2016-04-20 12:01:00

Dhana ya Sinodi na Urika wa Maaskofu


Baraza la Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu, limehitimisha kikao chake cha kumi na nne, kilichosimamiwa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 18- 19 Aprili 2016. Wajumbe wamemshukuru Baba Mtakatifu kwa Wosia wake wa kitume Furaha ya upendo ndani ya familia,  “Amoris laetitia”, Wosia ambao umepokelewa kwa mikono miwili na Makanisa mahalia kama kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya familia.

Wajumbe wa Baraza wameangalia tema itakayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi wakati ujao kutoka kwa viongozi wakuu wa Kanisa, Mabaraza ya Kipapa na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Baadhi ya tema hizi zimewasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa tafakari zaidi na hatimaye, kutolewa maamuzi. Mwishoni, wajumbe wamepembua kwa kina na mapana kuhusu Mwongozo wa Sinodi za Maaskofu, “Ordo Synodi Episcoporum” uliochambuliwa na Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu mintarafu hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 17 Oktoba 2015.

Wajumbe wamejadili tema hii wakiwa wamegawanyika katika makundi madogo madogo ya kufanyia kazi, maarufu kama “Circuli minores” na baadaye, kuwasilisha muhtasari wa mawazo makuu yaliyojitokeza. Hapa mkazo kwa wakati huu ni kuendeleza dhana ya Sinodi na Urika wa Maaskofu huku wakiwa wameshikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kuweza kupata matunda mengi zaidi katika maisha na utume wa Kanisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wajumbe kwa moyo wa umoja na udugu waliouonesha wakati wa mkutano wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.