2016-04-18 12:00:00

Wasichana waliotekwa nyara Nigeria bado wanakumbukwa!


Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anasema, familia ya Mungu nchini Nigeria inaendelea kuwakumbuka na kuwaombea wasichana 276 wa Shule ya Chibok waliotekwa nyara miaka miwili iliyopita na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram. Baadhi yao inasemekana bado wako hai na wametambuliwa na wazazi wao katika video iliyooneshwa hivi karibuni na hivyo kuchipua matumaini ya kuwaona tena wakiwa hai kati ya jamaa na ndugu zao!

Kardinali Onaiyekan anasema kwamba, anasikitishwa na kuhuzunishwa na kitendo cha wasichana hawa kuendelea kunyanyaswa mikononi mwa kikundi cha Boko Haram licha ya jitihada zote zilizofanywa  kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha kwamba wasichana hawa wanaachiliwa huru. Wasichana wa Chibok ni kielelezo kimojawapo cha watu waliotekwa huko Nigeria na hadi sasa hawajulikani mahali walipo. Kuna dalili za mafanikio kwa Serikali katika mapambano dhidi y avitendo vya kigaidi, lakini bado kuna watu wanateseka na kunyanyasika hata ndani ya nchi yao wenyewe kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Onaiyekan anasema, Serikali ya Nigeria haijatoa tamko rasmi kuhusu video inayosemekana kuwa na picha za baadhi ya wasichana waliotekwa nyara na Boko Haram miaka miwili iliyopita! Wananchi wamechoka kusikia maneno na uvumi, wanataka kuwaona watoto wao wakirejea kwenye familia zao. Juhudi za kuwaachia huru wasichana hawa na watu wote waliotekwa nyara nchini Nigeria hauna budi kuwa na mwelekeo mpana zaidi. Waamini waendelee kusali na Serikali iendelee kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kulinda raia na mali zao, Jambo la msingi ni kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; ili kweli wasichana hawa waweze hatimaye kuachiliwa huru. Wananchi wengi wanaanza kuonesha imani na matumaini kwa Serikali anasema Kardinali Onaiyekan, tayari kuanza maisha mapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.