2016-04-18 07:57:00

Nendeni mkajifunze mahangaiko ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea kutoka katika hija yake ya kitume kisiwani Lesvos, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 amepata nafasi ya kuchonga na waandishi wa ahabari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kujibu maswali na kutoa ufafanuzi wa kina. Baba Mtakatifu anasema, hija hii ya kitume imekuwa ni ya pekee kabisa katika maisha na utume wake, kwani ilikuwa inagusa utu na heshima ya binadamu na wala si masuala ya kisiasa!

Baba Mtakatifu amesema kwamba, amekutana na kuzungumza na Seneta Bernie Sanders kutoka Marekani ambaye alikuwa anashiriki kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapicha waraka wake wa kitume “Centesimus Annus” yaani “Miaka 100” tangu Waraka wa “Rerum Novarum” kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa ulipochapishwa.

Wamesalimiana kiungwana na wala hakukuwa na mkorogo wa masuala ya kisiasa kama ilivyochambuliwa na vyombo vya habari kuonesha kwamba, kulikuwa na mpasuko kati ya Baba Mtakatifu na Bwana Sanders ambaye anawania Urais nchini Marekani. Baba Mtakatifu anakaza kusema hiki ni kielelezo cha ustaarabu na uungwana. Kama waandishi wa habari walikuwa wanatarajia msukosuko wa kisiasa, wanalo jambo moyoni wakatafute tiba ya akili!

Akizungumzia kuhusu wahamiaji na wakimbizi kumi na wawili ambao Vatican imewapatia hifadhi na ukarimu anasema hakuna upendeleo wowote uliofanywa katika kuwachagua watu hawa ambao wote ni waamini wa dini ya Kiislam, bali hawa walikuwa tayari na nyaraka ambazo ziliwawezesha kupata upendeleo huu. Kulikuwepo na familia mbili za Kikristo, lakini hazikuwa na nyaraka zilizokuwa zimekamilika, kumbe, zikaachwa pembeni. Upendeleo wa pekee uliooneshwa na Vatican hapa ni kwamba, hawa wote ni watoto wa Mungu! Watahudumiwa na Vatican kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma. Itakumbukwa kwamba, tayari kuna familia kadhaa ambazo zimepewa hifadhi kwenye Parokia za Vatican.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuhusu wahamiaji na wakimbizi, kuna haja ya kujikita katika mchakato wa kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji hawa katika maisha, pengine huu ni msamihati ambao kwa watu wa nyakati na tamaduni mamboleo unaonekana kusahaulika au kupoteza maana yake. Leo hii kuna kambi za watu maalum, lakini ikumbukwe kwamba, baadhi ya watu wanaofanya mashambulizi ya kigaidi ni watoto, ndugu na jamaa ya watu kutoka Ulaya! Haya ni matokeo ya kukosekana kwa sera na mchakato wa kuwashirikisha watu hawa katika maisha na vipaumbele vya jamii. Hii ndiyo changamoto ambayo inapasw akufanyiwa kazi na Jumuiya yaUlaya ili kukuza dhana ya mshikamano na ushirikishwaji makini. Jamii inahitaji elimu ya ushirikishwaji wa kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu kuhusu mchakato wa ujenzi wa kuta zinazowatenganisha watu anakiri kwamba, kuna watu wenye hofu na wasi wasi, lakini kuna haja ya kuwajibika kwa kuonesha ukarimu, upendo na mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha. Ujenzi wa kuta za utengano si suluhisho makini, mchakato wa ujenzi wa madaraja ni jambo la msingi na ambalo linapaswa kuendelezwa kwa akili, majadiliano na ushirikishwaji wa watu. Kufunga mipaka kwa kujenga kuta za utengano si suluhu ya kweli ya matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumuiya ya Ulaya haina budi kuibua mbinu mkakati na sera makini zitakazosaidia kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi; kutengeneza fursa za ajira hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; ukarimu na ushirikishwaji; mambo msingi yanayoweza kudumisha amani, utulivu na maridhiano kati ya watu. Hali tete ya maisha walioiona na kuishuhudia kwenye kambi ya wakimbizi Kisiwani Lesvos, inatisha na kukatisha tamaa, kiasi hata cha mtu kutoa machozi ya uchungu!

Baba Mtakatifu amewaonesha waandishi wa habari michoro kadhaa aliyopewa na watoto kutoka Kisiwani Lesvos, Ugiriki. Watoto hawa wanatamani amani kwani wanateseka sana; wanatamani usalama, kwani wengi wao wanakufa maji; wengi wao wameshuhudia matukio haya mazito yakitendeka mbele ya macho yao, itakuwa ni vigumu sana kuweza kufuta picha za mateso na mahangaiko ya watoto hawa, picha ambazo zimeacha chapa ya kudumu katika maisha yao! Hapa kuna haja kwa watu kutokwa na machozi, wanaposhuhudia mateso na mahangaiko ya watoto wasiokuwa na hatia!

Baba Mtakatifu anasema, wakimbizi na wahamiaji wengi ni wale wanaokimbia vita, njaa, umaskini, nyanyaso, dhuluma na maafa asilia. Ni kweli kabisa kwamba, Jumuiya ya Ulaya haiwezi kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi wote hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Nyuma ya wakimbizi na wahamiaji hawa kuna biashara haramu ya silaha, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo! Baba Mtakatifu anauliza, Je, ni nani anayewapatia watu hawa silaha kiasi cha kufanya unyama huu dhidi ya ubinadamu?

Baba Mtakatifu anasema, umuhimu wa hija hii ya kitume, unajikita katika ushuhuda wa maisha na utume wa Mama Theresa wa Calcutta ambaye alishutumiwa kwamba, alikuwa anawasaidia watu kufa kifo chema! Lakini hata katika matukio kama haya, bado yanaweza kuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha ya watu. Wakimbizi na wahamiaji hawahitaji mambo makubwa, bali yale ya kawaida yanayofanywa kwa moyo wa upendo na majitoleo.

Jumuiya ya Kimataifa inaweza kulipatia baa la njaa kisogo, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa, dhamiri nyofu na mshikamano makini unaojikita katika kanuni ya auni. Kuna watu wanakula, wanashiba na kusaza na hapo hapo kuna mamillioni ya watu wanakufa kwa baa la njaa duniani. Hiki ni kielelezo cha utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kuna maelfu ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Amerika ya Kusini, hawa ni watu wanaokimbia baa la njaa, umaskini na hali ngumu ya maisha. Hii ni changamoto ya kimataifa ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anasema, amewaomba Maaskofu nchini Mexico kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu akijibu maswali kadhaa kuhusu Wosia wa Kitume: Furaha ya Upendo ndani ya familia, “Amoris laetitia” amewakumbusha waandishi wa habari kwamba, ni vyema ikiwa kama watafanya rejea kwa ufafanuzi wa kina uliotolewa na Kardinali Christoph Schonborn wakati wa uzinduzi wa Wosia huu wa kitume, kwani majibu ambayo angewapatia kwa wakati huo, yasingaliweza kufua dafu! Kardinali Schonborn ni mwataalimungu mahiri na katika tafakari yake ametoa majibu ya kina.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vyombo vya mawasiliano ya kijamii vimetoa kipaumbele cha kwanza kwa wanandoa waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena, jambo la kusikitisha sana, kwani, hili si tatizo msingi katika maisha na utume wa ndoa na familia, bali familia nzima inakabiliwa na kinzani pamoja na mmong’onyoko unaotishia utume na maisha yake ndani ya jamii na Kanisa katika ujumla wake. Bado watu hawajatambua kwamba, vijana wa kizazi kipya hawataki kuoa au kuolewa; watu hawajatambua kwamba, idadi ya watoto wanaozaliwa imepungua kwa kiasi kikubwa Barani Ulaya.

Baba Mtakatifu anasema vijana wengi hawana fursa za kazi na hata wakati mwingine kipato wanachopata hakitoshelezi mahitaji msingi ya familia? Kuna watoto wanaopata malezi tenge kwa kuzaliwa na kuishi katika familia zinazohudumiwa na mzazi mmoja? Hapa ni lini watoto hawa watajifunza kujadiliana na wenzi wao; kujadiliana na baba na mama zao? Haya ndiyo matatizo makubwa ya maisha ya ndoa na familia anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Baada ya kuwasili mjini Roma, Baba Mtakatifu Francisko alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, ili kutoa shukrani zake za dhati kwa Bikira Maria msaada wa Warumi, kwa tunza na ulinzi wake wa kimama! Itakumbukwa kwamba, hata kabla ya kwenda, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi iliyopita alikwenda Kanisa hapo ili kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wakati wa hija yake ya kitume Kisiwani Lesvos, Ugiriki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.