2016-04-28 12:02:00

Roho Mtakatifu analiwezesha na kulitegemeza Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, Alhamisi, tarehe 28 Aprili 2016, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha mjini Vatican anasema, kwa nyakati mbali mbali kama ilivyo hata leo hii, watu wameendelea kumpinga Roho Mtakatifu, lakini ni Roho Mtakatifu ndiye anayewawezesha waamini kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu pasi na woga, kwa kuhakikishia usalama wa maisha.

Baba Mtakatifu amefafanua kwamba, maadhimisho ya Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu kulibuliwa mawazo mazito katika maisha na utume wa Kanisa, lakini ikumbukwe kwamba, mhusika mkuu alikuwa ni Roho Mtakatifu, aliyewakirimia nguvu, ari na ujasiri wa kusonga mbele ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuliwezesha Kanisa kusonga mbele, licha ya mapungufu yake ya kibinadamu.

Wakati wa nyanyaso na madhulumu ni Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kutokana na utendaji wa Roho Mtakatifu usiokuwa na mipaka, baadhi ya viongozi wa Kanisa walidhani kwamba, Yesu alikuja kwa ajili ya Taifa teule peke yake, hali ambayo iliwafanya baadhi ya viongozi wa Kanisa kupingana na Roho Mtakatifu kwa kuwataka watu waliokuwa wamemwongokea Kristo kufuata Sheria ya Musa kwa kutahiriwa, hali ambayo ilisababisha mtafaruku mkubwa katika Kanisa la mwanzo.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Roho Mtakatifu alikuwa anaiandaa mioyo ya waamini kuanza maisha mapya kwa kusonga mbele ili kumshuhudia Kristo Yesu kwani hata wapagani waliweza kumpokea Roho Mtakatifu katika maisha yao! Katika mazingira kama haya, Mitume walijikuta wakiwa na changamoto kubwa katika maisha na utume wao na matokeo yao ni Mtaguso wa Yerusalemu, uliosikiliza kwa makini shuhuda zilizotolewa na Mtume Paulo na Barnaba, kwa kuonesha matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ametenda kupitia kwao.

Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na katika hali ya unyenyekevu kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anawategemeza katika hija ya maisha yao na matokeo yake hata wapagani wanapewa nafuu katika maisha na imani yao bila kulazimika kutahiriwa, hapa Kanisa likapigwa na mshangao wa kazi ya Roho Mtakatifu. Kanisa liliweza kupata ufumbuzi wa changamoto hii kwanza kabisa kwa kukutana, kusikiliza, kujadili, kusali na hatimaye, uamuzi wa busara kutolewa. Hii ndiyo njia anasema Baba Mtakatifu Francisko inayotumiwa na Kanisa hata leo hii.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikabiliwa na changamoto kubwa, hali inayojitokeza hata leo hii. Changamoto kubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kumwilisha dhana ya ”Sinodi” katika maisha na utume wa Kanisa ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa, daima kwa kutambua kwamba, mhusika mkuu hapa ni Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa imani, matumaini na uvumilivu!

Roho Mtakatifu analisaidia Kanisa kushinda kishawishi cha kinzani na kuliwezesha kusimama imara katika imani, kiasi hata cha kuwawezesha waamini kumimina maisha yao kama ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuomba neema na baraka za kuwa wanyenyekevu kwa maongozi ya Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili kufuata njia ambayo Kristo anaitaka kwa ajili ya kila mwamini na kwa Kanisa katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.