2016-04-25 08:03:00

Mapambano ya baa la njaa duniani yanahitaji uchumi endelevu!


Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi kwa kujikita katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Binadamu anakumbushwa kwamba, amekabidhiwa kazi ya kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, dhamana inayojikita katika haki. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo kwa kuondokana na tabia ya uharibifu wa chakula ambacho kingeweza kuganga njaa sehemu mbali mbali za dunia. Sekta ya uchimbaji wa madini haina budi kuwanufaisha wananchi sanjari na kulinda mazingira kwa kutumia teknolojia rafiki, daima binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza! 

Kwa ufupi haya ndiyo mawazo makuu yaliyotolewa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Jumatatu, tarehe 25 Aprili 2016 kwenye mkutano wa siku mbili kuhusu mazingira ulioandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Utunzaji wa nyumba ya wote katika mtazamo mpana wa uwekezaji katika sekta ya uchimbaji wa madini na kilimo”.

Kardinali Turkson amepembua changamoto hii mintarafu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” “Laudato si”. Amekazia umuhimu Waraka huu unaogusa medani mbali mbali za maisha na vipaumbele vya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Mazingira ni kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kuyatunza na kuyaendeleza. Uharibifu wa mazingira unaendelea kusababisha madhara makubwa katika maisha ya watu, kiasi hata cha kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu, changamoto ya kujikita katika ekolojia endelevu, majadiliano, uaminifu na matumaini katika ujenzi wa nyumba ya wote! Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa inayofumbatwa katika fumbo la: Uumbaji, Umwilisho na Ukombozi; mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Binadamu anapaswa kudumisha umoja, ushirikiano na udugu; mambo yanayopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu kama sehemu ya mchakato wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto endelevu inayohitaji mageuzi katika teknolojia, ili kuambata teknolojia rafiki kwa mazingira; mageuzi katika tabia na mtindo wa maisha kiroho na kimwili kwa kutambua kwamba amani ni jina jipya la maendeleo ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu katika waraka wake anawataka walimwengu kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu; mafao, ustawi na maendeleo ya wengi kwa kuondokana na ubinafsi, tayari kudumisha mshikamano unaongozwa na kanuni ya auni: kioo cha mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu. Watu wawe na mwamko wa kutunza mazingira ili yaweze kuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na kile kijacho kwa kujikita katika haki! Lengo ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mgawanyo mzuri wa rasilimali ya dunia unaodhibitiwa na kanuni maadili na uwajibikaji makini.

Kardinali Turkson anakaza kusema, shughuli za binadamu zimekuwa na athari kubwa katika sekta ya kilimo na uchimbaji wa madini; matokeo yake ni sekta ya kilimo kukabiliwa na changamoto ya kulisha watu billioni saba! Baa la njaa na utapiamlo linahitaji mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira, kwa kukazia ekolojia endelevu na kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ili kulisha idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sera makini za kilimo endelevu; utunzaji bora wa vyanzo vya maji na uzalishaji bora wa mazao ya chakula na kilimo, ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani.

Baba Mtakatifu katika waraka wake anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya kilimo, ili kupambana na baa la njaa na utapiamlo; kwa kulinda na kutunza mazingira sanjari na uwepo wa utawala bora unaozinatia sheria. Serikali ziwekeze katika miundombinu ya barabara, masoko; kilimo cha umwagiliaji na teknolojia rafiki pamoja na kuwa na mgawanyo bora zaidi wa rasilimali za dunia kwa ajili ya wote.

Katika sekta ya uchimbaji wa madini, Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, Makampuni makubwa ya madini yameendelea kujitajirisha zaidi kwa rasilimali ya dunia ili kutosheleza soko la kimataifa, lakini kwa hasara ya wananchi mahalia wanaokabiliwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Uchimbaji wa madini uzingatie ustawi na mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu na kwamba, uwekezaji unaofanywa uweze kuwa ni kikolezo cha maendeleo endelevu badala ya uchu wa mali na faida kubwa!

Kardinali Peter Turkson anaiambia familia ya Mungu nchini Zambia kwamba, waraka wa Baba Mtakatifu kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, unajikita katika utu na heshima ya binadamu; umoja na mshikamano katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira; kwa kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.