2016-04-20 13:17:00

Usichelewe kukimbilia huruma ya Mungu!


Wapendwa Mahujaji, tumekusanyika katika chumba hiki cha ghorofani - katika Kituo hiki cha Hija cha Huruma ya Mungu - Kiabakari - kama wanafunzi wa Yesu walivyofanya baada ya Kupaa kwake Bwana wakiwa pamoja na Maria, Mama yake Yesu wakisali usiku na mchana wakingoja Ahadi ya Baba. Ahadi ya Baba, ndiye Roho wa Huruma yu pamoja nasi saa hii.

Ndugu waamini wenzangu, Tukiwa hivi kama Familia ya Watoto wa Mungu iliyokusanywa hapa na Roho wa Huruma, tunaweza kujitazama, kujitafiti na kujiuliza - ‘Ni nini hasa hitaji la Kanisa Takatifu kwa wakati huu wa Milenia ya Tatu na wa Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu?’

Baba Mtakatifu Paulo VI naye alijiuliza swali kama hili wakati wake na kujibu kama ifuatavyo: ‘Hatuna budi kusema - kwa hofu na kwa kutetemeka, maana hili ni Fumbo la Kanisa: hitaji kuu la Kanisa ni Roho Mtakatifu. Kanisa linahitaji daima Pentekoste ya kudumu, Pentekoste inayoendelea, Kanisa linahitaji moto uwakao moyoni mwake, linahitaji Neno lenye nguvu na Unabii katika mtazamo wake. Tunamhitaji Roho Mtakatifu. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulivyofikiriwa na Papa Yohane wa XXIII, ulikusudiwa uwe Pentekoste mpya ya Kanisa. Ingekuwa ni jambo baya na la kukatisha tamaa kama tungebaki nje ya Chumba kile cha Ghorofani.”

Lakini, tujiulize kinagaubaga - tunawezaje kupokea maneno haya ya Baba Mtakatifu na kuyafanyia kazi wakati kimsingi tunasita kukubali kuanza upya maisha yetu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu? Tunahoji kwa mashaka kama Nikodemo - mtu anawezaje kuzaliwa kwa mara ya pili? Tunahoji kwa wasiwasi nafasi na nguvu ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Maana wengi wetu - haijalishi ni Padre, Mtawa, Katekista ama Mwamini Mlei - tunaonekana kana kwamba tumejifungia ndani ya chumba chetu cha ghorofani ambamo Roho Mtakatifu hajaingia bado ama amekwishatoka tayari.

Chumba hicho ni ulimwengu wa hofu zako, mashaka, wasiwasi, upweke, mateso, kushindwa kwako kuishi Ukristo kwa ujasiri na kwa uaminifu hata katika mambo madogo, kukata tamaa kwako, utumwa wa dhambi zako - hasa zile dhambi kuu za maisha yako, yaani dhambi ulizozoea au unazitenda mara kwa mara, pamoja na mashaka juu ya hatima ya Kanisa na hatima ya ulimwengu unamoishi. Mlango wa chumba hicho umefungwa imara kwa hofu ya changamoto zilizoko nje huko. Kumbe, unamhitaji Yule atakayekuhurumia na kuja kwa nguvu kuubomoa mlango na kukuweka huru katika Kristo Mfufuka, Bwana wetu, Mfalme wa Huruma.

Chumba chako cha ghorofani - gereza la dhambi na la kukata tamaa - kinatakiwa kugeuka kuwa chumba cha matumaini, nuru, amani na uweza wa Mungu kama chumba cha ghorofani kile cha awali cha siku ya Pentekoste. Chumba kilichojaa uvumi wa upepo na ndimi za moto. Mlango wa chumba hicho uliokuwa umefungwa  imara hadi siku hiyo, sasa uko wazi, tena umeng’olewa kabisa na fremu yake forever! Na kwa taarifa yako, mwenzangu, hautarudishwa tena! Ndiye Roho Mtakatifu wa Huruma aliyesababisha kwamba tangu siku ya Pentekoste hakuna tena mahali, hakuna chumba kingine cha ghorofani ambamo Mkristo ataweza kujificha kwa hofu ya ulimwengu. Hakuna.                                            

Baba Mtakatifu Francisko katika homilia ya Misa ya Krisma Takatifu mwaka juzi alizungumza kwa msisitizo mkubwa kabisa hitaji la kuhuisha na kuuthamini inavyostahili mpako katika maisha yetu ya kikristo kama alama ya kimsingi ya karama za Roho Mtakatifu zinazotujia na kutufanya wapya katika Kristo. Alisema - ‘Mungu Baba atufanye wapya katika Roho wa Utakatifu kwa mpako wake tuliopewa’. Tena alisema - ‘Padre anapoadhimisha Misa Takatifu analitwaa Taifa la Mungu alilokabidhiwa, akiyabeba majina yao… Mafuta ya thamani yaliyopaka kichwa cha Haruni haikupaka nafsi yake tu, bali yalimiminika na kuyafikia maeneo yote ya kandokando kwa ajili ya maskini, wafungwa, wagonjwa, wapweke na wenye huzuni.

Padre mwema hutambulika kwa kiwango cha upako wa watu wa Taifa la Mungu alilokabidhiwa na analowahudumia… Watu hao waonekane wanapotoka kanisani baada ya Misa wakiwa na nyuso zenye furaha kama za watu waliopewa Habari Njema kabisa hivi punde… Padre ambaye anatafuta nafsi yake tu katika Upadre wake, hayuko tayari kujikana kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na kuwaendea watu wa Mungu, basi, huyo hutoa mpako kidogo sana, sisemi hatoi kabisa, maana waamini - tumshukuru Mungu - wanatupora mpako huo kwa nguvu hata kama sisi hatutoi. Na Padre wa namna hii badala ya kuwa mshenga kati ya Mungu na watu wake hugeuka kuwa mtu wa mshahara na kibarua tu’.

Nitawezaje basi kuhisi harufu tamu ya mpako wa Roho Mtakatifu Mfariji na mwenye Huruma na mmimino wake katika maisha yangu kama Mkristo? Nitawezaje kuwa mshirika hai na kamili wa Pentekoste mpya ya Kanisa, mjumbe hai wa mapinduzi mapya ya Roho Mtakatifu, endapo maisha yangu ya kikristo ni jitihada za daima za kutafuta chumba cha ghorofani nipate kujificha na imani yangu haba na kuzama tena katika bahari ya hofu zangu?

Nitawezaje kumbeba Roho wa Huruma, wa imani hai na uinjilishaji mpya, endapo nashindwa kujinasua na mzigo wa maisha yangu ya zamani, kumbukumbu za dhambi nilizotenda, maanguko yangu ambayo Mungu amekwishanisamehe zamani sana na kuyasahau kabisa lakini mimi namkumbushia daima na nayakalia mambo hayo ya zamani yaliyopita na kuchokoza majeraha ambayo yamekwishapona zamani; kwa kifupi - nafukua kama mchawi makaburi ya dhambi zangu za zamani zilizokwishaondolewa na kuzikwa na Mungu katika Bahari ya Huruma yake?

Ndugu zangu wapendwa,

katika Mwaka huu wa Maalum wa Jubilei ya Huruma ya Mungu tunahitaji kumkazia macho Yesu wa Huruma katika picha hii (onyesha) ya Huruma yake. Tutazame macho yake ya Huruma. Tutazame mkono wake wa kulia uliovyonyanyuliwa katika tendo la kutubariki na kutushirikisha amani yake. Tutazame miali ya Damu ya Maji inavyotoka katika Moyo wake wenye Huruma na kusambaa kote na kutupenyeza sisi sote.

Nikuambie habari njema? Ukitaka kukutana na Yesu huyo wa Huruma anayetuvuvia Roho wa Huruma, Roho wa Amani, Umoja, Ujasiri na Roho wa Msukumo wa kwenda nje kuhubiri Habari Njema kwa watu wote - kwa kweli huhitaji kwenda mbali. Inatosha umfikie Baba Askofu na Padre yeyote aliye jirani yako. Wao ndio kielelezo hai cha Yesu wa Huruma, ndani mwao na kupitia kwao Yesu wa Huruma anaendelea kumimina Huruma yake isiyo na mipaka katika Kanisa lake. Wao ndio ‘alter Christus’ - yaani Kristo mwingine anayetuambia - Amani iwe kwenu! Pokeeni Roho Mtakatifu!

Mtazame Padre wako kwa makini na kwa jicho la imani. Mtazame akiwa amevaa alba yake nyeupe vizuri, amejifungia kiunoni mshipi au cingulum na amevaa stola tayari kutoa huduma takatifu iliyosheni Huruma ya Mungu. Miisho miwili ya stola yake inafanana na miali ya Damu na Maji kutoka katika Moyo wenye Huruma wa Yesu. Ni alama za Sakramenti mbili za Huruma ya Mungu anazoweza kuadhimisha Padre peke yake - Upatanisho na Ekaristi Takatifu.

Padre wako akinyanyua mkono akubariki na kukupa amani, anayekubariki ni Yesu mwenyewe, anapokaa katika kiungamishio, ni Huruma ya Mungu inatenda kazi ndani mwako kupitia kwa huduma ya kipadre. Anapoadhimisha Misa Takatifu kama kuhani wa Agano Jipya, anafanya yale yale aliyoyafanya Yesu Alhamisi Kuu na Ijumaa Kuu Msalabani.

Wapendwa,

Kwa njia ya Ubatizo, ambayo kwa hulka yake ni Sakramenti ya Huruma ya Ajabu ya Baba, tunarudishiwa heshima ya kuwa watoto wapendwa wa Mungu Baba, tunashirikishwa Uzima wa Mungu mwenyewe, tunaunganishwa na Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, katika Kanisa lake ambalo ni Mwili wake wa fumbo na tunapakwa mpako wa Roho Mtakatifu anayetufanya kuwa hekalu lake takatifu. Tunashirikishwa utume wa Yesu mwenyewe alipokuwa hapa duniani – kuwa nabii wa Huruma, kuhani mwenye Huruma na mfalme wa Huruma – kama tunavyofundishwa katika sala ya Mpako wa Krisma baada ya Ubatizo wetu: Mungu Mwenyezi, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyewaokoa katika dhambi na kuwapa uzima mpya kwa maji na Roho Mtakatifu, Yeye mwenyewe anawapaka Krisma ya wokovu, ili mwunganike na taifa lake, mwendelee kuwa viungo vyake Kristo – kuhani, nabii na mfalme, hadi mpate uzima wa milele. Amina.

Unapotenda dhambi, hali inabadilika ghafula. Unapoteza Uzima wa milele. Unaamua kuondoka nyumbani kwa Baba wa Huruma. Badala ya kuwa mwana wa ahadi na kuishi kwa amani ya Roho Mtakatifu, unageuka kwa hiari yako kuwa mwana mpotevu na kulisha nguruwe - ni tendo la uasi, na kuabudu tamaa zako na dhambi. Game over! Ndoto ya kupata maisha mazuri yenye mafanikio, amani, furaha na upendo mbali na Baba inafikia ukomo wa kutisha.

Lakini kwa Mungu wa Huruma hakuna neno - game is over! Wakati wote tunapoondoka nyumbani kwake na kufuata tamaa zetu na mipango yetu binafsi ya maisha, Baba anaendelea kututazama kwa upendo na huruma akiheshimu uhuru wetu wa kuamua. Ni kwa ajili ya Roho wa Huruma yake anayefanya kazi katika dhamiri zetu, kila siku tunapata fursa ya kurudi kwa Baba wa Huruma katika Sakramenti ya Huruma yake. Baba wa Huruma anatamani tupatikane tena, tufufuke, tuanze tena kupumua kwa pumzi ya Roho Mtakatifu na kuanza upya yote ndani yake. Fursa ipo. Ni wewe tu.

Yesu Kristo Mfufuka na mwenye Huruma, Yesu - Uso wa Huruma wa Baba, Yesu aliyejaa Roho wa Huruma anakungoja katika Galilaya mpya - yaani katika kiungamishio. Huko ndiko utakapomkuta. Katika nafsi ya Padre muungamishaji. Usimwogope Padre huyo. Huenda Padre huyo anahitaji zaidi Huruma ya Mungu kuliko hata wewe unayeungama kwake.

Ndugu zangu,

Sijui kama mnaelewa kwamba cheo chetu rasmi - sisi Wachungaji wenu - katika Liturujia ya Kanisa ni - MDHAMBI. Padre anapojibidisha kuzihurumia na kuziokoa roho za watu wa Mungu anaelewa fika na kujitambua kwamba yeye mwenyewe anahitaji kuokolewa kwanza. Kardinali Josef Ratzinger (Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI) alisema siku moja - ‘Siku zote nilikuwa najiuliza kwa nini katika Sala ya Ekaristi ya Kwanza ambapo Mapadre wanajiombea wenyewe, wanajitambulisha kwa Mungu na kwa kusanyiko Takatifu kama wadhambi. Kwa kilatini tunatamka hapo na kujipiga kifuani kwa unyenyekevu na toba - Usque nobis peccatoribus - yaani ‘Nasi wadhambi tunaotumainia Huruma yako, utujalie ushirika na Mitume wako Watakatifu na Mashahidi wako na Watakatifu wako wote…’ Sisi - Maaskofu na Mapadre, tunakumbuka daima hadhi yetu hii mbele ya Mungu na mbele ya Taifa lake - sisi ni wadhambi. Tunaweza kurudia pamoja na Petro - ‘Ondoka kwangu, Bwana, maana mimi ni mwenye dhambi’. (Lk 5:8)

Ndugu Mahujaji,

mtutazame sisi Mapadre wenu. Tazameni wadhambi wenzenu. Ndivyo tulivyo. Sisi ni wadhambi. Na tunahitaji Huruma ya Mungu kama ninyi. Lakini Yesu wa Huruma anapotunyanyua, vilindi vya maji vinapoteza nguvu yao, nasi tunabebwa na Yesu juu ya mawimbi ya tamaa na dhambi zetu, kama Petro alivyobebwa na Yesu hadi hapo Petro alipoacha kumkazia macho Bwana wake na kuanza kutazama mawimbi, yaani madhaifu yake na dhambi zake na kuanza kuzama… Sisi Mapadre na Maaskofu tunakuwa salama tunapomkazia macho Yesu wa Huruma, na kwa unyenyekevu tunakubali Yeye atubebe juu ya mawimbi ya madhaifu yetu na kututumia kama Mitume wakuu wa Huruma yake kwa njia ya Huruma iliyojaa katika Upadre wetu.

Ndugu zangu,

Tunabeba hazina hii ya ajabu kabisa ya Huruma ya Mungu isiyo na mipaka kupitia kwa Upadre wetu katika vyombo vya udongo vya ubinadamu wetu. Tunahitaji msaada wa sala zenu na upendo wenu na ulinzi wenu. Tunahitaji huruma yenu na upendo. Mmwone Yesu wa Huruma katika Upadre wetu na mfuate kwa imani hai, amani, matumaini na upendo. Msiishi mbali nasi Mapadre wenu. Katika Mwaka wa Huruma ya Mungu mnatuhitaji zaidi sana. Kwa njia ya Upadre wetu hazina hii ya Huruma ya Mungu inawafikia kwa kishindo!

Msiogope kututafuta, msisite kufanya maamuzi ya dhati ya kuongoka, kubadilika, kwenda kuungama, kupokea Komunyo Takatifu katika hali ya neema ya utakaso, kwa imani hai, uchaji na upendo wa dhati kwa Yesu wa Huruma - na kupata thawabu kubwa kabisa ya Mwaka huu wa Jubilei ya Huruma, yaani rehema kamili! Katika rehema kamili Baba wa Huruma anakuambia - mwanangu, ninachukua kitabu cha maisha yako na ninafuta kumbukumbu zote na adhabu zako zote na historia nzima ya maisha yako ya dhambi. Ninakupa sasa daftari jipya uanze kuandika upya historia ya maisha yako. Kazi ni kwako!

Kabla Lango la Huruma la Jubilei halijafungwa tarehe 13 Novemba mwaka huu na fursa ya kuanza upya maisha yako baada ya kupokea rehema kamili kutokuwepo tena kwa njia rahisi hii hadi hapo Lango la Jubilei litakapofunguliwa tena mwaka wa Jubilei ya kawaida - 2025 - nakusihi, fanya juu chini kuondoa vikwazo, kuvua utu wa kale, kutubu na kukamilisha safari yako ya wongofu ili uzamishwe katika Bahari ya Mungu kwa njia ya Sakramenti za Huruma - Upatanisho na Ekaristi Takatifu, upate kuvuka Lango la Huruma kwa moyo safi katika hali ya neema ya utakaso na kupata rehema kamili. Baba yuko tayari kukupa second chance in your life. Take it. NOW.

Kumbuka, mikononi mwako imo sekunde moja tu ambayo inaitwa - SASA. Sekunde zilizopita si mali yako tena na hazijirudii tena. Sekunde ambazo hazijaja, zimo bado mikononi mwa Mungu. Maisha yako yanakujia kwa mgawo wa sekunde moja moja. Itumie ipasavyo. Usiahirishe basi wongofu wako. Wewe si Bwana wa nyakati. Mungu ndiye Bwana wa nyakati. Wakati wako unaweza kuisha kabla hujaamua.

And then it will be game over for sure.

Kama unasita kwenda kuungama kwa ajili ya wingi wa dhambi zako na hujui hata pa kuanzia, kumbuka maneno ya Mt. Isaya wa Syria - ‘Kiganja cha mchanga kinachotupwa baharini - ndizo dhambi zote za ulimwengu mbele ya Huruma ya Mungu isiyo na mipaka’. Usiogope basi! Mungu Baba wa Huruma amekwishasimama kwenye kizingiti cha Lango la Huruma la nyumba yake na kuangaza macho akitamani kukuona. Usimfanye akusubiri sana. “Do not make Him wait”. Nenda kwa Padre wako kuanza upya kwa rehema kamili ya Baba wa Huruma, kwa neema na baraka ya Kristo, Mfalme wa Huruma na kwa nguvu na msaada na mwanga wa Roho wa Huruma! 

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak.

Kituo cha Hija ya Huruma ya Mungu, Kiabakari, 

Jimbo Katoliki la Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.