2016-04-20 10:43:00

Wanawake wa Afrika watangazaji wa huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika, Africae Munus anawataka wanawake Barani Afrika kutambua dhamana na mchango wao katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na upatanisho. Ili kufikia lengo hili kuna haja kwa wanawake Barani Afrika kujengewa uwezo kwa njia ya elimu na katekesi makini na endelevu katika maisha yao. Kanisa lina dhamana ya kuchangia mchakato wa ukombozi wa wanawake Barani Afrika, ili kuweza kuchangia kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya: Familia, Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Wanawake wanapaswa kujiamini kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa,  kwani wao ni uti wa mgongo kwa Makanisa mahalia. Wanawake ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu, hawa ndio wanaotumwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa Familia ya Mungu Barani Afrika, kwa kuonesha utakatifu wa maisha, ujasiri, utu na heshima ya binadamu. Kanisa linawategemea wanawake kujenga na kudumisha ekolojia ya binadamu kwa njia ya upendo, upole, ukarimu, utulivu na moyo wa huruma, tunu ambazo, wanawake wanafahamu namna ya kuzirithisha kwa vijana wa kizazi kipya, kielelezo cha utajiri wa zawadi pekee ya umama!

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO;  kuanzia tarehe 29 Agosti hadi tarehe 5 Septemba 2016 litafanya mkutano wake mkuu Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi. Taarifa hii imethibitishwa na Mama Bernadette Chiwaya, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Malawi ambaye amefafanua kwamba, wajumbe kutoka katika nchi 22 za Kiafrika wanatarajiwa kuhudhuria.

Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “ Wanawake wa Afrika, Watangazaji wa Huruma ya Mungu”. Wanawake hawa wanasindikizwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu isemayo “ Njooni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda, Je, haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?” Yoh. 4: 29. Mkutano huu utafunguliwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Michezo wa Civo, Lilongwe, Malawi. Hii itakuwa ni fursa ya kumwangalia mwanamke wa Afrika kama wakala wa mabadiliko, maendeleo, majadiliano haki na amani; mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu Barani Afrika. Wanawake wa Afrika watapembua kwa kina na mapana matumaini ya utendaji katika huduma ya familia, vijana na mahangaiko ya watu wa Bara la Afrika.

Wataangalia kwa karibu sana dhana ya wanawake  na watoto wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu; Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Duniani katika mwanga wa Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko Furaha ya Injili, Evangelii gaudium. Ni mkutano utakaochambua dhana ya maji safi na salama; afya, haki msingi za binadamu; mabadiliko ya tabianchi; vijana na mchango wao katika mchakato wa Uinjilishaji; haki, amani na maendeleo endelevu! Mama Chiwaya anasema, hili litakuwa ni darasa endelevu, litakalowarejesha tena Wanawake Wakatoliki darasani kama sehemu ya mchakato wa majiundo endelevu, ili kushirikishana mawazo, uzoefu na mang’amuzi kutoka katika medani mbali mbali za maisha, tayari kusimama kidete kutangaza na kushuhudia ukuu na utakatifu; heshima na utu wa mwanamke Barani Afrika.

Mkutano huu utafungwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kituo cha Bingu cha Mikutano Kimataifa, BICC, huko Lilongwe, Jumapili tarehe 5 Septemba 2016. Shirikisho la Wanawake Wakatoliki Kimataifa lina wanachama wake Barani Afrika, Asia na Pacific, Ulaya Amerika ya Kaskazini na Amerika ya Kusini. Kwa mara ya mwisho mkutano mkuu wa Shirikisho hili ulifanyika mjini Fatima, Ureno kunako mwaka 2014. Mkutano huu kwa Kanda ya Afrika kwa mara ya mwisho ulifanyika kunako mwaka 2013, huko Abuja, nchini Nigeria. Jumla ya wajumbe 200 wanatajiwa kushiriki na wengine 250 watakuwa ni wajumbe kutoka ndani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.