2016-04-19 07:30:00

Afrika ya Kati wanataka kuandika ukurasa mpya wa amani na umoja wa kitaifa!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tatehe 18 Aprili 2016 amekutana na kuzungumza na Professa Faustin Archange Touadèra, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ambaye baadaye pia amekutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekua ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher. Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu na Professa Faustin wamezungumzia kwa ufupi hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Bangui, Mwezi Novemba 2016; mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo na maendeleo makubwa ya majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali. Haya ni matunda makubwa ya ujasiri wa imani ulioneshwa na kushuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake Afrika ya Kati. Kwa sasa wananchi wanaendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa.

Viongozi hawa wawili wamezungumzia kuhusu madhara ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inavyoendelea kuwaathiri wananchi wengi Afrika ya Kati na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaendelea kutoa msaada wa hali na mali katika mchakato wa maendeleo endelevu nchini humo. Kwa pamoja wameridhishwa na uhusiano mwema kati ya Vatican na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na kwamba, wataendelea kushirikiana kadiri ya sheria za kimataifa.

Baba Mtakatifu na mgeni wake wamepongeza na kushukuru mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afrika ya Kati katika sekta ya elimu, afya sanjari na mchakato wa haki, amani, upatanisho na maridhiano, ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.