2016-04-28 15:22:00

Mchakato wa ushirikiano na Uekumene wa huduma unaendelea!


Mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima uliofanyika hivi karibuni nchini Cuba ni tukio la kihistoria kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox na Cuba ikawa ni uwanja wa kiekumene, tayari kutandaza jamvi la majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika maisha na utume wa Makanisa haya mawili. Ni tukio ambao limeadhimishwa mbali kabisa na Bara la Ulaya ambalo limekuwa ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya Kikanisa katika historia ya mwanadamu.

Viongozi wa Makanisa haya wameonesha masikitiko yao makubwa katika Tamko lao la kichungaji baada ya Makanisa haya mawili kutokuwa na ushirikiano kwa takribani miaka elfu moja na ushehe! Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo yamewapatia ujasiri, ari na mwamko wa kuanza tena upya kwa kuvuka kinzani zilizojikita katika mambo ya kitaalimungu, kitamaduni na kihistoria, ili Wakristo waweze kushikamana tayari kukabiliana na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mambaoleo kwa kuishi kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu, ili kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinazoyaunganisha Makanisa haya mawili!

Hivi ndivyo anavyotafakari Askofu mkuu Ilarione wa Kanisa la Kiorthodox la Russia anapoangalia kwa umakini mkubwa tukio la kihistoria lililowakutanisha viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox huko Havana, Cuba, hapo tarehe 12 Februari 2016. Ni matumaini ya Askofu mkuu Ilarione kwamba, masuala ya kitaalimungu yataendelea kufanyiwa kazi na Tume ya pamoja ya Kitaalimungu baina ya Makanisa haya mawili, ili siku moja, waweze kuwa wamoja chini ya mchungaji mkuu, Kristo Yesu. Changamoto za ulimwengu mamboleo zinahitaji Makanisa yaliyoungana, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili zenye mvuto na mashiko kwa watu!

Mauaji, dhuluma na nyanyaso za Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni changamoto ya kukuza na  kudumisha Uekumene wa damu na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda haki msingi za binadamu. Changamoto hii anasema Askofu mkuu Ilarione imepelekea Marekani na Russia kuanza tena mchakato wa kusitisha mashambulizi huko Syria, tayari kuanza mchakato wa majadiliano yatakayosaidia kupatikana kwa amani ya kudumu. Ni matumaini ya Makanisa kwamba, hata mgogoro wa kivita nchini Ukraine utaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Ili Makanisa haya ambayo kwa miaka mingi yameangaliana kwa jicho la “kengeza” kumekuwepo na haja ya kujenga mwamko wa kuaminiana na hili ndilo chimbuko la Tamko la Kichungaji lililotolewa na viongozi wa Makanisa haya mawili. Hili ni tako linalotandika mkeka wa ushirikiano wa kidugu ili kukabiliana na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo kwa kuwa na ari na mwamko mpya zaidi.

Makanisa haya mawili yamebainisha sera na mikakati ya ushirikiano, ili kutembea kwa umoja na mshikamano; kwa kuwa na maeneo ya hija ya pamoja; ili Wakristo wanapokutana katika maeneo haya waweze kufahamiana na kupendana zaidi. Cuba imekuwa ni mahali ambapo Jumuiya ya Kimataifa imeshuhudia roho ya umoja na mshikamano wa kichungaji; huruma na upendo kwa waliokata tamaa; hamasa ya haki na amani kwa viongozi wa kisiasa na kiuchumi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.