2016-04-22 10:50:00

Maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani ni moto wa kuotea mbali!


Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia nchini Poland inaongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Maadhimisho haya yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 26 – 31 Julai 2016 kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko. Hizi ni siku za sala, tafakari, katekesi, upendo na mshikamano miongoni mwa vijana wa kizazi kipya wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha na utume wao! Ni siku za Uinjilishaji miongoni mwa vijana!

Katika maadhimisho ya Siku ya XXX ya Vijana Duniani yaliyofanyika huko Rio de Janeiro, nchini Brazil, kunako mwaka 2013 vijana kutoka Nchi Takatifu walioshiriki walikuwa ni thelathini tu! Lakini kwa maadhimisho ya Mwaka 2016 wameamua kutoka kimasomaso kwani hadi sasa kuna vijana 700 ambao wamekwishajiandikisha kushiriki katika maadhimisho haya ambayo kwa mwaka huu yana mvuto wa pekee kwa vijana kwani yanakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Pili ni maadhimisho yanayofanyika nchini Poland alikozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa Siku za Vijana Kimataifa. Tatu, maadhimisho haya ni fursa kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko anayewachangamotisha vijana kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Poland ni mahali alipozaliwa pia Sr, Faustina Kowalska, mtume na shuhuda wa Ibada ya huruma ya Mungu inayowachangamotisha waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Sr. Faustina katika shajara yake anakaza kusema, Yesu anawadai waja wake matendo ya huruma yanayopata chimbuko kutoka kwake. Huu ni wajibu wa kuonesha huruma kwa jirani na wale wote wanaowazunguka hata imani kali ni bure kama haimwilishwi katika matendo ya huruma na mapendo!

Taarifa kutoka Nchi Takatifu inaonesha kwamba, vijana wote hawa 700 wataanzia safari yao kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Tel Aviv na kwamba, tayari vibali maalum vimekwisha kutolewa kwa ajili ya vijana kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Hii ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya kuonja na kushuhudia Ukatoliki wa Kanisa.

Hadi sasa kuna katekesi makini kuhusu utume kwa vijana mintarafu Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili inaendelea kutolewa, ili kuwaimarisha vijana katika maisha ya kiroho na kimwili, ili kumshuhudia Kristo Mfufuka katika maisha yao. Vijana hawa watakuwepo nchini Poland kwa majuma mawili ili kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya kimissionari ili kuwangazia vijana wenzao Injili ya furaha kwa kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.