2016-04-21 12:31:00

Papa Francisko: Salam na matashi mema kwa Pasaka ya Wayahudi!


Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiyahudi, kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 30 Aprili, 2016 wanaadhimisha Pasaka ya Wayahudi, kwa kukumbuka jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo alivyowakomboa kutoka utumwani Misri kwa nguvu na uweza mkuu! Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe wa salam na matashi mema  Dr. Riccardo Segni, Rabi mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma, huku akikumbuka kwa namna ya pekee, tarehe 17 Januari 2015 alipotembelea Hekalu kuu la Wayahudi mjini Roma.

Baba Mtakatifu anawatakia Wayahudi wote heri na baraka kwa Siku kuu ya Pasaka, wanapokumbuka jinsi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani Misri na kuwaongoza kwenye Nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo anasema Baba Mtakatifu aendelee kuwaongoza hata wakati huu, awapatie baraka na kuwalinda katika huruma yake, huku akiwapatia amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaomba waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma, kumkumbuka katika sala na sadaka yao kwani hata yeye anapenda kuwahakikishia sala zake, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia nguvu ya kukua na kukomaa katika urafiki wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.