2016-04-24 10:06:00

Kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari Armenia, 1915!


Familia ya Mungu nchini Armenia inafanya kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari 'Metz Yeghern' yaliyotokea kunako tarehe 24 Aprili 1915. Tukio ambalo limeadhimishwa kwa makesha na Ibada ya Misa Takatifu. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, Jumamosi jioni, ameshiriki katika mkesha wa kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari huko Armenia, ili kuwakumbusha walimwengu matukio ambao yameacha kurasa chungu katika historia ya maisha ya mwanadamu, tayari kuanza mchakato wa uponyaji, upatanisho na msamaha wa kweli ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kardinali Sandri anakaza kusema, kumbu kumbu ni muhimu sana kwa ajili ya kutafakari mambo ambayo yamedhalilisha: maisha, utu na heshima ya binadamu. Ni matukio yanayojikita katika utamaduni wa kifo, yaani vita, nyanyaso na madhulumu na kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha Injili ya uhai ili kuwa na mwelekeo mpya na matumaini mapya katika maisha. Hata leo hii bado kuna makovu ya machungu yaliyosababishwa na mauaji haya ya kimbari na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusaidia suluhu ya mgogoro huu kwa wananchi wanaoishi huko Armenia. Kinzani na vita kwa misingi ya kidini na kisiasa haina nafasi tena, bali watu waanze mchakato wa uponyaji, msamaha, upatanisho na umoja wa kitaifa!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mwezi Juni, 2016 anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Armenia na huko Azebaigian, Georgia, ili kuendelea kujenga madaraja ya watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, tayari kuendeleza majadiliano ya kiekumene yanayosimiwa katika huduma ya upendo na mshikamano kati ya waamini. Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Armenia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani.

Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwafariji wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili, ili katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waweze kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu unaokoa na kuponya. Wananchi wawe na ujasiri wa kushinda kishawishi cha vita, kinzani, mipasuko na utengano kwa misingi mbali mbali, tayari kuambata ushuhuda unaothamini, tetea na kudumisha maisha, utu na heshima ya binadamu.

Katika kinzani na vita, waathirika wakubwa anasema Kardinali Sandri ni wanawake, watoto na wazee, mambo ambayo kwa sasa si habari inayopewa kipaumbele cha kwanza. Lakini Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kuwakumbusha walimwengu kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ipo na inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee na ndiyo maana, alitembelea kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kuchaguliwa kwake huko Lampedusa, Kusini mwa Italia na hivi karibuni ametembelea pia huko Lesvos, Ugiriki! Haya ni matukio ambayo yanakwenda kinyume cha maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Yanaendelea kujitokeza huko Mashariki ya kati. Baba Mtakatifu kama kiongozi na mchungaji mkuu wa Kanisa anaendelea kuwahamasisha walimwengu kuguswa na mahangaiko ya maskini, wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha.

Ni matumaini ya Kardinali Sandri kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Armenia itasaidia kuanza mchakato wa kuandika ukurasa mpya unaojikita katika misingi ya haki, amani, upendo, msamaha, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kinzani, vita na mipasuko ya kijamii ni majanga katika maisha ya watu wengi1

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.