2016-04-18 09:28:00

Mh. P. Khaled Ayad Bishay ateuliwa kuwa Askofu wa Luqsor, Tebe, Misri


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia uteuzi wa Mheshimiwa Khaled Ayad Bishay kuwa Askofu wa Luqsor, Tebe, Misri uliofanywa na Sinodi ya Maaskofu wa Upatriaki wa Kanisa Kikoptik la Alexandria nchini Misri. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mtarajiwa Bishay alikuwa ni Afisa mwandamizi katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Baada ya kuteuliwa ameamua kuitwa Emmanuel.

Askofu mteule Emmanuel Bishay alizaliwa huko Kom Gharg, (Tema- Sohag) tarehe 5 Januari 1972. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 25 Septemba 1995 huko Kom- Gharib kwa ajili ya Jimbo la Sohag. Baadaye alipata nafasi ya kuendelea na masomo ya juu mjini Roma na hatimaye kujipatia shahada ya uzamili katika taalimungu maadili kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Alfonsianum, kilichoko mjini Roma pamoja na Shahada ya uzamili kwenye Sheria za Kanisa kutoka katika Taasisi ya Elimu ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya mashariki.

Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Jaalim wa maadili; mlezi Seminari kuu ya Maadi na Paroko wa Parokia ya Sohag. Kuanzia mwaka 2003 hadi uteuzi huu, amekuwa ni Afisa mwandamizi kutoka katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Amekuwa akitoa huduma yake ya kichungaji kwenye Parokia ya Mtakatifu Francisko Xsaveri huko Garbatella!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C. PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.