2016-04-20 08:56:00

Miaka 1050 ya Ukristo Poland!


Familia ya Mungu nchini Poland inaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani; huruma na mapendo kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani huko Poland, atajiunga na waamini nchini Poland kuendelea kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani, kwa wema na ukarimu wake na kwamba, matunda ya miaka 1050 ya Ukristo nchini humo yanaonekana!

Miaka hii yote imekuwa ni fursa kwa Familia ya Mungu nchini Poland kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, kwa kuambata Mafundisho tanzu ya Kanisa na Neno la Mungu, mambo ambayo yamesaidia kujenga utamaduni wa Familia ya Mungu nchini Poland, ushuhuda unaojionesha katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Kanisa nchini Poland anasema Baba Mtakatifu Francisko limeonesha mshikamano wa upendo na wananchi wa Poland katika hija ya maisha yao kwa kufurahi pamoja nao wakati wa furaha; kwa kulia nao wakati wa shida na majonzi, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake!

Katika kipindi chote hiki, waamini wamejenga na kukuza matumaini kwa Mwenyezi Mungu, wamekuza Ibada kwa Bikira Maria wa Czestochowa; wameimarisha imani na sasa wako tayari kusonga mbele kwa ujasiri mkubwa zaidi, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji. Waamini wanaalika kujenga na kuimarisha mahusiano yao na Kristo Yesu, tayari kuwashirikisha jirani zao ile furaha ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Haya ni kati ya mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Uwanja wa Manispaa ya Pozan, Poland kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Kardinali Parolin, katika maadhimisho haya alikuwa anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko anayekazia umoja wa shughuli za kimissionari kwa kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini wajitokeze kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wa mataifa kwa njia ya uhalisia wa maisha yao. Imani thabiti kwa Kristo na Kanisa lake, iwe ni chachu ya Uinjilishaji wa kina unaojikita katika ushuhuda wa maisha! Miaka 1050 isaidie kuimarisha mchakato wa waamini kuwa wafuasi na wamissionari wanaotumwa kushuhudia  uzuri wa imani yao pasi na hofu ya madhulumu na nyanyaso, kwani wao ni sehemu ya fungu na kondoo wa Kristo.

Watu wajifunze kuwa na kiasi na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu. Wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kutafakari Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha ushuhuda wa Kristo Mfufuka. Mwishoni, Kardinali Parolin, amemshukuru Mungu kwa zawadi ya imani, amani na utulivu. Kwa matunda mengi ya ushuhuda wa imani unaopambwa na watakatifu pamoja na wafiadini kutoka Poland katika ujumla wao, lakini kwa namna ya pekee Sr. Faustina Kowalska na Yohane Paulo II mashuhuda wa huruma ya Mungu na wainjilishaji wenye ujasiri; waliothubutu kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Maadhimisho ya Miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto kwa familia ya Mungu nchini Poland kutumia vyema neema na baraka walizopokea kutoka kwa Mungu, kama kielelezo cha huruma na upendo wake. Imani inaimarika kwa kuwashirikisha wengine; kwa kujenga na kuimarisha mshikamano na maskini, wakimbizi na wahamiaji kwa kuendelea kumuiga Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, chemchemi ya mapendo, huruma, furaha na ukweli!

Bikira Maria wa Jasna Gora asimamie na kuilinda Poland; watakatifu kutoka Poland waisaidie familia ya Mungu kugundua kwa mara nyingine tena uzuri wa Sakramenti ya Ubatizo na kuifanya iweze kuzaa matunda katika maisha ya kila mwamini. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kugundua tena na tena mizizi ya imani, kwa kuwashirikisha jirani zao, ili kweli familia ya Mungu nchini Poland iendelee kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu na Kristo Mfufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.