake, na kuwa kama Paulo anavyowaandikia Wagalatia “Siyo mimi bali Yesu anayeishi katika mimi.” Dominika iliyopita tulianza kusikia wosia wa Yesu alioanza kuwatolea wafuasi wake baada ya kuondoka Yuda Iskariota. Wafuasi wa Yesu walipogundua kuwa ilikuwa ni lala salama ya kuwa pamoja na Yesu, wakaanza kuhaha na kumhoji maswali mengi. Kabla ya kusikia maneno ya lala salama tuyaweke wazi malumbano ya maswali na majibu kati ya Yesu na wafuasi wake.

Mfuasi wa kwanza alikuwa Petro akamwuliza: “Bwana unakwenda wapi?” Yesu akamjibu, “Niendako huwezi kunifuata sasa; lakini utanifuata baadaye.” Petro hakutosheka na jibu, akaendelea kudadisi: “Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako.” Lakini kwa vile Petro hakuelewa, hapo Yesu akaona amweleze wazi kwamba atamkana. “Amin, amin, nakuambia: Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.” Hapa udadisi wa Petro unatufungua akili juu ya ugumu wa kuzifuata nyayo za Yesu za kujitoa mwenyewe kwa ajili ya wengine, kwani hiyo ni njia ya kwenda kwa Baba.

Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake kuwa wanaijua namna hiyo itakayomwongoza nyumbani kwa Baba aliposema: “Nami niendako ninyi mnajua njia,” hapo Tomaso akamrushia swali la nyongeza: “Bwana, sisi hatujui uendako, tunawezaje kujua njia?” Udadisi wa Tomaso ni kutaka kujua njia itakayomwezesha kufika huko anakoenda Yesu. Naye Yesu akamjibu kiulaini kabisa:“Mimi ndiye njia.” Yesu anapoendelea kuzungumza juu ya kumjua Baba kwa kupitia Yeye: “Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.” Filipo akadakiza: “Bwana utuoneshe Baba inatosha.” Yesu anamjibu mara moja:“Aliyeniona mimi amemwona Baba.” Maswali haya yanataka kuijua jinsi sura ya Mungu wa mbinguni ilivyo.

Jibu la Yesu laonesha kuwa unaweza kumwona Mungu kwa kutafakari uso wake Yesu. Kisha Yesu anasema kuwa atajidhihirisha kwa wale tu wanaotaka kuingia katika mahusiano ya upendo pamoja naye: “Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Maneno hayo yalimkuna mfuasi mwingine aitwaye Yuda lakini siyo yule Iskarioti, akauliza swali. “Kwa vipi mwalimu unajionesha kwa sisi na siyo kwa ulimwengu?” Swali hili linakuja kwa sababu wafuasi walitegemea Yesu angesema anajidhihirisha ulimwenguni kote, kumbe anajidhihirisha kwa wale tu wanaotaka kulinganisha maisha yao na yake.

Ili kuweza kuyaelewa vizuri malumbano na hatima yake katika swali la Yuda, basi tunaletewa mwendelezo wa jibu la Yesu kwa Yuda katika fasuli ya leo inayoanza hivi: “Mtu akinipenda atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.” Ni nafasi pekee Yesu anapoomba kupendwa anaposema: “Mtu akinipenda.” Huu ni upendo wa kufungamanisha maisha yako na yake. Kuwa na mradi mmoja na lengo moja na Yesu. Kisha anasema: “Mtu akinipenda atashika Amri (Neno) langu.” Haina maana ya kushika amri kumi za Musa, bali ni amri ya upendo, yaani kuwasaidia wenye njaa, kiu, fukara nk.

Kadiri ya lugha ya Yohane, ulimwengu ni ule unaoshughulika na mambo ya binafsi. Kumbe Yesu anapendekeza mtu kujisahau mwenyewe na kujitoa kwa wengine. Kwa hiyo Yesu anajidhihirisha katika ulimwengu unaochagua upendo na kujitoa. Ndivyo anavyotaka kusema anapomjibu Yuda. “Kama kuna mtu ananipenda atashika neno langu, na baba yangu atampenda.” Ukiingia katika ushirika wa upendo wa Kristu, hapo moja kwa moja unaingia katika upendo wa Mungu aliye upendo. Kisha anaendelea: “nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.” Hapa haimaanishi unaingizwa katika urika wa utatu mtakatifu, bali kukutana na Mungu ni alama ya uwepo wa roho wa Mungu ndani ya maisha ya binadamu. Mungu anapokuwa nafsini mwa mtu, hali ya mtu huyo inajionesha hadi nje katika haiba na katika kuzungumza, katika kutenda mambo, kwani unakuwa kitu kingine kabisa kwa vile unalingana na upendo wa Mungu. Hivi Mungu amejidhihirisha ndani mwako.

Kuna namna nyingi za uwepo wa Yesu ndani mwetu kama anavyosema: “Anayewapokea ninyi ananipokea mimi, anayempokea fukara ananipokea mimi, pale wawili walipokutana kwa jina langu mimi niko kati yao.” Kumbe, kuna kumpokea Yesu katika fukara na katika jumuyia walipokusanyika wafuasi wa Kristo!. Halafu anatajwa paraclito yaani mfariji, au msaidizi toka kwa Baba: Baba hatawaacheni yatima bali atawapeni Roho Mtakatifu kwa jina langu. Hapa mfariji (paraclito) au msaidizi ni sawa na anayemtuliza mfiwa au mtu mwenye matatizo. Kwa hiyo paraclito siyo jina la Roho mtakatifu, bali ni kazi ya roho aliyoileta Yesu yaani kukaa karibu na kuwa jirani, kwa maneno mengine ni kumwilisha huruma na upendo wa Baba kama allivyofanya Yesu, kielelezo cha Msamaria mwema, changamoto kubwa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Yesu alipokuwa alipoishi hapa duniani alikuwa mfariji (paraclito) wa kwanza aliyekaa karibu na wafuasi, sasa anamtuma mfariji paraclito wa pili. Sisi tunahitaji kuwa na mtu anayekaa jirani, kwani kuna changamoto nyingi sana katika imani yetu kiasi unakuwa na mashaka kama unachofanya au njia unayofuata ndiyo yenyewe au la. Wengi wanafuata njia nyingine, kwa mfano, kuwasamehe maadui, kuwapenda wengine, kujiamini na kujitawala, suala la useja na ubikira, upendo usio na mipaka, maisha ya kifamilia.Zote hizi ni changamoto za maisha ya wafuasi wa Kristo!

Mara nyingi anayefuata mfumo huo wa maisha na kuzungumzia masuala hayo anaonekana kama mgeni anayeishi ulimwengu wa pekee. Kwa hiyo katika mazingira kama hayo, mtu unajisikia mpweke na unahitaji mmoja anayeweza kuwa karibu nawe na kukupa moyo na kukuhimiza katika maisha yako ya imani, na kukuambia kuwa upo sawa na hayo ndiyo maisha ya Yesu. Mtu huyo ndiye paraclito, ni mfariji, ni msaidizi na ni jirani mwema. Kama anavyosema Yesu:“Roho huyo atawatetea, atawakinga” yaani, Roho ndiye anayetetea maisha ya Mungu, dhidi ya sauti zinazoweza kukupotosha. Kwa hiyo roho inayokushauri kufuata sauti ya Kristu, huyo ndiye mfariji, paraclito na msaidizi.

Roho huyo siyo mwalimu wa nadharia ya darasani au anayepepeta mdomo au kusambaza udaku, bali ni mwalimu wa maisha mapya. “Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Toka kwa mfariji huo tunapata nguvu ya ndani inayotupelekea kupenda. Roho anatufanya tuishi na kutenda mambo kama vile ingekuwa huluka ya ndani ya mtu ya kuwa wema. Kama ilivyokuwa kwa Yesu mwenyewe aliyekuwa Mwana kamili wa Mungu katika maisha na katika uwepo wake. Kwa hiyo Roho inatufanya tuwe na ukumbuko hai wa watoto wa Mungu.

Kisha Yesu anaendelea: Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Amani ya ulimwengu ni inapatikana baada ya mapambano yaani baada ya vita moja na nyingine kuna amani. Amani namna hiyo inaisha pale aliyeshinda anaposhindwa kuendelea kumkandamiza yule aliyemshinda. Kwa hiyo hiyo ni amani ya wale wanaowakandamiza wengine. Kumbe, amani ya Krist, ni hii kwamba wote tunakuwa wana wa Baba mmoja na kila mmoja anajitahidi kusimama kidete kutafuta, kulinda na kutetea mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano, hasa zaidi na maskini pamoja na wale wpte wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Kisha Yesu anawatuliza wafuasi wake kwa kuwaambia: “Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Naenda zangu tena naja kwenu.” Yesu anasema ninaondoka lakini ninakuja, katika msisitizo tofauti anaonesha mwendelezo wa uwepo wake. Kwamba anaondoka, lakini hafungi milango, bali uwepo wake sasa ni mzuri zaidi kuliko alipokuwa na mwili wa kibinadamu. Sasa kila kitu kinawezekana na yuko karibu zaidi. Tukiunganisha maisha yetu na yale ya Kristo tunaonesha na kudhihirisha zaidi uwepo wa Kristo katika maisha yetu.

Kwa kutambua kwamba, leo hii kuna mambo mengi yanayomhuzunisha mwanadamu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwilisha matendo ya huruma kwa kuwaonesha jirani zao huruma kama Baba yao wa mbinguni, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.