2016-04-25 06:58:00

Kanisa na utunzaji bora wa mazingira Zambia


Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia kuanzia tarehe 25- 26 Aprili, 2016 linafanya mkutano wa kitaifa ili kupembua kwa kina na mapana athari za uchimbaji wa madini katika sekta ya kilimo na utunzaji bora wa mazingira. Mkutano huu unatarajiwa pia kuhudhuriwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani. Hii itakuwa ni nafasi kwa familia ya Mungu nchini Zambia kuweza kufanya tafakari ya kina kuhusu Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote, Laudato si!

Haya yamefafanuliwa na Padre Cleophas Lungu, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia ambaye amekaza kusema, Kardinali Turkson, atatoa hotuba elekezi katika mkutano huu wa siku mbili kwa kutambua kwamba, Zambia ni kati ya nchi ambazo kwa miaka ya hivi karibuni imeathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo inatishia mchakato wa uchumi na maendeleo kwani uzalishaji wa umeme katika Bwana la Kariba umepungua sana kutokana na kina cha maji kuendelea kushuka mwaka hadi mwaka, hali ambayo imepelekea Shirika la Umeme nchini Zambia, ZESCO kuanza kutoa umeme wa mgao.

Athari za mabadiliko ya tabianchi Zambia na matokeo ya ukataji miti ovyo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani! Zambia imebahatika kuwa na ardhi yenye rutuba nzuri kwa shughuli za kilimo, lakini uharibifu wa mazingira unaendelea kusababisha madhara makubwa hata katika sekta ya kilimo. Athari hizi zinachangiwa pia na uchimbaji wa madini kwa kiwango kikubwa unaofanywa nchini Zambia. Katika changamoto kama hizi anasema Padre Lungu, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Zambia kubadilika kitabia na kuanza kuwa na mwelekeo mpya katika maisha. Mkutano huu unahudhuriwa pia na wajumbe wawakilishi kutoka katika baadhi ya nchi za kiafrika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.