2016-04-25 08:59:00

Penye msitu kuna msamaha na maisha; penye Jangwa: utupu na kifo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 24 Aprili 2016 majira ya jioni ametembelea “Kijiji cha Dunia”, kilichoko mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Dunia iliyoandaliwa na Chama cha Kitume cha Wafokolari. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Chama hiki wanaoendelea kujikita katika mchakato wa kugeuza majangwa kuwa ni misitu na mahali bora zaidi pa mwanadamu kuishi! Penye misitu hapo kuna zawadi ya maisha na penye jangwa huko kuna utupu na kifo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna majangwa ya maisha yanayoendelea kujitokeza mijini na katika maisha ya watu binafsi, kiasi hata cha watu kukosa dira, mwelekeo na matumaini ya maisha kutokana na maamuzi mbele, woga na hofu zisizo na mashiko! Hawa ni watu wanaoishi na kufariki dunia katika majangwa ya miji na kwamba, Kanisa litaendelea kuunga mkono jitihada za vyama vya kitume katika kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Watu wajitahidi kupokea zawadi ya maisha pasi na woga na kwamba, kinzani za maisha ni hatari, lakini pia ni fursa za kujenga na kudumisha mshikamano wa huruma na upendo kama alivyofanya Msamaria mwema! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wafokolari kwa huduma makini wanazotoa kwa wafunga magerezani, kielelezo cha huruma ya Baba wa mbinguni, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kinzani na mipasuko ya kijamii itaendelea kuwepo, changamoto kwa binadamu ni kuikubali na kuipatia ufumbuzi, badala ya kuigeuzia kisogo. Jangwa la maisha ya watu na upweke hasi unaojionesha mijini ni changamoto kwa watu kushirikiana kwa dhati, ili kuweza kugeuza majangwa na upweke huu kuwa ni misitu na chemchemi ya maisha mapya yanayojikita katika uhuru, haki na furaha. Mchakato wa mabadiliko kutoka katika jangwa kuelekea katika msitu unafumbata ndani mwake chemchemi ya maisha na furaha ya kweli!

Baba Mtakatifu anasema, leo kuna watu wengi ambao wamegubikwa na wasi wasi, woga na majonzi katika maisha, hawana furaha, huruma na mapendo hata kidogo! Ni watu waliojifungia katika undani na ubinafsi wao, kiasi cha kukosa urafiki wa kijamii; matokeo yake ni: chuki, uhasama na vita inayoendelea kuzagaa sehemu mbali mbali za dunia kama walimwengu wanavyoshuhudia kwa sasa! Urafiki jamii unajikita katika msamaha, sadaka na furaha ya kuwa wamoja kwa hali na mali; binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza katika medani mbali mbali za maisha.

Lakini kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu, watu wamempuuza mwanadamu na matokeo yake, fedha na mali vinashika hatamu! Maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi wanaishia kunyanyaswa na baa la njaa, umaskini, magonjwa na unyoywaji; hali inayojitokeza kwa namna ya pekee kwa watoto na vijana! Sadaka ya maisha ni jambo muhimu sana ambalo linamwezesha mtu kushirikiana na jirani zake, tayari kutengeneza msitu unaofumbata maisha na upendo, tayari kusamehe na kusahau ili kusonga mbele na kuambata huruma ya Mungu katika maisha ya binadamu. Msamaha una mvuto wa nguvu unaowawezesha watu kujenga madaraja ya kukutana na wala si kuharibu.

Baba Mtakatifu anasema, yote haya yanawezekana kutendeka kwani ni sehemu ya maisha ya mwanadamu yanayowawezesha kufanya kazi kwa pamoja huku wakidumisha majadiliano ya kidini, kiekumene, kijamii na kitamaduni, huku wakiheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, kielelezo makini cha jangwa linalogeuka kuwa ni msitu mnene wa maisha, furaha na matumaini mapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.