2016-04-23 12:02:00

OSCE inapaswa kudumisha uhuru wa kidini dhidi ya sera za kibaguzi!


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha maridhiano kati ya watu ili kuondokana na sera pamoja na vitendo vya kibaguzi dhidi ya wakristo katika nchi za Ulaya. Hii inatokana na ukweli kwamba, haki za kidini au kiimani zinaendelea kumong’onyoka kwa kasi kubwa Barani Ulaya, hali ambayo inakinzana kimsingi na uhuru wa kuabudu ambayo ni haki msingi ya kila raia.

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Monsinyo Janusz Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirikisho la Usalama na Ushirikiano Ulaya, OSCE, wakati walipokuwa wanajadili sera na mikakati ya kudumisha maridhiano ili kuondokana na ubaguzi dhidi ya Wakristo Barani Ulaya. Kuna baadhi ya viongozi wa serikali wanaopania kwa hali na mali kuhakikisha kwamba, wanafifisha uhuru wa kidini au kuudhalilisha ili usiwe na sauti tena katika maisha ya hadhara.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alipokuwa Jimbo kuu la Philadelphia, mwaka 2015, aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuunganisha sauti zao kudai: amani, maridhiano, heshima, utu na haki msingi za binadamu. Monsinyo Janusz Urbanczyk anakaza kusema, kuna ubaguzi mkubwa unaoendelea kujitokeza katika Nchi zinazounda Shirikisho la Usalama na Ushirikiano Ulaya, OSCE. Wakristo wanaendelea kunyimwa sauti katika maisha ya hadhara, hali inayodhoofisha uhuru wa kuabudu, kinyume kabisa na Mkataba wa Helnsinki.

Mwelekeo mwingine unaoendelea kujitokeza ni kukataa katu katu mchango wa dini na imani katika maisha ya hadhara na sera za nchi; mambo ambayo kimsingi yanapania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kutaka Jamii iweze kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wazee na wagonjwa. Mchango wa dini unapania kukuza na kudumisha amani, usalama na umoja kati ya wananchi.

Baadhi ya Serikali na vyombo vingi vya mawasiliano ya jamii Barani Ulaya vimeonesha udhaifu mkubwa katika kukuza na kudumisha maridhiano kati kati ya watu kiasi hata cha wakati mwingine kuragibisha sera zinazokwenda kinyume na: imani, kanuni na maadili ya Kikristo, kielelezo makini cha sera za kibaguzi. Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, OSCE itaweza kusimama kidete kulinda, kudumisha na kuendeleza haki msingi za binadamu sanjari na kuondokana na sera za kibaguzi wanazofanyiwa Wakristo kana kwamba, ni dini hatari kwa usalama na ustawi wa nchi wanachama wa OSCE. Ikiwa kama sera na mikakati hii haitaweza kudhibitiwa kikamilifu, Jamii inaweza kujikuta inatumbukia katika maafa makubwa. Uhuru wa kidini ni jambo muhimu sana na ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwenye mkutano wa OSCE kwamba, mawaziri wenye dhamana ya kulinda na kudumisha uhuru wa kidini wataweza kuifanyia kazi changamoto hi ina hatimaye, kuitolea tamko la jumla!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.