2016-04-23 13:02:00

Ubaguzi wa kidini na kikabila unaweza kusababisha majanga katika jamii!


Monsinyo Janusz Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirikisho la Usalama na Ushirikiano Ulaya, OSCE, hivi karibuni ameshiriki na kuchangia taarifa ya mkurugenzi wa Ofisi ya taasisi za kidemokrasia na haki za binadamu kwa kuonesha umuhimu wake katika ustawi na maendeleo ya binadamu. Ujumbe wa Vatican pamoja na kukiri mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika Ofisi hii, lakini pia umegusia umuhimu wa Serikali za nchi wanachama OSCE kuheshimu na kutekeleza sera na mikakati iliyobainishwa, ili kukuza na kudumisha maendeleo na usalama kwa nchi wanachama wa OSCE.

Monsinyo Urbanczyk amekumbusha kwamba, OSCE ni jukwaa muhimu sana la shughuli za kisiasa mintarafu: ulinzi na usalama, kumbe, sheria, kanuni na taratibu zake hazina budi kufuatwa kikamilifu. Ukosefu wa maridhiano na sera za kibaguzi ni kati ya mambo yanayochangia kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, kiasi cha kuhatarisha amani, utulivu na usalama duniani. Dhana ya ubaguzi wa kidini na kikabila inaweza kuonekana na wengi kuwa imepitwa na wakati, lakini kuna maeneo ambayo Wakristo wanateseka na kunyanyasika kutokana na imani yao.

Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu, umewataka viongozi wakuu wa OSCE kuandaa mwongozo utakaosaidia kupambana na sera za kibaguzi na ukosefu wa maridhiano kati ya watu, bila kusahau kwamba, Wakristo ni kati ya makundi yanayotengwa sana Barani Ulaya kana kwamba, wao ni raia wa daraja la pili!. Uhuru wa kidini ni jambo muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya wengi na kamwe usipuuziwe na kwamba, kipimo cha utekelezaji wa uhuru wa kuabudu kinafumbatwa kwa namna ya pekee katika utekelezaji wa haki msingi za binadamu. Ujumbe wa Vatican umekazia pia umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliani ya kidini na kiekumene; kisiasa na kidiplomasia; ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na usalama kwa raia wote. Majadiliano ya kina na hali ya kuaminiana kati ya wanachama wa OSCE ni muhimu sana ili kuweza kupata ufanisi zaidi katika utekelezaji wa mikakati na maazimio ya OSCE.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.