2016-04-20 14:09:00

Watoto kuwasha moto wa Injili ya huruma ya Mungu!


Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki, zaidi ya watoto 60, 000 kwa mkupuo kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuanzia tarehe 23 – 25 Aprili 2016 watakuwa mjini Roma ili kuungana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yanaongozwa na  kauli mbiu “Kukua katika huruma kama baba wa mbinguni”. Kilele cha Jubilei ya watoto ni Jumapili, tarehe 24 Aprili 2016, majira ya saa 4:30 asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko atakapoongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jubilei ya watoto wa Kanisa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Waandaaji wa Jubilei ya watoto wanasema, hizi ni siku kuu tatu za sherehe, sala, tafakari, toba na ibada mbali mbali kama sehemu ya hija kuelekea katika Lango la Huruma, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika watoto kuchuchumilia toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha hata katika udogo wao. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Jumamosi tarehe 23 Aprili 2016, watoto wataianza siku kwa hija kuelekea kwenye Lango la Huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kuna Mapadre waungamishaji 150 watakaoshiriki kikamilifu katika kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto hawa. Watahitimisha hija hii kwa kukiri Kanuni ya Imani kuzunguka Kaburi la Mtakatifu Petro.

Baadaye, jioni wataelekea kwenye Uwanja wa michezo wa Olimpic, ulioko mjini Roma, ili kuendelea kuserebuka kwa muziki na shuhuda mbali mbali kutoka kwa watoto hawa ambao kweli ni jeuri ya Kanisa na tumaini la wengi! Hiki ni kipindi cha utume wa vijana kuonesha karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Mambo yote haya yatakuwa “Live kwenye TV 2000 na Radio INBLUE.

Jumapili tarehe 24 Aprili 2016 watoto watashiriki Ibada ya Misa takatifu itakaoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Watoto watapata fursa ya kutembelea mahema ya huruma ya Mungu yaliyoandaliwa kwenye Makanisa mbali mbali mjini Roma. Humo watashuhudia matendo ya huruma: kiroho na kimwili yanayotekelezwa na waamini mbali mbali, tayari kujifunza, ili kuamwilisha hata wao miongoni mwa watoto wenzao, kama kielelezo cha imani tendaji.

Watoto hawa watakirimiwa kwenye Jumuiya za Kikristo zipatazo 200, kielelezo cha ukarimu na upendo wa Familia ya Mungu. Jeshi la Polisi nalo liko bega kwa bega ili kuwasaidia watoto kuwa na matumizi bora na sahihi ya mitandao ya jamii, zoezi litakalofanywa kuzunguka Castel Sant’ Angelo, pembeni kidogo tu mwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.