2016-04-19 11:42:00

Kipaumbele: Haki, amani, usalama na upatanisho wa kitaifa!


Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati imekuwa na umuhimu wa pekee katika maisha ya watu, kwani ameonesha ari na ujasiri wa imani katika kukabiliana na changamoto za maisha badala ya malumbano, kinzani na vita. Uwepo na ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko mjini Bangui, umeacha chapa ya kudumu katika akili na mioyo ya watu! Ni kiongozi aliyezunguza wazi na katika ukweli kuhusu umuhimu wa kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki, amani, maridhiano, msamaha, upatanisho na umoja wa kitaifa, changamoto kubwa zinazofanyiwa kazi kwa sasa na wananchi wa Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati.

Tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoondoka, wananchi wa Afrika ya Kati, wameweza kufanya uchaguzi mkuu katika uhuru, amani na utulivu. Uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, lilikuwa ni tukio la kihistoria kwa Kanisa Barani Afrika. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutembelea na kusali na waamini wa dini ya Kiislam, ameonesha na kushuhudia umuhimu wa mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya waamini katika mchakato wa kukuza na kudumisha amani, upendo, mshikamano na mafao ya wengi na kwamba, tofauti za kidini ni utajiri unaopaswa kuendelezwa na kamwe kisiwe ni chanzo cha kinzani, misigano na mipasuko ya kijamii!

Haya kwa ufupi ni yale ambayo yamezungumzwa na Professa Faustin Archange Touadèra, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati wakati wa mahojiano maalum na Radio Vatican, tarehe 18 Aprili 2016, baada ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Professa Faustin anasema, nia ya ziara yake mjini Vatican ni kuja kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda na ujasiri wake wa imani na matumaini; kwa maneno yake ya amani, umoja, huruma, msamaha na upatanisho na kwamba, alionesha upendeleo wa pekee kwa Familia ya Mungu nchini Afrika ya kati, uwepo wao mjini Vatican ni kielelezo cha moyo wa shukrani!

Professa Faustin anasema, Serikali yake kwa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wengi, inataka kuanzisha mchakato wa ushirikiano na Vatican. Kama Rais, anasema, changamoto na vipaumbele vyake kwa sasa ni: amani na upatanisho wa kitaifa; umoja na mshikamano wa kitaifa; usalama kwa kukusanya silaha na kuwaingiza wanajeshi wa zamani katika mfumo wa ulinzi na usalama kitaifa.

Serikali inapania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kisiasa na kidini, ili kweli amani na utulivu viweze kukita mizizi yake katika akili na nyoyo za watu, ili kweli haki, amani na maridhiano viweze kutawala. Umoja wa Afrika unaendelea kuimarisha mchakato wa ulinzi na usalama, ili kupambana na kinzani na migogoro inayosababisha mipasuko ya kijamii na vita. Wananchi wamechoshwa na vita wanataka kuona haki, amani, msamaha, upatanisho na umoja wa kitaifa ukishika mkondo wake. Changamoto hii inakwenda sanjari na mapambano dhidi rushwa na ufisadi; ukabila na udini; mambo ambayo hayana mshiko wa mvuto kwa ustawi na maendeleo ya watu! Amani, usalama na upatanisho ndiyo ujumbe ambao Professa Faustin anasema, anataka kuufanyia kazi mara moja na kwamba, anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa ujenzi mpya wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.