2016-04-25 15:31:00

Wafungwa washeni moto wa imani na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wafungwa wanaotumikia adhabu yao huko Velletri, Italia kwa kumwandikia barua inayoonesha shida, mateso na mahangaiko yao ya ndani na kwamba, anawakumbuka na wakati mwingine hata yeye mwenyewe anatafakari kuhusu hali ya gereza katika maisha yake. Kutokana na changamoto hii, ndiyo maana wakati wa hija zake za kitume anapenda kukutana na kuzungumza na wafungwa Gerezani, ili kuwaonesha upendo na uwepo wake wa karibu katika shida na mahangaiko yao!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kutakuwepo na siku moja kwa ajili ya Jubilei ya wafungwa, siku ambayo Kanisa litashikamana kwa pamoja kwa ajili ya kusali na kuwaombea wafungwa magerezani, kielelezo cha uwepo wa karibu kiroho! Baba Mtakatifu anawaambia wafungwa kutoka kata tamaa, bali waendelee kuwa na matumaini hata pake wanapodhani kwamba, muda kwao umesimama na wala hausongi mbele!

Baba Mtakatifu anawataka wafungwa kuendea kuwasha moto wa matumaini na imani ili kuyaangaza mapito ya maisha yao. Waendelee kumwomba Yesu Kristo Mfufuka ili aweze kuwa kipimo cha muda na matumaini yao, ili waweze kuishi kipindi hiki kigumu cha maisha yao pasi na kukata tamaa ya imani, kwani kamwe Yesu hawezi kumtelekeza mtu awaye yote, anayekimbilia ulinzi na tunza yake! Wafungwa watambue kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu, licha ya matatizo na changamoto za maisha wanazokumbana nazo.

Wafungwa wawe na ujasiri wa kuondokana na historia na maisha ya zamani, tayari kukua na kukomaa katika imani na upendo kwa kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwafunda upya kutokana na mang’amuzi ya adhabu zao gerezani. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, kuna watakatifu wengi ambao wamefikia utakatifu wa maisha kwa njia ya taabu na suluba nyingi za maisha, lakini wakawa tayari kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, aliyegeuza mchakato wa maisha na leo hii wamekuwa kama walivyo, changamoto endelevu hata kwa wafungwa wa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa wafungwa wa Gereza la Velletri uliowasilishwa kwao na Askofu Marcello Semeraro alipotembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu gerezani hapo hivi karibuni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.