2016-04-24 11:20:00

Waliotekwa nyara sehemu mbali mbali za dunia wakumbukwa na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watoto, Jumapili, tarehe 24 Aprili 2016, wakati wa sala ya Malkia wa mbingu, ametumia nafasi hii kuwashukuru watoto waliofika kwa wingi ili kuadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa kuishi na kushuhudia imani yao inayojikita katika udugu. Amewashukuru kwa furaha na ushuhuda wa maisha yao mjini Roma. Amewataka watoto hawa kusonga mbele kwa imani na matumaini!

Baba Mtakatifu amewakumbuka pia Padre Valentin Palencia Marquina, Shahidi wa imani pamoja na mapadre wenzake wanne waliotangazwa kuwa wenyeheri huko Burgos, Hispania kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa mashuhuda hawa wa imani waliouwawa kikatiliki nchini Hispania wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kwa sala na maombi yao, wenyeheri hawa wapya wasaidie kuikoa dunia kutoka katika vita na mipasuko ya kijamii.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, bado anawakumbuka: Maaskofu, Mapadre na Watawa wa Kanisa Katoliki la Kanisa la Kiorthodox waliotekwa nyara kitambo sasa huko Syria. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma ili aguse nyoyo za wateka nyara hawa, ili waweze kuwaachia huru mapema iwezekanavyo, ili waweze kurejea tena katika jumuiya zao. Kwa nia hii, Baba Mtakatifu amewaalika waamini wote kuendelea kusali na kuwaombea watu waliotekwa nyara sehemu mbali mbali za dunia. Mwishoni, ameyaweka matumaini ya familia ya Mungu chini ya maombezi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa huruma! Baba Mtakatifu amewataka vijana hawa baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei y ahuruma ya Mungu kwa watoto, kurejea makwao wakiwa na furaha inayojikita katika utambulisho wa Kikristo ambao umepigwa chapa moyoni na akilini mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.