2016-04-19 14:52:00

Wosia wa Marehemu Askofu Isuja!


Askofu Mathias Isuja Josefu aliyefariki dunia hivi karibuni, anazikwa tarehe 20 Aprili 2016 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma, chini ya sanamu ya Mtakatifu Yosefu msimamizi wa Kanisa. Katika maisha na utume wake, Askofu Isuja aliwahi kuwaambia Watawa wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania kutunza urithi wa imani na maendeleo walioachiwa na Wamissionari wenzao, matunda ya bidi, juhudi, maarifa na sadaka. Aliwataka kuendeleza kazi, utume na tasaufi yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Hayati Askofu Isuja, aliwataka wana Kanisa kudumisha umoja na mshikamano katika imani, matumaini, mapendo na ufuasi wao kwa Kristo pasi na kupinda pinda! Waendelee kufanya kazi kwa juhudi, hekima, busara na maarifa, huku wakiiga na kufuata mifano bora ya wamissionari waliowatangalia; wengi wao walikuwa ni mapadre na wamissionari wachapa kazi na matunda ya kazi zao yanaonekana hadi leo hii katika medani mbali mbali za maendeleo ya mwanadamu ndani na nje ya Tanzania. Wamissionari waendeleze mchakato wa utamadunisho wa karama na tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu. Pale panapohitajika maboresho, yafanyike kwa kuzingatia utaratibu, kanuni na sheria za Shirika na Kanisa katika ujumla wake, katika uungwana na udugu. Askofu Isuja aliwataka watawa kuweka kando mambo yote yanayosababisha kinzani, mipasuko na migawanyiko katika maisha na utume wao. Daima wajenge utamaduni wa majadiliano ili kuendeleza maisha na utume wa Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, ili kupata mwelekeo na mipango mipya zaidi ya maisha!

Familia ya Mungu kutoka Tanzania inaoishi mjini Roma, Jumatatu, tarehe 18 Aprili 2016 ilikusanyika kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Laterano, kilichoko mjini Roma kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Askofu Mathias Isuja Josefu. Ibada hii ya Misa Takatifu imeongozwa na Padre Felix Mushobozi na kukazia umuhimu wa watanzania kudumisha mshikamano na uzalendo wakati wa raha na magumu. Marehemu Askofu Isuja atakumbukwa na wengi kutokana na moyo wake wa kibaba, tasaufi yake ya ndani, maisha ya kichungaji na busara ya kibinadamu.

Kwa niaba ya Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma, Padre Deodatus Masasi ansema, wamepokea msiba wa Askofu Isuja kwa moyo wa masikitiko na majonzi, lakini pia kwa moyo wa shukrani. Atambukwa moyo wake wa upendo, ukarimu, ucheshi na utumishi, uliomfanya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma: kiroho, kiutu, kilasilimali na matunda ya sera na mikakati yake ya kichungaji yanaonekana. Wanaombea umoja, upendo na mshikamano wa dhati wakati huu wa maombolezo wa msiba huu mzito!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.