2016-04-25 15:57:00

Wosia wa kitume: Furaha ya upendo ndani ya familia!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina Yetu, Tumsifu Yesu Kristo! Bila shaka utakumbuka kwamba, tarehe 8 Oktoba 2013; Baba Mtakatifu Fransisko alitangaza kwamba mwezi Oktoba 2014 kungekuwa na Sinodi ya pekee  ya Maaskofu kuhusu mambo yahusuyo familia na uinjilishaji. Sambamba na hilo, akatangaza pia kwamba Sinodi hiyo ya pekee ingefuatiwa na sinodi ya kawaida ya Maaskofu kuhusu ndoa na familia kwa mwaka 2015. Hayo matukio yote mawili yalikamilika baraabara kwa muda uliopangwa.

Kadiri ya taratibu za Kanisa letu takatifu sana,  baada ya kukamilika kwa kila mkutano wowote, kunatolewa andiko maalumu, lenye kutuongoza katika utekelezaji wa yale yaliyojri katika mkutano huo.  Na ndivyo ilivyo kwa sinodi zetu mbili tulizozishuhudia kwa mwaka 2014 na 2015. Baada ya yote kukamilika; Baba Mtakatifu Francisko ametoa waraka ulio katika mfumo wa ‘Wosia wa Kitume’, wenye kichwa cha habari Amoris laetitia yaani Furaha ya Upendo. Waraka huu, umesheheni mtazamo na mwongozo wa Kanisa mintarafu ndoa na familia.

Hivyo mpendwa msikilizaji katika vipindi vifuatavyo, tutasafiri pamoja huku tukikumegea machache yaliyosheheni katika waraka huu. Pamoja na kukuletea mantiki iliyobebwa katika waraka huu, tutaambatanisha pia na mashauri ya kichungaji kadiri ya mazingira ya wasilikizaji wetu. Ndani ya Amoris Letitia, Baba Mtakatifu anaanza kwa kusema, furaha ya upendo inayoonjeka katika familia, ni furaha ya Kanisa pia. Kama vile Mababa wa Sinodi walivyobainisha, pamoja na changamoto nyingi zinazokumba mtaala wa maisha ya ndoa; “hamu ya kutaka kuoa na kuolewa inabaki kuwa hai, hususan miongoni mwa vijana; na hilo ni jambo jema sana kwa Kanisa”.

Katika kipengele hiki cha kwanza mpendwa msikilizaji, Kanisa linatazama maisha ya ndoa na familia kama Baraka kwa Kanisa. Na si kwa kanisa tu bali kwa taifa kwa ujumla. Bado Kanisa linakazia juu ya utakatifu na unadhifu wa maisha ya ndoa, inayojengwa kati ya upendo unaowaka katika ya mtu mume na mtu mke. Kanisa linatambua fika changamoto mbalimbali zinazolikumba kanisa la Nyumbani yaani familia; au mtaala wa maisha ya ndoa kwa ujumla wake. Changamoto hizo ni pamoja na masuala ya kiuchumi, masuala ya kijamii na hata masuala ya kibaiologia na kisaikolojia, yanayofanya muungano wa ndoa au maisha ya familia kuwa ni magumu.

Kanisa linaona fahari na faraja tele kwamba, pamoja na changamoto zote hizo, bado ile hali ya kupenda kuoa na kuolewa haijazima mioyoni mwa vijana. Ikumbukwe kwamba, matatizo ni sehemu ya maisha. Hatuwezi kuacha kuyachuchumilia mambo mema kwa sababu ya kuogopa matatizo. Kama vile ajali nyingi za angani hazituzuii kuendelea kusafiri, ajali nyingi za barabarani hazitufanyi tukwepe kutumia magari, matetemeko mengi ya ardhi hayatufanyi tuache kujenga nyumba, kukosa ajira kwingi, hakutufanyi tuache kusoma; hali kadhalika, matatizo na changamoto nyingi zinazowatikisa watu wa ndoa na familia, haziwezi kutufanya tukaacha kupendana na kuoana.  Kuoa na kuolewa ni mtaala uliosisiwa na Mungu mwenyewe, changamoto na matatizo ni matokeo ya mifumo yetu ambayo tunaweza kujitahidi kuidhibiti ili tuendelee kusherehekema maisha katika ndoa na familia.

Mchakato mzima wa sinodi, ulilenga kuangazia na kupembua kwa kina hali ya familia katika ulimwengu mambo leo, na kutazama kwa mapana zaidi umuhimu wa maisha ya ndoa na familia. Changamoto zilizojitokeza katika sinodi hizo, ziliashiria umuhimu wa kuendela kuwa na mdahalo wazi juu ya masuala ya kitasaufi, kimaadili na kichungaji mintarafu ndoa. Namna ya kufikiri ya wachungaji wetu na wanataalimungu; huku wakidumu kuwa waaminifu kwa Kanisa, wahalisia na wabunifu; daima kutatusaidia kupata mwanga mkubwa sana.

Mpendwa msikilizaji, daima tunaalikwa kuwa na masikio yanayo sikia na kusikiliza, pia kuwa na akili pembuzi, yenye uwezo wa kuchuja mambo, kutofautisha kati ya mafundisho ya Kanisa na maelezo ya vyombo vya habari. Mara si chache, vyombo vya habari vimekuwa vikitoa ufafanuzi potofu juu ya mafundisho ya Kanisa. Wajanja wachache wamekuwa wakipotosha ulimwengu kwa kusema yale wanayopenda wao yasemwe na siyo mafundisho ya Kanisa, wala tanzu ya imani yetu. Kwa mantiki hiyo kipengele cha pili cha waraka wetu ‘Amoris Letitia’, kinaonya juu ya wanahabari wa kiulimwengu wenye shauku isiyoratibiwa ya kutamani mabadiliko tu yasiyo na misingi; jambo ambalo lingetatua kila kitu kwa kutumia kanuni za jumla, au kutoa uelewa wa jumla kutokana na uwelewa wa jambo fulani halisia.

Hivyo basi, kila jambo lina namna yake ya kulitazama na kulielewa. Masuala ya kiimani, hayatazamwi kwa macho ya kisiasa au kishabiki. Masuala ya kikanisa, yanatafsiriwa na Kanisa. Kadiri ya taratibu za Kanisa letu, mwenye mamlaka ya kutoa ufafanuzi stahiki kwa masuala yanayoliongoza Kanisa, ni yule tu mwenye mamlaka halali ndani ya kanisa kufanya hivyo, au  yule ambaye ametumwa na mamlaka halali kufanya hivyo. Waraka tulionao mkononi sasa hivi, ndiyo ufafanuzi sahihi wa mambo yale yaliyojiri katika Sinodi za maaskofu mintarafu ndoa na familia. Waraka huu ndio mwondoko mpya wa Kanisa baada ya Sinodi. Tuendelee kushirikiana ili tuelewe Kanisa linatueleza nini juu ya ndoa na familia.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni Mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.