2016-04-23 14:02:00

Papa Francisko atoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu George, Shahidi sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanaongozwa na  kauli mbiu “Kukua katika huruma kama Baba wa mbinguni”, Jumamosi, tarehe 23 Aprili 2016, amejiunga na Mapadre wengine 150 ili kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto wenye umri kati ya miaka 13- 16 wanaoshiriki maadhimisho ya Jubilei ya watoto hapa mjini Vatican.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amewaungamisha watoto kumi na sita kuanzia saa 5: 30 hadi saa 6: 45 majira ya mchana kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu kama mapadre wengine walitawanyika kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ili kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto ambao walikuwa wanakimbilia huruma ya Mungu kama sehemu ya masharti pia ya kupata rehema kamili wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ni uhakika anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Uso wa huruma kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni kiini cha uhakika wa huruma ya Mungu kwa sababu inamfanya mwamini aguse kwa mkono wake ukuu wa huruma ya Mungu katika maisha yake na kwamba, toba ya kweli ni chimbuko la amani ya ndani!

Kilele cha Jubilei ya watoto ni Jumapili, tarehe 24 Aprili 2016, majira ya saa 4:30 asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko atakapoongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jubilei ya watoto wa Kanisa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Waandaaji wa Jubilei ya watoto wanasema, hizi ni siku kuu tatu za sherehe, sala, tafakari, toba na ibada mbali mbali kama sehemu ya hija kuelekea katika Lango la Huruma, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika watoto kuchuchumilia toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha hata katika udogo wao. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Jumamosi tarehe 23 Aprili 2016, watoto wataianza siku kwa hija kuelekea kwenye Lango la Huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kuna Mapadre waungamishaji 150 watakaoshiriki kikamilifu katika kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto hawa. Watahitimisha hija hii kwa kukiri Kanuni ya Imani kuzunguka Kaburi la Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.