2016-04-20 09:29:00

Ondoeni woga usiokuwa na mashiko!


Kardinali Antonio Louis Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema, ziara ya viongozi wa Makanisa huko Lesvos, Ugiriki ni kielelezo cha upendo na mshikamano kwa watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na hali ngumu ya maisha. Anasema, kuna wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wanaoteseka pia katika kambi ya Idomen iliyoko mpakani mwa Macedonia na Ugiriki.

Ni ushuhuda wa matumaini, furaha na huduma ya upendo. Hawa ni watu wasiotaka makuu, bali kuonjeshwa cheche za: imani, matumaini na mapendo; usalama na faraja; mambo yanayomwilishwa kwa namna ya pekee katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ndio ushuhuda wa imani tendaji; kwani huruma na upendo ni chanda na pete katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha ushuhuda huu kwa kuwachukua wakimbizi na wahamiaji 12 watakaohudumiwa na Vatican! Hii ni idadi ndogo sana ikilinganishwa na mamillioni ya wakimbizi na wahamiaji, lakini ikiwa kama kila mtu atatekeleza tendo la huruma hapana shaka kwamba, wahamiaji na wakimbizi wengi wataweza kusaidiwa kwa hali na mali!

Matendo haya yanapata chimbuko lake katika maisha na utume wa Kanisa, katika undani wa maisha na utume wa Papa Francisko ambaye maskini na wanyonge wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani hawa ndio walengwa wa Habari Njema ya Injili na kwa namna ya pekee, Kanisa linapotangaza na kushuhudia Mwaka wa Bwana Uliokubaliwa! Baba Mtakatifu anaendelea kufunda na kuamsha dhamiri za Jumuiya ya Kimataifa kuona, kushuhudia na kutenda ili kuwasaidia watu wanaoteseka, bila ya kuwa na hofu wa woga, bila ya kuwatenga watu kwa kujenga kuta zinazozungushiwa nyaya za umeme.

Wakimbizi na wahamiaji hawa ni watu wanaotoka kwenye dhiki kubwa na mateso makali, wanahitaji kuonjeshwa huruma na mapendo. Waswahili husuma, mwenzako akinyolewa, nawe anza kutia maji! Kardinali Tagle anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kubomoa kuta za utengano, woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.