2016-04-28 08:25:00

Tasnia ya habari na mageuzi mjini Vatican!


Mchakato wa mageuzi unaoendelea kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko mintarafu vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican unapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, vinachangia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote wa Mataifa; kusimamia na kuratibu vyema rasilimali watu na fedha ili kuongeza tija la ufanisi pamoja na kubana matumizi, ili kila senti inayotumika iweze kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu.

Haya ni kati ya mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican, wakati alipokuwa anazungumza na washiriki wa semina ya kumi ya mawasiliano ya jamii iliyoandaliwa na Chuo kikuu cha Kipapa cha Santa Croce, kilichoko mjini Roma. Semina hii inahudhuriwa na washiriki 400 kutoka katika nchi 40 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika tasnia ya habari ulimwenguni.

Kigezo kikuu cha mchakato wa mageuzi ya tasnia ya mawasiliano mjini Vatican ni shughuli za kichungaji. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu miundombinu sanjari na mchakato wa mawasiliano, ili kuweza kukabiliana na changamoto za mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na maendeleo makubwa ya teknolojia. Mageuzi yanayoendelea kufanyiwa kazi kwa sasa yanazingatia kwa namna ya pekee utume wa Kanisa na mambo mengine yote yanafuata.

Lengo ni kuwezesha Injili na Mafundisho ya Kanisa kufika na kugusa nyoyo za watu wengi! Lengo si kuzima dhamana na utume wa Makanisa mahalia, bali kuendelea kuunga mkono juhudi za Makanisa mahalia katika maisha na utume wake, ili kujenga umoja na mshikamano ndani ya Kanisa!. Mageuzi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii mjini Vatican yanagusa kwa namna ya pekee: Radio Vatican, Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV na Gazeti la L’Osservatore Romano. Hapa si mchakato wa kuunganisha vyombo hivi vya habari, bali ni kuhakikisha kwamba, tija na ufanisi zaidi vinapatikana kwa kuzingatia mageuzi makubwa yanayofanywa katika mfumo wa digitali.

Hapa kuna haja ya kuunganisha na kuboresha huduma ya habari inayotolewa na vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Huu ni mfumo mpya wa mawasiliano ya jamii unaoendelea kuboreshwa kwa kuwa ni teknolojia mpya ya mawasiliano, ili kuzima kiu ya mawasiliano inayoendelea kujiokeza katika ulimwengu mamboleo! Mageuzi haya yanataka kuleta mwelekeo mpya katika tasnia ya habari mjini Vatican kwa kusikiliza kwa makini mahitaji ya wasikilizaji, watazamaji na wasomaji wa vyombo vya habari vya Vatican.

Ili kufikia lengo hili, rasilimali watu inapewa pia msukumo wa pekee, ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa kufanya kazi kama timu; kwa kuwashirikisha wadau na kufanya maamuzi ya pamoja; kwa kukazia majiundo awali na endelevu, ili kweli kazi ya timu iweze kuwa na ufanisi mkubwa zaidi kwa kushinda ubinafsi na hali ya kutokuwa na uratibu mzuri zaidi.  

Monsinyo Dario Edoardo Vigano anasema, mchakato huu wa mageuzi katika tasnia ya habari mjini Vatican, unajikita katika mfumo wa uongozi wa kimtandao unaowashirikisha wadau mbali mbali na kuthamini mchango wa kila mtu; kwa kushirikishana na pale panapopungua kujazwa na mchango wa wengine. Ni wakati wa kujielekeza katika kutoa dira badala ya kupokea majibu na kwamba, mahusiano ya kibinadamu na kiutu ni muhimu sana katika mchakato wa mawasiliano ili kujenga na kudumisha mahusiano na urafiki mwema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.