2016-04-23 15:17:00

Msumbiji tarehe 22 Mei 2016 kuombea amani!


Katika maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Mungu mmoja mwenye nafsi tatu: Mungu Baba Muumbaji; Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayelitakatifuza Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, hapo tarehe 22 Mei 2016 litapiga magoti kumlilia na kukimbilia huruma ya Mungu kwa ajili ya kuombea amani na usalama nchini mwao! Sadaka na mchango utakaotolewa siku hii, utakusanywa kwa ajili ya kusaidia huduma ya huruma na mapendo kwa wananchi wa Msumbiji wenye kuhitaji msaada zaidi!

Uamuzi huu umefikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, CEM, katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni. Kwa muda mrefu sasa, kumekuwepo na mgogoro wa kisiasa unaotishia amani, usalama, umoja na mshikamano wa kitaifa kutokana na malumbano ya kisiasa kati ya FRELIMO na Chama cha upinzani cha RENAMO. Kutokana na mapigano yanayoendelea chini kwa chini kati ya Serikali na RENAMO, baadhi ya wananchi wa Msumbiji wamelazimika kukimbilia mpakani kati ya Msumbiji na Malawi, ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kabisa na wananchi wote wanaoendelea kuteseka kutokana na vita na malumbano ya kisiasa yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Msumbiji katika ujumla wake. Maaskofu wanakaza kusema, wao kama Kanisa hawana ushabiki wa chama chochote kile cha kisiasa, bali wataka kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na vita isiyokuwa na kichwa wala miguu!

Maaskofu wanawaomba viongozi wa FRELIMO na RENAMO kuonesha ujasiri na utashi wa kisiasa ili kurejea tena katika majadiliano yanayojikita katika ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Msumbiji, ili amani ya kweli iweze kupatikana na hatimaye, kutawala akili na mioyo ya watu. Haya ni majadiliano ambayo yanapaswa pia kuwahusisha wananchi kwani wao ndio waathirika wakubwa wa malumbano na vita visivyokuwa na tija hata kidogo!

Ufike wakati, viongozi hawa waweze kuibuka na mbinu mkakati utakaotekelezeka, ili amani iweze kupatikana na hatimate kuzika tofauti, chuki na uhasama wa kisiasa ambao umedumu kwa miaka mingi na hivyo kuwa ni kikwazo cha haki, amani, upendo na mshikamano na umoja wa kitaifa. Vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii imedumaza hata ukuaji wa uchumi, kwani wawekezaji wengi wanashindwa kuwekeza kutokana na ukosefu wa uhakika wa usalama na amani nchini Msumbiji.

Wafadhili wamegoma kutoa msaada kwa ajili ya maendeleo ya nchi kutokana na vita na kwamba, sekta ya utalii imeathirika vibaya. Zaidi ya watoto thelathi na sita elfu hawana nafasi ya kuendelea na masomo kutokana na wasi wasi ya vita na kinzani za kijamii. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wananchi wa Msumbiji elfu kumi na moja ambao wamekimbilia nchini Malawi ambako hata wao wanateseka kutokana na hali ngumu ya uchumi na ukame wa kutisha. Nguvu kazi na rasilimali watu inakosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha, ili kuchangia katika mchakato wa kukuza na kuimarisha uchumi kwa sababu ya uchu wa mali na madaraka kutoka kwa watu wachache ndani ya jamii! Maaskofu wanauliza swali la msingi, Je, wanasiasa wanataka kuipeleka wapi Msumbiji na watu wake?

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linakaza kusema, kuna haja kwa RENAMO na FRELIMO kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kina na upatanisho wa kitaifa, ili kujenga na kudumisha amani sanjari na kuhakikisha kwamba Makubaliano ya  Amani yaliyotiwa sahihi kunako mwaka 1992 mjini Roma, yanatekelezwa kwa umakini mkubwa. Vita iliyojitokeza huko nyuma, ilisababisha watu zaidi ya millioni moja kuathirika na kwamba, hakuna haja tena ya kuwa na vita, watu wamechoka na wanataka amani ya kudumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.