2016-04-21 08:02:00

Marehemu Askofu Isuja, Jembe la nguvu!


Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma, Tanzania, Jumatano tarehe 20 Aprili 2016 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Marehemu Askofu Mathias Isuja Josefu kwenye usingizi wa amani, baada ya kukamilisha safari ya maisha yake hapa duniani. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Dodoma.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza ndiye aliyetoa mahubiri katika Ibada hii ya Misa Takatifu kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha, wito na mateso ya Marehemu Askofu Isuja na kwamba, Kanisa linaamini maisha ya uzima wa milele. Katika Fumbo la mateso na kifo, ndani yake kuna maisha ya uzima wa milele. Yesu Kristo alionesha utii na unyenyekevu wa pekee uliojikita katika huduma kwa kuwaosha miguu mitume wake, akawaonesha umuhimu wa huduma ya upendo inayomwilishwa katika matendo.

Yesu, baada ya mateso na kifo, alifufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu na kumkirimia maisha mapya yanayojikita katika uzima wa milele. Kwa mwelekeo huu, Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima, kwa wale wote waliompokea siku ile walipobatizwa, wakajiongezea heshima na utukufu wake. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma imepokea taarifa ya kifo cha Askofu mstaafu Isuja kwa huzuni na simanzi, lakini, waamini wanapaswa kutambua kwamba kifo ni sehemu ya maisha na kwamba, kifo si mwisho bali ni daraja ya kuwapeleka waamini kwenye Ufalme wa Mungu.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma inapaswa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na mateso aliyomkirimia Askofu Mathias Isuja; ameishi zaidi ya miaka 86. Ameonesha fadhila ya imani kubwa katika maisha yake kama Mkristo, Padre na Askofu. Alitumia muda wake mwingi kwa ajili ya kuwategemeza na kuwawezesha wanadodoma, ili kuwajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Amekuwa Padre kwa miaka 56 na akalitumia Kanisa, Jamii na Taifa kwa ari na moyo mkuu. Aliugua na kuteseka sana, lakini maisha yake ya uzeeni, Kanisa linayatafakari kama zawadi na chombo cha utakaso.

Ibada ya Mkesha wa Mazishi ya Askofu Isuja:

Walimu, Wazazi wametakiwa kumuenzi Askofu Mng`atuka Mathias Isuja Joseph kwa vitendo na mfano kwa kujifunga kibwebwe katika utendaji kazi wao ili waweze kulitumikia kanisa katika maadili na weledi uliotukuka. Hayo yalibainishwa na Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Katika ibada ya Masifu ya Jioni ya kumwombea Marehemu Askofu Mng`atuka Mathias Issuja Josefu yaliyofanyikayofanyika wenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Jumanne tarehe 19 Aprili 2016.

Askofu Mkuu Kinyaiya alisema Marehemu Askofu Mng`atuka Isuja alilitumikia Kanisa kwa miaka 56 na alikuwa ni mtu wa kujitoa na kuwasaidia wengine hususani katika shughuli za elimu, afya, maji na huduma za kijamii. Akizungumzia suala la afya alisema kuwa Marehemu Askofu Isuja aliyahimiza mashirika ya kitawa na kazi za kitume yaliyofika Jimboni Dodoma kuanzisha vituo vya afya ili kuwahudumia watu mbalimbali ili waweze kuwaonjesha huruma na matumaini ya kulisikiliza Neno la Mungu na kwamba, hii ilikuwa ni sehemu ya utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili

"Ninawaombeni wahudumu wa afya mtoe huduma zenye tija kwa wagonjwa na kamwe ninawaombeni muache tabia ya kutoa lugha chafu kwa wagonjwa pindi wanapokuja kupata huduma za afya sehemu mahalia," aliongeza Askofu Mkuu Kinyaiya. Alisema kuwa kumekuwa na kasumba ya wahudumu wa afya katika vituo vya afya, zahanati na hata mahospitali kuwatukana wagonjwa hali amabyo inakuwa ni kinyume na maadi li ya kazi yao hivyo kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.

Kuhusu suala la elimu alisema kuwa Askofu Mng`atuka Isuja alipenda sana watu wawe na elimu iliyo bora hususani alipokuwa Mkurugenzi wa elimu Jimbo la Dodoma katika uhai wake. "Walimu ninawaombeni mfundishe vizuri ili tuweze kujenga taifa la watu wenye elimu iliyo bora na waadilifu kwa kumuenzi Marehemu Askofu Isuja" aliongeza Askofu mkuu Kinyaiya. Askofu mkuu Kinyaiya alisema kuwa watu mbalimbali wamekuwa wakisema kuwa shule za sekondari za Kanisa zimekuwa zikifanya vizuri ni nini wanachofanya wanakuwa na ufaulu mkubwa? Hapana shule hizo zinafanya vizuri kwa sababu walimu wana nidhamu, juhudi, bidii na maarifa katika ufundishaji wao.

Aidha Askofu Kinyaiya pia waliwataka wazazi na walezi kuwa na ari na moyo kuchangia suala la elimu kwani wazazi wa enzi hizi wamekuwa wakisema kuwa elimu ni bure hivyo wao hawana jukumu la kuchangia elimu, hivyo Askofu mkuu Kinyaiya aliwataka wazazi na walezi kuachana na mapokeo hasi katika suala la elimu bure kwani kwani sio kila kitu kinatolewa na serikali bali hata  wazazi na walezi wanapaswa kuwa wachangiaji katika maendeleo ya elimu ili kujenga taifa la watu wenye elimu bora na endelevu!

Wakati huo huo, Waziri mkuu Kassim M. Majaliwa akitoa salam za rambi rambi kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania alisema, kifo cha Askofu mstaafu Isuja ni pigo kubwa kwa familia ya Mungu nchini Tanzania, kwani aliwahudumia watu wote kiroho na kimwili. Serikali itaendelea kumuenzi Askofu Isuja kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa uhai wake na kuyaendeleza yale aliyoyafanya kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Askofu  Isuja alikuwa kiongozi makini katika huduma kiroho na kimwili na daima alilenga kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na waandishi maalum kutoka Dodoma, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.