2016-04-22 06:30:00

Huruma ya Mungu kwa watoto wadogo!


Kwa nini tunahitaji mafundisho haya kabla ya ubatizo wa watoto wachanga na wadogo? Wakatekumeni – watoto wa shule na watu wazima wanapata malezi na wanafuata kipindi maalum cha mafundisho kabla ya ubatizo wao Watoto wadogo wanawategemea wazazi na wazazi wa ubatizo katika malezi, chakula, nguo n.k.; vile vile malezi yao ya awali ya kikristo yatategemea wazazi na wazazi wa ubatizo.

Safari ya wokovu ya binadamu inaanza kwa Sakramenti tatu za mwanzo ambazo zinaitwa Sacraments of christian initiation au Sakramenti za jando la kikristo. Sakramenti hizi ni Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Isipokuwa jando yetu ni kumwandaa na kumhamisha binadamu kutoka katika ulimwengu wa dhambi na kumhamishia kwenye ulimwengu wa Mungu, ulimwengu mtakatifu. Jando yetu ni kumwingiza binadamu kwenye Fumbo la Mungu – Fumbo la wokovu na mpango wake ulioandaliwa na Mungu ili wote wamfahamu na wapate kuokoka bila kujali kabila la mtu, rangi yake, itikadi n.k.

Utaratibu wa kuingia kwenye fumbo hili linaanza na imani inayozaliwa kwa ajili ya mtu kuhubiriwa Neno la Mungu. Neno linaloamsha imani ya mtu linamwalika aongoke na kubadili mwenendo wa maisha na kuishi kulingana na mapenzi ya Mungu ambaye anataka kutushirikisha Uzima wake. Utaratibu huo unafanyika katika Kanisa na kwa njia ya jumuiya ya Kanisa, maana mtu anayemfuata Kristo anaunda Mwili wa Kanisa na ataishi maisha ya Kanisa na ibada zake. Tangu mwanzo wa Kanisa, Mababa wa Kanisa walifundisha kuwa ukatekumenati ni sawa na mimba ya mtu. Kuingia kwenye ukatekumenati ni sawa na mimba kutungwa. Kipindi cha ukatekumenati ni uwepo wa katoto tumboni mwa Mama-Kanisa; Ubatizo ndio kuzaliwa kwa mtoto.

Ningependa sasa nieleze utofauti uliopo kati ya uhai na uzima. Uhai ndio huu tunaopewa na wazazi wetu kwa ajili ya mpango na uwezo waliopewa na Mwenyezi Mungu. Huu ndio uhai wa viumbe vyote vya Mungu. Uzima ni maisha ya Mungu mwenyewe, ni Uhai wa Mungu mwenyewe. Mungu alipowaumba wazazi wetu wa kwanza, aliwaumba na kuwavuvia Roho wa uzima ndani mwao. Kwa hiyo wazazi wetu wa kwanza walikuwa na uhai wa viumbe vya Mungu lakini walitofautiana na viumbe vingine kwa sababu tangu mwanzo waliumbwa kwa namna ya ajabu zaidi kuliko viumbe vingine – walishirikishwa Uzima wa Mungu.

Dhambi ya asili ilisababisha kuwa walipoteza Uzima wa Mungu. Na kifo kikaingia katika maisha ya watu hao wa kwanza. Kifo hicho ni alama ya Huruma ya Mungu maana wangeendelea kuishi milele, basi, wangeishi milele katika laana. Kila mmoja wetu, ukimwacha Mama Bikira Maria aliyekingwa na dhmabi ya asili tangu mwanzo, anazaliwa akiwa na uhai tu. Uzima wa Mungu haumo ndani mwetu. Inabidi tuzaliwe mara ya pili, yaani, kwa njia ya Ubatizo tushirikishwe tena upya Uzima wa Mungu.

Hivyo, ndugu zangu, kuna utofauti mkubwa wa kimsingi kabisa kati yetu tuliobatizwa na wale ambao hawajabatizwa. Ufahari wetu na hadhi yetu ndiyo hii – sisi ni watoto wenye uhai na uzima wa Mungu; tunashiriki tayari kiroho ile hali tutakayoshiriki kikamilifu huko mbinguni nyumbani kwa Baba. Heri yangu ni kubwa mno kwani nimebatizwa!

Njia ya ukatekumene katika Kanisa:

Watu wazima wanafuata vipindi vifuatavyo katika safari ya wongofu:

Kipindi I – kipindi cha kumtafuta Kristo; kwa upande wa Kanisa ni kipindi cha kumhubiri Mungu Aliye Hai na Yesu Kristu aliyetumwa na Baba kutukomboa, ili watu wakisukumwa na kumtii Roho Mtakatifu, wamwamini Yesu na kwa hiari yao waongoke na kumfuata Mungu. Tunda la kipindi hiki ni imani hai na wongofu wa awali wa mkandidati, ambao unamfanya aamue kumfuata Yesu na kupokea Ubatizo. Kipindi hiki kinamfikisha mkandidati kwene hatua muhimu ya kupokelewa au kuandikishwa kwenye orodha ya waombaji au watakaji (ipo ibada yake maalum).

Kipindi II – ukatekumenati wenyewe; Mama-Kanisa anawalisha watakaji Neno la Mungu, maelezo yake, anawashirikisha habari zote muhimu za mafundisho sahihi ya Kanisa; watakaji wanashiriki katika ibada mbalimbali, hasa Misa Takatifu za Jumapili na sikukuu zilizoamriwa n.k. Wanashiriki kwa bidii katika maisha yote ya Kanisa hasa katika jumuiya ndogondogo ambazo zina nafasi kubwa sana na muhimu katika malezi ya wakatekumeni. Tunda la kipindi hiki cha pili ni wongofu kamili wa mtakaji, kugeuka kuwa mtu mpya anayeishi tayari maisha ya kikristo kikamilifu. Msaada mkubwa katika kipindi hiki ni ibada maalum zinazomsaidia mtakaji kutakaswa na kuimarishwa katika nia njema ya kumfuata Kristo. Mwishoni mwa kipindi hicho kunakuwepo na hatua ya pili muhimu katika safari ya wokovu ya mkatekumeni – uteuzi, yaani kuteuliwa kuwa mkatekumeni.

Kipindi III – kipindi cha kuimarisha na kukomaza maisha ya kiroho ya mkatekumeni, kumtakasa zaidi na zaidi kwa njia ya kutafuta dhambi za maisha yake au upekuzi wa dhamiri zake; kwa njia ya toba na malipizi na kwa njia ya kumtafuta zaidi na kufahamu zaidi Bwana Yesu. Wakatekumeni wanashiriki zaidi liturjia ya Kanisa na maisha ya jumuiya zao; Msaada mkubwa katika kipindi hiki ni ibada zinazoitwa takaso na mausia. Takaso zinatakasa viungo vya mwili wake – macho, masikio, ulimi n.k.; mausia ni ibada ambazo wakati wake Mama-Kanisa anawakabidhi rasmi wakatekumeni Kanuni ya Imani ya Kanisa na Sala ya Bwana, yaani wanapewa muhtasari wa imani yetu na sala ambayo inaunganisha sala zote za Kanisa na inawafanya wakatekumeni wamhafamu Mungu kama Baba yao anayewapenda upeo. Tunda la kipindi hiki ni Ubatizo, Komunyo ya Kwanza na Kipaimara – sakramenti za jando ya kikristu wanazopewa wakatekumeni. Pengine Kipaimara inaweza kuahirishwa hadi hapo watakapopata zaidi mafundisho au wakati ambapo Baba Askofu atakuwepo kwa ajili ya kuonyesha umuhimu wa sakramenti hii ya utu mzima katika Kanisa.

Kipindi IV – wakati baada ya Ubatizo katika kipindi cha Pasaka (kama walibatizwa Pasaka) au kwa muda kama huo wabatizwa wanaendelea kufundishwa zaidi mafumbo makuu ya imani na kuyaishi – hasa kwa njia ya kushiriki Ekaristi Takatifu, kusikiliza Neno la Mungu, kusali sana na kuingia zaidi kwenye maisha ya jumuiya ya waumini.

Ukatekumeni wa watoto wachanga haupo kabla ya Ubatizo wao. Nafasi yake inachukuliwa na malezi ya wazazi wao na mafundisho wanayoyapata kabla ya Ubatizo wa watoto wao. Watoto wanaingizwa moja kwa moja kwenye Ukristo – kama vile wanapewa dhamana. Dhamana hiyo ni Ukristo wa wazazi na walezi wao. Ndio maana katika Ubatizo wa watoto, Mama-Kanisa anataka kuondoka shaka lolote kuhusu msimamo wa wazazi na wazazi wa ubatizo. Watoto watakuwa na kipindi cha ukatekumenati wakati wanapofikia umri wa kuanza mafundisho ya Komunyo ya kwanza. Ndio maana hatuna budi kuhakikisha kuwa neema ya Ubatizo wa watoto waliobatizwa haifi katikati hapo kwa ajili ya malezi mabaya ya wazazi na wazazi wa Ubatizo.

Hapa tunafikia ukweli wa kwamba wazazi na wazazi wa ubatizo wana wajibu mkubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu kuhakikisha kuwa watoto wanapata malezi ya awali katika familia – shule ya sala za msingi, shule ya maadili, shule ya utu, shule ya ibada za Jumapili na katika jumuiya na familia. Wazazi na wazazi wa ubatizo ni makatekista wa kwanza watoto wanaokutana nao katika historia ya maisha yao na ukristu wao.

Tofauti na ukatekumenati wa watu wazima, ambao wanapimwa kabla ya Ubatizo na kupelelezwa kiasi cha kutosha wakati wote wa mafundisho yao, watoto wadogo tunapata uhakika fulani kuhusu jinsi watakavyoweza kuishi kikristu tukiwatazama wazazi na wazazi wa ubatizo. Kama imani yao ni hai, kama wanaishi maisha ya kikristu kikamilifu, wanashiriki meza ya Bwana, wanaishi safi katika ndoa takatifu n.k. – basi, tunaona haya kama dalili ya Ukristo hai ambaqo watoto wataukuta na kuufaidi katika utoto wao wanapojiandaa kusoma zaidi kabla ya Komunyo.

Tuthamini sana nafasi ya wazazi na wazazi wa Ubatizo; tuzingatie sana umuhimu na umakini katika namna ya kuwachagua wazazi wa Ubatizo; kuwathamini na kuwaheshimu na kuwatii katika maisha yote; Wazazi na wazazi wa ubatizo – jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa imani ya watoto wao inakuwa na inaonekana kimatendo; wajibu wa kuwasinidikiza na kuwalea; kuonya, kushauri, kukosoa na kusaidia panapotakiwa. Umuhimu wa kuwachagua wazazi wa Ubatizo wazuri, wanaowajibika kikristo; umuhimu wa kuwaheshimu na kuwatii; umuhimu wa wazazi kuwajibika sana!

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak.

Kituo cha Hija ya Huruma ya Mungu Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.