2016-04-22 11:55:00

Upendo ndio utambulisho wa Mkristo!


Tangazo moja la biashara lilikuwa linaitambulisha bidhaa iliyoukuwa inatangazwa kwa kuonesha kwamba pale mmoja anapoitumia bidhaa hiyo anakuwa tofauti na wengine. Kauli mbiu yake iliyotumika ambayo ilikuwa katika lugha la kiingereza ni “stand out of the crowd” ambayo inaweza kutafsiriwa “jiweke nje ya umati”. Kuna tofati kati  umati na kundi. Umati wa watu ni mkusanyiko wa watu ambao hawaunganishwi na kitu chochote. Kila mmoja anakuwa na shughuli yake na yenye malengo binafsi. Kundi la watu kwa upande mwingine linadai kuwa na nia fulani maalum. Kwa mfano unaweza kusikia juu ya kikundi cha vijana wanaharakati wa mazingira na vikundi vinginevyo vingi ambavyo huwa na malengo mahsusi.

Maisha yetu ya kikristo yanatufanya sisi kuwa kundi moja ambalo linapata pia utambulisho kwa kuwa na lengo moja au njia moja. Sisi kama Wakristo hatupaswi kuwa kama umati tunapaswa “kujiweka nje ya umati” na kujitambulisha kadiri ya hadhi yetu. Dominika hii ya tano ya Pasaka inatuelekeza katika kutambua na kutafakari kwa kina huo utambulisho wetu. Injili ya leo linatuwekea mbele yetu mwongozo ambao unatufanya tuweze kweli “kujiweka nje ya umati”. Utambulisho huo ni upendo: “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile mimi nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo”. Kristo anatupatia utambulisho huo kama amri. Hii inamaanisha kwamba hili si jambo la hiari bali na hitajiko la lazima katika kuifunua hadhi yetu: “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi”.

Kristo anaendelea kuonesha kuwa kipimo cha upendo huo ni Yeye Krsito mwenyewe: “kama mimi nilivyowapenda ninyi”. Hili ni dokezo zuri ambalo linatufanya sisi wakristo kweli “kujiweka nje ya umati”. Upendo wa Kristo kwetu sisi wanadamu ambao unatafsiriwa katika lugha ya kiyunani kama “agape” ni upendo usio na kipimo, upendo usio na mipaka na ni upendo ambao unapenda kwa sababu tu mmoja anastahili kupendwa. Ni upendo ambao unapenya ndani kabisa katika uzuri na ukamilifu wa asili ya mwanadamu na si katika makandokando ambayo si sehemu yake mwanadamu. Sifa za upendo huu zinafafanuliwa vizuri katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto sura ya 13. Upendo huu ni kinyume na upendo ni kinyume na upendo wa kidunia ambao unatafsiriwa katika lugha ya kiyunani kama “eros”, aina fulani ya upendo ambao katika ujumla wake unaonesha ubinafsi na kujijali mwenyewe, upendo ambo unaweza kuitwa upendo wa nipe nikupe au nitakupenda kwa sababu ya haiba fulani au kwa sababu ya kutenda kitu fulani.

Maisha ya kikristo yanapokea tunu hii ya upendo na kufanya upya maisha ya kibinadamu na upya huu wa maisha ndiyo unaifunua huruma ya Mungu. Mtume Yohane anayafafanua maisha haya katika somo la pili: “Mimi Yohane, nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita”. Jumuiya ya kikristo ni jumuiya ya kipasaka. Ni katika fumbo la Pasaka ndipo tunaona utimilifu wa ufunuo wa huruma ya Mungu. Ukristo ambao unapambwa na Upendo wa kimungu unatuweka nje ya umati wa jamii ya kisasa. Hiyo ndiyo hali anayoiona Mtume Yohane na ndicho ambacho tunapaswa kukionesha kama bendera yetu na utambulisho wetu wa kikristo. Wakati tunakianza kipindi hiki cha Pasaka tuliombwa kushuhudia maisha ya kipasaka. Ushuhuda huo unajikita katika upya huu wa maisha na upya huo unaoimarishwa na Upendo wa kikristo.

Jumuiya hii mpya inaujenga upya ubinadamu wetu. Hapa tunaiona huruma ya Mungu inavyojengeka katika upendo wake na hivyo sisi wakristo tunapoalikwa kuudhihirisha upendo huo tunapaswa kunuia kuistawisha huruma hiyo ya Mungu kwa wanadamu wote. Mtume Yohane ameendelea kuielezea jumuiya hii mpya kwa kulitilia mkazo suala la upya huo katika mwanadamu. “Tazama maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake ... naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita”. Kumwilika kwa Kristo ndiko kumelidhihirisha hili na limekamilishwa katika fumbo la Pasaka, yaani mateso kifo na ufufuko wake. Mwanadamu ambaye alikuwa amejeruhiwa na dhambi sasa amefanyika upya na amerejeshewa hadhi yake.

Jumuiya ya Wakristo inapoendelea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu inaalikwa kwa njia hii ya kupyaisha maisha yake. Jamii yetu inamshuhudia mwanadamu ambaye amejeruhiwa kwa dhiki nyingi; mwanadamu ambaye amekosa upendo wa dhati kutoka kwa mwenzake, mwanadamu ambaye amejaa visasi na vinyongo na mbaya zaidi kutokuwa na huruma na wenzake, mwanadamu ambaye amejijengea uzio katika maisha yake na hataki kabisa kujifunua na kuwa tayari kushirikiana, kupokea na kusaidia wengine. Hayo yote ni matokeo ya dhambi, matokeo ya kumweka mbali Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Upendo wenyewe. Katika hali mbaya zaidi mambo haya yanatiliwa mbolea na mwelekeo wa kijamii mambosasa ambayo imetawaliwa zaidi na usekulari na kupoteza hofu ya Mungu.

Jumuiya ya waamini inaalikwa leo hii kupenyeza katika jamii hii na “kujiweka nje ya umati”, yaani kutosawazishwa na mienendo ya dunia hii. Ni wazi kwamba raha na mielekeo ya kidunia inatupatia faraja lakini mara nyingi huisha kwa muda mfupi sana. Hii ni kwa sababu mwanadamu anataka kutengeneza huku akiwa amejitenga na Mungu. Hivyo tunapaswa kujiweka tayari kupitia katika upingamizi huo wa kidunia ambao kibinadamu hutupatia dhiki nyingi lakini katika ulimwengu wa kiroho unapaswa kuwa faraja kwetu na kutupatia nguvu ya kusonga mbele bila woga. Paulo na Barnaba katika somo la kwanza wanawaonya wakristo Listra na Ikonio na Antiokia wakiwaambia “wakae katika Imani, na kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi”. Uimara wetu katika imani utatuepusha na kubabaishwa na upepo wa kidua ambao unatuvuta kuitikia vionjo na matakwa ya kimwili na kutufanya tuweze kuitikia wito wa Mungu wa kudhihirisha upendo wake kwa watu wote na kwa njia hiyo kuifunua huruma yake.

Wanajumuiya wa jamii hii mpya wanajengwa na Upendo wa kimungu. Hawana chuki na hawajengi visasi kwa sababu daima wananuia mema kwa wale wanaowakosea na hivyo wanatafuta kuwaondoa katika hali zao kwa kuwaombea na kutafuta suluhu. Hawa ni wale ambao daima wanatafuta kujenga umoja kati yao kwa kushirikishana katika matukio mbalimbali kila mmoja kwa kadiri ya kipawa chake na kama tulivyotafakari Dominika ya Kristo mchungaji mwema wanajimithilisha na Kristo Mchungaji Mwema katika utendaji wao. Wanajumuiya hawa ni wapatanishi. Panapotokea kutokuelewana hawatafuti makundi bali wanatafuta mbinu ya kueleweshana kusudi wote wafikie kuwa kundi moja chini ya Mchungaji mmoja yaani Yesu Kristo. Wanaweza kutenda haya yote kwa sababu ni yale “aliyofanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani”.

Tunaalikwa leo hii kutafakari juu ya maisha yetu ya kikristo. Ni jinsi gani tumeweza kuyafanya upya na hivyo kupyaisha jumuiya ya mwanadamu. Tugutuke tusije tukajisawazisha na maisha ya kawaida ya kijamii. Maisha ya kikristo yanapaswa kuwa ya kuishangaza dunia na “kujiweka nje ya umati”. Maisha ya kikristo ni upya wa masiha na upya huo wa maisha unaifunua huruma ya Mungu na Upendo wake. Utambulisho wetu ni Upendo wa Kristo ambao hauna mipaka. Tuendelee kuwafunda na kuwarithisha watoto wetu utambulisho huu wa kiimani, ili kweli hata wao waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, Jumapili hii wanapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watoto, maadhimisho yanayoongozwa na kauli mbiu "Kukua katika huruma kama Baba wa mbinguni". Si watoto wote watakaobahatika kufika Roma kwa Jubilei hii, basi, Makanisa mahalia yawaandalie watoto hawa Jubilei yao, ili waweze kukua katika huruma na upendo wa Baba wa milele!

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.