2016-04-22 09:12:00

Papa: kukumbuka mambo mema ya Mungu katika maisha yetu


Wakristo wanatakiwa daima kuyakumbuka  mambo mema  aliyowatendea  Mungu katika  maisha yao,  kwa kuwa , kufanya hivyo , huonyesha uimara  katika kuifuata njia ya Imani.  Papa Francisko alieleza Alhamis asubuhi,  wakati wa Ibada ya Misa aliyoiongoza katika Kanisa dogo la Mtakatifu Vatican. Papa aliielezea Imani  kuwa ni  safari  tunayoifanya  katika maisha yetu ya kila siku kuelekea kwa Mungu. Hivyo ni jambo jema na lazima mara kwa mara  kuyakumbuka yote Mungu aliyotufanyika  katika hija hii, yaliyo mazuri.  na pia  majaribu na matatizo  kwa sababu,  Mungu kutembea na sisi,  hakuondoi udhaifu wetu wa kibinadamu.

 Papa katika homilía hii alifanya rejea kwa  Mtume Paulo,  wakati alipoingia katika Sinagogi la Antiokia na kuanza kutangaza habari njema ya Injili kwa kuwarejea kwa Wahenga wa Imani  tangu  Ibrahimu na Musa, Misri na Nchi ya Ahadi,  mpaka kuja kwa Yesu. Papa aliyaita kwamba yalikuwa ni mahubiri ya kihistoria, yaliyotoa msingi  muhimu wa imani kwa wafuasi wa Yesu ,  kwa sababu, Papa alisisitiza yanatukumbusha  sote  mambo muhimu, na ishara za uwepo wa Mungu katika maisha ya binadamu.  

Papa aliendelea kutaja  umuhimu kuyakumbuka ya nyuma, akirejea pia tukio la Alhamisi Kuu ambamo Yesu aliwaambia Mitume wake  wakati wa karamu yake ya  mwisho,  kunyweni damu yangu na Kuleni mwili wangu kwa ukumbusho wangu. Na hivyo kwa kumbukumbu hii tunakumbushwa jinsi Mungu alivyotuokoa. Hivyo tunapaswa kuifanya  kumbukumbu hii kwa moyo wa kina na uchaji , maana inatukumbusha  jinsi Mungu alivyo tukomboa kwa upendo wake Mkuu, hadi kumtoa mwanae Msalabani .  

Akasema, hivo ndiyo maana Kanisa linataka kila mara tushiriki katika  kumbukumbu hii  inayoadhimishwa katika  Sakramenti ya Ekaristi, kama vile, ilivyokuwa kwa Wana wa Israel, ilivyoelezwa katika Kitabu cha Bibilia cha Kumbukumbu ya Torati.   Sisi, pia, anasema Francis, ni lazima kufanya hivyo katika maisha yetu binafsi, kwa sababu kila mmoja wetu  ametengeneza njia yake katika kumufuata Mungu , kutembea karibu na  Mungu au katika kujiweka mbali na Bwana.

Papa alitaja umuhimu kufanya kumbukumbu hii katika ukweli  toka ndani ya moyo na kutoa asante kwa Yesu, ambaye kamwe haachi kutembea  pamoja nasi katika historia ya maisha yetu.  Na akaonya, lakini bahati mbaya mara kwa mara katika udhaifu wetu wa kibinadamu tunaufunga mlango wa kiroho, tunamfungia Yesu nje,  nje ya  maisha yetu , na kupoteza imani kwake na hivyo tunakanusha wokovu aliotuletea.  Lakini kwa kuyakumbuka ya nyuma , twaweza kujenga upya urafiki wetu na Yesu , na kuanza kutembea tena pamoja nae. Papa alieleza na kuhimiza  kila mmoja wetu, daima kufanya kumbukumbu kwa mema mengi aliyotudea Mungu , tukiyaunganisha na matatizo na majaribu pia kwa kuwa vyote ni sehemu ya njia ya hija inayoelekea kwa Mungu.  








All the contents on this site are copyrighted ©.